Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Julio amvulia kofia Benchikha

Julio Kocha.jpeg Julio amvulia kofia Benchikha

Thu, 21 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Aliyewahi kuwa Mchezaji na Kocha wa Simba SC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amemwagia sifa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha, kufuatia ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam juzi Jumanne (Desemba 19).

Ushindi huo umeifanya Simba SC ifikishe alama tano na kukaa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B nyuma ya vinara ASEC Mimosas yenye pointi 10.

Julio amesema mbinu zilizofundishwa na Benchikha ndio zilizoamua mechi hiyo ambayo matokeo yake yamefufua matumaini ya Simba kusonga mbele katika michuano hiyo ya kimataifa.

Beki huyo wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi pia alisifu kiwango kilichoonyeshwa na winga raia wa Cameroom, Essomba Onana, ambaye alipachika mabao yote mawili katika mechi hiyo.

“Kwa muda mfupi tu ameibadilisha Simba SC na kama atapata muda mrefu itakuwa timu ya kutisha zaidi, sio Tanzania, bali Afrika nzima, kuifunga Wydad Casablanca si jambo jepesi, ndugu zangu hizi timu za Waarabu siyo za mchezo mchezo, ni timu ngumu na nzuri ambazo mara nyingi zinachukua hivi vikombe vya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho,” amesema mchezaji huyo wa zamani wa Simba SC aliyeitumikia klabu hiyo kati ya mwaka 1980 hadi katikati ya 1990.

Ameongeza anaamini Simba SC itarejea katika ubora wake na kuwa tishio kwa sababu ya ujio wa kocha huyo mkongwe hapa barani Afrika.

Kuhusu Onana, Julio amesema anadhani Benchikha amembadilisha tofauti kocha aliyepita ambaye alimwacha afanye anavyotaka.

Tatizo la Onana ni kujinufaisha yeye na nadhani kocha wa zamani alikuwa hamkemei, huyu aliyekuja naona kama anamkemea na unaona amebadilika kwa vitu anavyovifanya, si mchezaji mbaya, ni mzuri,” amesema Julio.

Naye mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Sharaf Eldin Shiboub, alisema kocha Benchika ndiyo nyota wa mchezo katika mechi hiyo kwa sababu alichanga karata zake vizuri na alizuia kila kitu kipindi cha pili.

“Pongezi kwa wachezaji wote, walikuwa na viwango bora, lakini pongezi zangu kubwa na za dhati nizipeleke kwa Kocha Mkuu (Benchika), aliicheza mechi vizuri sana, hasa kipindi cha pili, alizuia kila kitu cha Wydad Casablanca,” amesema kiungo huyo ambaye kwa sasa anaichezea APR ya Rwanda na alikuja nchini kwa ajili ya kuangalia mechi hiyo.

Alimtaja Onana ni mchezaji mzuri na mwenye kipaji, lakini akaongeza mabao aliyofunga yametokana na ushirikiano wa wachezaji wote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: