Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Himid Mao: Mabeki hawampendi Kibu

Kibu D KIBU DENGA.jpeg Kibu Denis.

Fri, 18 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ipo kauli moja inayosema ‘Muomba Mungu hachoki’ na ile inayosema mafanikio ya mtu yapo tu ila kuna siri kubwa mpaka mtu kufikia ndoto zako.

Kwa kila kijana hususan wachezaji wanakuwa na stori zenye kusisimua mpaka kufikia malengo yao.

Mwanaspoti limepata bahati ya kuzungumza na kiungo wa zamani wa Azam FC ambaye msimu huu atakipiga Tala’ea El Gaish SC ya Misri kutoka Ghazl El Mahallah iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Misri, Himid Mao.

Amefunguka mambo mengi ikiwa ni pamoja na maisha yake Misri akiweka wazi siku yake ya kwanza kuanza majukumu namna alivyochelewa mazoezini.

“Nilikutana na mazingira magumu miezi mitatu ya mwanzo hii ni kutokana na kuto kuzoea hali ya hewa na mazingira;

“Nakumbuka siku ya kwanza mazoezini nilichelewa kuamka kwasababu ya mazoea na nchi yangu ambapo tulikuwa tunafahamu muda wa kuamka. Nilichelewa dakika 15 zilinitoa mchezoni kwasababu sikujisikia vizuri kuanza na mguu mbaya,” anasema.

Himid anasema baada ya kuanza kuzoea alikuwa anaamka mapema na kufika kwa wakati mazoezini huku akithibitisha ukichelewa mazoezi unakatwa mshahara na hakuna masuala ya kuingia kambini kama Tanzania.

“Tukitoka mazoezini kila mtu anarudi kwake tunakutana siku moja kabla ya mechi ila kukiwa na mchezo nje ya uwanja wetu wa nyumbani ndio tunakutana siku mbili kabla ya mchezo kwaajili ya safari lakini tukitoka huko kila mmoja anarudi kwake,” anasema Himid ambaye pia anadai hata muda wa kukaa pamoja kuzungumza mambo nje ya soka ni lazima upangwe.

UKIONGEZEKA KILO UMEKWISHA

Soka la Tanzania linazidi kukua kadiri miaka inavyozidi kusonga ukitaka kuthibitisha hilo ni namna mastaa kutoka mataifa mbalimbali wanavyomiminika kuja kucheza lakini kuna vitu bado haviwabani kama anavyothibitisha Himid.

“Soka la kulipwa katika mataifa mengi yaliyoendelea lina vipengele vigumu mfano Misri nimecheza misimu sita sasa kuna vipengele vigumu sana tofauti na Tanzania;

“Kule mchezaji ukichelewa mazoezini, ukiongezeka kilo ukicheza michezo michache tofauti na makubaliano unakatwa mshahara, hayo ni makubaliano;

“Kitu kizuri ni kwamba kama umepewa mkataba na makubaliano ni kucheza basi una kila sababu ya kuhoji kwanini haupangwi wakati mkataba unakutaka ucheze hili ndio zuri kwa upande wetu nafikiri ndio maana hata mimi napata sana nafasi ya kucheza,” anasema kiungo huyo ambaye amekiri kuwa hajawahi kubaguliwa akiwa Misri.

KIBU NI MCHEZAJI WA KISASA

Kibu Denis ambaye anazungumzwa sana na mashabiki pale anapokosea tu, lakini akifanya vizuri hakuna anayemzungumzia lakini Himid Mao ameibuka na kumsifia mchezaji huyo.

“Kwasasa namkubali sana mshambuliaji wa Simba, Kibu ni mchezaji ambaye kila kocha anahitaji wachezaji aina kama yake hawezi kumuacha;

“Kibu ni aina ya washambuliaji ambao wanatumia nguvu na ni watata kwa mabeki ukikaa na mabeki ukawauliza hawawezi kuacha kumtaja kwasababu ana kasi na nguvu na mabeki hawapendi kukimbizwa sana,” anaongeza.

BACCA, MWAMNYETO HAO MISRI

Mabeki wa kati wa Yanga na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambao wameonyesha uwezo mkubwa ndani ya misimu miwili iliyoisha na kuisaidia timu yao kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara, Ngao na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) wamemkosha Himid.

“Ikitokea nikapata nafasi ya kupendekeza majina mawili au moja ya nafasi ya beki kwa upande wangu siwezi kuwaacha Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ kutokana na uwezo walionao;

“Ni wachezaji wazuri wapambanaji ukicheza nao unajua kuna watu wapambanaji nyuma wanauwezo wa kumkinga kipa, hivyo ni wazi hata kocha ambaye nitampa majina yao hawezi kuwakataa wanaweza kupanda na kushuka pamoja na kucheza beki ya kati.” anasema Himid.

KUPATA LESENI MTIHANI

Kila nchi ina utaratibu wake wa kuendesha Tanzania ili umiliki leseni ni wepesi wako wa kuelewa darasani lakini kwa Misri, Himid amesema ni changamoto.

“Nina maisha mazuri Misri nimekabidhiwa kila kitu naishi nyumba nzuri nina gari zuri hii ni kwa mujibu wa mkataba wangu;

“Mkataba wangu unanitaka nipewe mahitaji yote muhimu na natakiwa kuutumikia kwa kupata nafasi ya kucheza, hivyo sina changamoto yoyote kwa vitu vya kujikimu,” anafafanua.

Mao anasema pamoja na kumiliki gari zuri lakini hana uwezo wa kuliendesha kwasababu ameshindwa kupata leseni hivyo ameajiri mtu wa kumuendesha.

Anasema Misri wanaangalia mapato zaidi kuendelea kubaki kwenye nchi yao, hivyo sio rahisi kuona mgeni anapata njia zote za kujiendesha.

AUCHO, BAJANA HATARI

Himid anawataja viungo wake bora wanaocheza nafasi yake.

“Tanzania imebarikiwa kuwa na viungo wengi wenye uwezo mkubwa navutiwa sana na Kelvin Nashon (Mtibwa Sugar)huyu ni mchezaji wangu bora kwenye kizazi cha sasa anajua kucheza;

“Mzamiru Yassin (Simba), Sospeter Bajana (Azam FC), Mudathir Yahya (Yanga), Jonas Mkude japo msimu ulioisha hakuwa na mechi nyingi lakini ni kiungo wangu bora pia,” anasema Himid ambaye amemtaja Khalid Aucho kuwa ni mzuri huku akikiri ni aina ya wachezaji waliotakiwa kucheza Tanzania ili kukuza vipaji.

MASTRAIKA

Utawala wa John Bocco kwenye eneo la ushambuliaji unaelekea mwisho kutokana na umri kumtupa mkono lakini hadi sasa hakuna staa mwingine ambaye anaweza kumrithi kutokana na wachezaji kuibuka na kupotea kiungo Himid anafunguka sababu za kutokuzalishwa kwa washambuliaji wengi.

“Tanzania imebarikiwa kutengeneza wachezaji wanaocheza nafasi ya kiungo kwa wingi hii ni kutokana na nafasi hiyo kuchezesha wachezaji zaidi ya watatu kiwanjani tofauti na washambuliaji;

“Timu nyingi zinatumia sana mshambuliaji mmoja na kujaza viungo ndio sababu ya wachezaji kuchagua kucheza nafasi ya kiungo,” anasema.

Himid anasema shida wachezaji wanaocheza nafasi ya ushambuliaji kuwa ndogo inatokana na wachezaji kuamua kucheza nafasi ambazo wanauhakika wa kupata namba za kucheza mara kwa mara.

AJAZA FAMILIA MWILINI

Ni wachezaji wachache wazawa ambao wamechora tattoo kwenye miili yao na baadhi ya waliochora ni wale wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi Mwanaspoti limeona kwa Himid ambaye amefunguka maana ya tattoo zake.

“Nimechora tattoo saba zote zina maana kwasababu nimechora majina ya familia yangu;

“Nina tattoo ya jina la mama, baba, mke, watoto na tarehe na mwaka wa siku nilipofunga ndoa,” anasema.

ELFU TANO HADI LAKI 2

Soka ni mchezo wa wazi ambao unatazamwa na watu wengi kutokana na kupendwa kuna wadau wa soka wanaenda kuangalia mpira wakiwa wanafahamu aina ya viatu na bei zake Himid anasema viatu ni silaha mojawapo ya kumfanya mchezaji kuwa kwenye hali nzuri.

“Nakumbuka kiatu changu cha kwanza kuvaa cha mpira nilinunua Karume kwa Sh 5,000 nilikitumia kwa muda hii ni kutokana na hali ya kiuchumi;

“Familia yangu ilikuwa inanipa ushirikiano kwa kuninunulia vifaa vya mpira hilo lilinifanya nivae hadi vya Sh30,000;

“Lakini kwasasa napambana na nachezea kiatu hadi cha Sh200,000 aina ya Mercurial na Nike,” anafunguka.

NYEKUNDU NI BARA TU

Ukitaja majina ya viungo walio na kadi nyingi nyekundu wanaocheza nafasi ya kiungo huwezi kuacha kumtaja Himid.

“Sina kumbukumbu nzuri lakini nadhani ni kati ya kadi sita hadi saba hazizidi hapo nikiwa Ligi Kuu Bara tu lakini huwezi amini miaka yangu sita Misri sijapewa kadi nyekundu;

“Naweza kusema labda akili ya mpira imepevuka nakua zaidi hilo ndio linanifanya nicheze mpira kiakili zaidi maana sina kadi hata moja nyekundu,” anasema kiungo huyo ambaye amekiri kuwa kwa upande wa Misri hakuna mchezaji anaweza kuja kucheza huku zaidi wanapenda vaibu la mashabiki wanavyojazana uwanjani tofauti na kwao wanazuiwa kutokana na vurugu zao.

AZAM, MTIBWA ZIPEWE MAUA YAO

Himid amezisifu timu hizo kwa kuzijali timu za vijana na kutaka zipewe maua yao.

“Tangu nikiwa Azam FC na kuondoka kinachonifurahia hadi sasa ni namna wanavyowaamini vijana.

“Sio Azam tu Mtibwa Sugar pia inatakiwa kupewa maua yao ni timu ambao inaamini katika damu changa na kutengeneza wachezaji wengi wazuri miaka ya mbele ambao wanatumika kwenye timu za taifa,” anasema Himid ambaye amesema anafurahia kila dakika ya maisha yake ndani ya Azam FC timu iliyomkuza kisoka.

ITAENDELEA KESHO

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: