Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Humtaki Robertinho ? Hiki ndicho kinachombeba Simba

Robertinho Mtego.jpeg Robertinho akiwa na viongozi wa Simba baada ya kunyakua Ngao ya Jamii

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huku kwenye mitandao ya kijamii kuna kelele nyingi za mashabiki na wapenzi wa Simba juu ya Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Wanasema Simba inashinda mechi zake, lakini hawana imani na kocha huyo kutoka Brazili. Mwanaspoti limekuwa likipokea maoni ya wasomaji ambao ni mashabiki wa klabu hiyo, wakitaka mabosi wa Simba kumrudisha Mgunda ili aendelee kuwa kocha msaidizi wa Robertinho mambo yawe mepesi.

Wapo wanaotaka hata ikiwezekana atimuliwe kabisa kwa madai anawapa presha timu inapocheza, lakini ukweli ni kwamba kocha huyo Mbrazili anabebwa na namba ndani ya timu hiyo, kwani rekodi zimemfanya awafunike makocha karibu watano waliomtangulia akiwamo Mgunda mwenyewe.

Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2019, Simba imenolewa na makocha tofauti sita, huku jamaa akifunika kwa matokeo aliyopata katika mechi 13 alizoiongoza timu hiyo tangu alipojiunga nayo Januari mwaka huu.

HUU NDIO UKWELI

Robertinho alitua Simba Januari 3 akimpokea Mgunda aliyekuwa amekaimu nafasi ya kocha mkuu tangu Zoran Maki alipojiondoa Septemba 6 mwaka jana na hadi sasa amekamilisha jumla ya mechi 13 katika Ligi Kuu Bara akishinda 11 na kutoka sare mbili, hajapoteza mchezo wowote.

Katika ligi ya msimu huu amecheza mechi mbili zote ameshinda na kuifanya timu ikae kileleni ikiwa na pointi sita na mabao sita, ikiruhusu mawili tu. Ilianza kwa kuifumua Mtibwa Sugar 4-2 kisha Dodoma Jiji 2-0.

Wakati msimu uliopita mwamba huyo, katika michezo 11 aliyoongoza Simba kushinda 3-2 dhidi ya Mbeya City, kisha Dodoma Jiji kwa bao 1-0, Singida Big Stars 3-1, Mtibwa (3-0), Yanga 2-0, ikiwa ni ushindi wa kwanza wa Simba tangu Februari 16, 2019 dhidi ya watani zao.

Pia, iliichapa Ruvu Shooting 3-0, Polisi Tanzania 6-1 na ikamalizia msimu huo wa 2022-2023 kwa kuinyoosha Coastal Union kwa mabao 3-1 japo Mnyama ilimaliza bila kutwaa taji lolote.

Michezo ambao aliiongoza timu hiyo kutoka sare ni ile ya Azam FC na Namungo ambao yote iliisha kwa 1-1 na kupitia michezo yote 13 aliyoiongoza Simba, Robertinho amevuna jumla ya mabao 32 ikiwa ni wastani wa mabao 2.5, na akiruhusu tisa tu. Simba ya Robertinho ndio iliyofunga mabao mengi zaidi tangu 2019 kulinganisha na watangulizi wake.

Sven Vandenbroeck

Baada ya Simba kuachana na Patrick Aussems ilimpa kazi Mbelgiji, Sven aliyechukua mataji matatu akianza na taji la Ngao ya Jamii 2020, pia Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) msimu wa 2019/2020.

Sven alianza kazi rasmi Simba Desemba 12, 2019 na katika michezo yake 13 ya mwanzo alishinda 11, sare mmoja na kupoteza mmoja.

Michezo aliyoshinda ni (4-0) v Lipuli, (0-2) v KMC, (2-0) v Ndanda, (2-1) v Mbao, (4-1) v Alliance, (3-2) v Namungo, (2-0) v Coastal Union, (2-1) v Polisi Tanzania, (3-0) v Mtibwa Sugar, (0-1) v Lipuli na (1-0) v Kagera Sugar.

Mchezo wa sare ni wa (2-2) v Yanga huku ule wa kichapo ni ule wa (1-0) kutoka kwa JKT Tanzania ambapo kiujumla katika michezo hiyo, timu hiyo ilifunga mabao 28 na kufungwa manane.

Didier Gomes da Rosa

Mfaransa huyu alijiunga na Simba, Januari 24, 2021 akichukua nafasi ya Sven aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco na katika michezo yake 13 ya mwanzo, aliiongoza timu hiyo kushinda 11 na kutoka sare miwili huku akiwa hajapoteza hata mmoja, akiwa sambamba na Robertinho.

Gomes alishnda 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji, Biashara United 1-0, JKT TZ kwa 3-0, Mtibwa Sugara 5-0, Mwadui (1-0), Kagera Sugarv (2-0), Gwambina (1-0), Dodoma Jiji (3-1), Namungo (3-1), Ruvu Shooting (3-0) na Polisi Tanzania (1-0).

Michezo iliyoisha kwa sare ni ile ya Azam FC iliyotoka nao 2-2 na Tanzania Prisons 1-1, huku safu ya washambuliaji wakifunga mabao 28 na kuruhusu sita tu.

Pablo Franco

Raia huyo wa Hispania alitambulishwa Simba Novemba 8, 2021 akitokea Ligi Kuu ya Kuwait ya Al-Qadsia akichukua nafasi ya Didier Gomes aliyetimuliwa baada ya kuondoshwa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Katika michezo yake 13 ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara, Pablo alishinda tisa tu, sare miwili na kuchezea kichapo mara mbili.

Michezo aliyoshinda ni (3-1) dhidi ya Ruvu Shooting, Geita Gold (2-1), KMC (1-4), Azam FC (2-1), Tanzania Prisons (1-0), Mbeya Kwanza (1-0), Biashara United (3-0), Dodoma Jiji (2-0) na Coastal Union (2-1) na alizopoteza dhidi ya Mbeya City (1-0) na Kagera Sugar (1-0) na suluhu dhidi ya Yanga na Mtibwa Sugar na timu ilifunga jumla ya mabao 20 na iliruhusu saba tu.

Zoran Maki

Kocha huyu kutoka Serbia na Ureno alitua Msimbazi Juni 28, 2022 akimpokea Pablo Franco, hata hivyo alikaa Simba muda mfupi mno hakufikisha mechi 13 kama wenzake walimtangulia.

Zoran alijiondoa ghafa Simba Septemba 6 kwa kile kilichoelezwa na aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez kufikia makubaliano ya pande mbili ya kusitisha mkataba wa mwaka mmoja aliousaini, na siku hiyo hiyo akatambulishwa Al Ittihad ya Misri.

Kocha huyo aliiongoza Simba katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara ambazo zote alishinda akianza na mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold kisha ikaifumua Kagera Sugar 2-0 na kukusanya jumla ya mabao matano na bila wavu wake kuguswa.

Juma Mgunda

Mara alipoondoka Zoran, Simba ilimtangaza Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda Septemba 7, 2022. Katika michezo 13 ya Ligi Kuu Bara ambayo aliiongoza Simba kushinda mechi tisa, sare tatu na kupoteza mmoja. Michezo ya ushindi ni (1-0) v Tanzania Prisons, (3-0) v Dodoma Jiji, (5-0) v Mtibwa Sugar, (1-0) v Ihefu, (1-0) v Namungo, (4-0) v Ruvu Shooting, (3-1) v Polisi Tanzania, (3-0) v Coastal Union, (5-0) v Geita Gold.

Sare ni (1-1) v Yanga, (1-1) v Singida Big Stars, (1-1) v Mbeya City wakati ule wa kichapo ni (1-0) v Azam FC.

Katika michezo hiyo aliyoongoza Mgunda timu hiyo ilifunga mabao 29 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano. Kabla ya Mgunda kuachana na timu hiyo aliiongoza katika michezo 16 ya Ligi Kuu Bara na kushinda 11, sare minne na kupoteza mmoja tu huku akiiwezesha kutinga hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

MSIKIE ROBERTINHO

Akizungumzia mwenendo wake kwenye Ligi Kuu Bara, Robertinho alisema siri ya mafanikio ni staili ya kucheza soka la kushambulia.

“Binafsi napenda kuona siku zote timu ikicheza kwa kushambulia na kucheza katika nusu ya mpinzani mara kwa mara, hii ni mojawapo ya kati ya njia bora kwetu wakati tukimiliki au tukiwa hatuna mpira,” alisema Robertinho ambaye amekuwa na benchi jipya kabisa la ufundi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: