Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jobe kabeba mbeleko mpya Simba

Jobe Simbaa (15).jpeg Jobe kabeba mbeleko mpya Simba

Mon, 5 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Dirisha dogo la usajili Simba walifanya uamuzi mgumu kwa kuachana na washambuliaji nyota, Jean Baleke na Moses Phiri.

Hakuna ambaye alifikiria kukatwa kwa Baleke licha ya kuwa na mabadiliko ya uchezaji, lakini kwa upande wa Phiri wengi waliamini hata asipoachwa na timu hiyo basi atavunja mkataba

Simba waliachana na washambuliaji hao wakiwa tayari wamejitengenezea majina ndani ya kikosi hicho, hivyo kuacha alama kwa wanachama na mashabiki wa timu hiyo.

Zilianza kama tetesi, lakini kisha ikawa kweli kwa kuthibitishwa na taarifa rasmi ya klabu kupitia kitengo cha habari.

Taarifa hiyo ilikuwa ni kubwa zaidi katika dirisha la usajili na ukubwa wake hasa ulitokana na mashabiki wa soka nchini kutaka kujua, kipi kinafuata baada ya Phiri na Baleke kupewa 'thank you'.

Katikati ya maswali na mjadala huo yakaibuka majina ya washambuliaji wawili, Freddy Koublan raia wa Ivory Coast na Pa Omar Jobe, raia wa Gambia ambaye leo hii ndiye tunamzungumzia.

Jobe ni mshambuliaji kiasili tangu alipotoka na ametua Simba akiwa amebeba matumaini lukuki ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.

Tayari ameshaanza kutumika ndani ya kikosi akiwa amecheza dakika 61, akifunga bao moja na alianza dhidi ya Tembo mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) akitumika kwa dakika 53 na kufunga bao kwenye ushindi wa mabao 4-0. Kisha aliopewa dakika nane dhidi ya Mashujaa ambapo Simba ilishinda bao 1-0.

Kabla ya kujiunga na Simba alikuwa akicheza Ligi Daraja la Kwanza nchini Kazakhstan katika timu ya Zhenis. Katika msimu ambao umeshamalizika wa ligi hiyo, Jobe alifunga mabao 13 katika mechi 25 alizocheza.

Namba zake zinashawishi kuamini kuwa huenda Simba wamepata mtu sahihi wa kufumania nyavu kama mwenyewe anavyojinasibu.

"Nimetoka Ulaya nimerudi Afrika katika timu ya Simba kwa ajili ya kuja kufanya kazi moja tu ya kufunga mabao ya kutosha," anasema Jobe, hiyo ikiwa ni baada ya kufunga bao la kwanza akiwa na jezi ya Simba kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya timu ya Tembo.

Hadi sasa Jobe ana bao hilo ikiwa tayari amecheza mechi yake ya pili ambayo ilikuwa ni ya ligi dhidi ya Mashujaa.

Kwa mujibu wa takwimu, bado mchezaji huyo yupo katika mstari mzuri lakini yeye mwenyewe anadai kuwa gari lake bado halijawaka.

Alipozungumza mara baada ya mchezo dhidi ya Tembo, Jobe anasema kuwa ana imani kubwa ya kufanya vizuri akiwa Tanzania, lakini kuna namna atahitaji muda wa kuyamudu mazingira ya hapa.

"Nilikotoka na hapa huna (Tanzania) kuna hali mbili tofauti za hewa. Ulaya kuna baridi sana, lakini hapa nimekuta hali ya joto. Nitafanya kila liwezekanavyo niweze kuzoea na hapo ndipo kiwango changu halisi kitaonekana," anasema.

Suala la kupewa muda ni kawaida kwa wachezaji kote duniani, lakini ishu inakuja kwamba Simba wameondoa watu wakiamini wanaokuja pia ni watu.

Kama unakumbuka Baleke wakati anajiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo msimu uliopita hakuhitaji sana muda, zaidi alianza kuwasha moto mapema tu katika mechi zake za mwanzo.

Pengine ni kutokana na aina ya mazingira aliyotoka nchini DR Congo hayana tofauti na hapa Tanzania, lakini kubwa zaidi tayari alikuwa na jamaa zake kama vile Henock Inonga ambao ni wenyeji ndani ya Simba wakiwa wanatoka taifa moja.

Hii ina tofauti kidogo na Jobe ambaye hatuna shaka kama anaweza kuwa ndiye raia wa kwanza wa Gambia kucheza Ligi Kuu Bara kwa mafanikio.

Bado kuna vitu vingi ambayo nyota huyo anatakiwa kuvizoea katika mazingira mapya ikiwemo vyakula, marafiki na hata aina ya soka la Bongo.

Hata hivyo wakati akiwa anajitafuta, lakini pia muda haupo pamoja na yeye wakati huu ambao ratiba za michuano mbalimbali zimepamba moto. Simba inakabiliwa na michuano ya ligi, ASFC pamoja na michuano ya kimataifa ambayo ndio haswa kocha Abdelhak Benchikha aliona kuna upungufu katika safu ya ushambuliaji na akaomba washambuliaji wapya.

Kwenye michuano ya ndani, Baleke na Phiri walikuwa wanafunga watakavyo, lakini takwimu zao kwenye mechi za kimataifa hazikuwa nzuri. Si Phiri wala Baleke ambaye aliweza kufunga bao kwenye mechi za kimataifa msimu huu.

Hivyo, ujio wa Jobe umebeba matumaini makubwa kwa wana Simba ambapo sasa wanaamini kile ambacho alishindwa kufanya Phiri na Baleke yeye ataweza kufanya.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: