Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Karabaka kubadili upepo Simba?

Karabaka Simbaaa Karabaka kubadili upepo Simba?

Tue, 9 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Huenda usajili mpya wa winga wa Simba, Saleh Masoud ‘Karabaka’ kutoka JKU ukabadilisha upepo kuanzia miaka ya 2000 wa wachezaji wa Zanzibar kushindwa kutamba Msimbazi ikilinganishwa na Yanga pamoja na Azam FC.

Kuanzia miaka hiyo, Yanga na Azam zimebahatika kupata wachezaji kutoka Zanzibar waliodumu muda mrefu kutokana na viwango vyao bora, lakini imekuwa tofauti na Wekundu wa Msimbazi ambako ni nadra kuwaona wakifanya vizuri kiasi cha kuimbwa na mashabiki.

Baadhi ya nyota waliofanya vizuri Simba wenye asili ya Zanzibar kuanzia miaka hiyo ingawa sio wote walitoka moja kwa moja kwenye timu za Zanzibar, ni aliyewahi kuwa nahodha Nassor Masoud ‘Chollo’, Awadh Juma na Abdulhalim Humoud waliosajiliwa Msimbazi wakitokea Mtibwa Sugar msimu wa 2010/11.

Wakati Adeyun Saleh, Abdulaziz Makame na Mohamed Faki walicheza msimu mmoja tena kwa kiwango cha kawaida, huku timu hiyo msimu uliopita ilimsajili Mohamed Mussa kutokea Malindi FC, lakini aling’ara katika mechi dhidi ya Coastal Union tu katika Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC). Hata hivyo, Musa ambaye bado yupo Simba anayo nafasi ya atabadili upepo na kuwa nyota atayeimbwa na mashabiki wa Mnyama.

Kwa upande wake, Karabaka ambaye amesaini mkataba wa miaka mitatu Simba, dhidi ya timu yake ya zamani, JKU, alifunga bao zuri katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar katika ushindi wa mabao 3-1 walioupata.

Akizungumzia usajili wake Simba, Karabaka aliwaomba mashabiki wa Simba wamuamini kwani hawatawaangusha.

“Naomba mashabiki wa Simba waniamini, makocha waniamini, lakini bao langu (dhidi ya JKU wiki iliyopita) ni zawadi kwa mama yangu. Nimefurahi kuanza na mguu mzuri wa kufunga bao.”

YANGA

Kuna wachezaji kadhaa Yanga ambao waling’ara na kuimbwa na midomoni mwa mashabiki wa Jangwani akiwamo Abdi Kassim ‘Babi’ aliyeitumikia kuanzia 2007-2010 akitokea Mtibwa Sugar ambayo ilimsajili kutokea Mlandege, huku Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akitua 2006-2018 akitokea Malindi.

Hawa wote walitua kikosini wakiwa moto na waliingia kikosini moja kwa moja, ambapo kwa nyakati tofauti walisimama kama manahodha wa timu hiyo.

Mbali ya wakongwe hao, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ni usajili mwingine uliofanya vizuri Yanga msimu wa kwanza, licha ya baadaye kufunikiwa na waliomkuta. Ninja alitua akitokea Taifa Jang’ombe 2017-2019, na akiwa kikosini hapo alipata dili la kujiunga na MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech iliyomtoa kwa mkopo LA Galaxy II ya Marekani, kabla ya kurejea tena katika mwendelezo wa majina yaliyong’ara Yanga kutokea Zanzibar.

Na hivi sasa kuna Ibrahim Bacca aliyesajiliwa akitokea JKU. Huyu ni beki wa kati aliyetua msimu uliopita. Pia kuna Mudathir Yahya anayeichezea timu hiyo akitokea Azam FC.

Wengine waliong’ara na kuimbwa sana Yanga ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyetokea JKU, Abdulaziz Makame (Mafunzo), Adeyum Salehe, Mohamed Issa ‘Banka’, Haji Mwinyi Mngwali na msimu huu imemsajili Shekhan Ibrahim (JKU).

AZAM FC

Kwa upande wa Azam FC baadhi ya wachezaji ambao walifanya na wanafanya vizuri ndani ya kikosi hicho ni pamoja na nahodha mstaafu Agrey Morris, Abdallah Kheri ‘Sebo’, Mudathir (sasa yupo Yanga), Ahmed Selula (alishaondoka), Fei Toto na Babi (kastaafu).

WAKONGWE WANASEMAJE

Akizungumzia vipaji kutoka Zanzibar, Cannavaro aliwahi kusema: “Nidhamu na uvumilivu ndio siri ya mafanikio ya kuaminiwa Yanga na kupewa unahodha. Lazima wachezaji ambao wanapata nafasi wajue ukubwa wa majukumu ndani ya timu hizo.”

Naye Bacca alisema: “Sikuanza moja kwa moja kucheza. Nilivumilia na kujifunza na sasa naisaidia Yanga.”

Babi alisema: “Vijana wanaotoka Zanzibar wanaopata nafasi ya kucheza klabu za Yanga na Simba wasijisahau na kuvimba vichwa.”

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: