Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiki ndicho kilichojiri kikao cha Wachezaji, Viongozi Simba SC

Wajumbe Wa Bodi Simba Wakutana Na Wachezaji.jpeg Hiki ndicho kilichojiri kikao cha Wachezaji, Viongozi Simba SC

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huko Simba mambo bado sio shwari, kwani mara baada ya timu kulazimishwa sare ya 1-1 na Asec Mimosas ya Ivory Coast, viongozi wa klabu hiyo waliamua kuwazukia mastaa wa timu iyo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kujifungia kwa zaidi ya saa mbili na nusu wakipeana makavu laivu.

Simba ililazimishwa sare hiyo kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa juzi jioni Kwa Mkapa, Wekundu hao wakipata penalti katika kipindi cha kwanza kupitia Saido Ntibazonkiza, huku wageni wakisawazisha bao hilo dakika ya 77 na kuifanya Simba ipate sare ya tano mfululizo msimu huu kwenye michuano ya kimataifa ikiwamo na ile ya African Football League.

Mara baada ya mchezo huo, huku mashabiki wakionekana kuwa na hasira na kuwazomea wachezaji, ambao wakiwa vyumba vya kubadilishia nguo ili watimke zao, walishtukizwa na ugeni wa mabosi wa klabu hiyo ambao walianza kwa kuwawakia kwa kile walichokionyesha uwanjani kabla ya mastaa nao kujibu mapigo.

Habari kutoka ndani ya chumba hicho, kinasema baadhi ya wachezaji waliwapasha viongozi kuwa kama wanaamini kuna wachezaji wanaoihujumu timu ni bora wawatimue kwani inawapa wakati mgumu wenye moyo wa kujituma uwanjani.

Mabosi wa Simba wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’, Mtendaji Mkuu wa klabu, Imani Majula na wajumbe wa bodi akiwamo Issa Masoud wanatajwa ndio waliokuwa wasemaji wakuu kwenye kikao hicho, huku mmoja wa mastaa wa timu hiyo (jina tunalo) aliamua kujivika mabomu na kuhoji viongozi kama wana ushahidi wa tuhuma kwa wenzao kwanini hawawaadhibu.

“Viongozi waliingia na kuanza kufoka hasa (anamtaja jina), ila wachezaji nao waliamua kufunguka ambapo (anamtaja kiungo mshambuliaji), aliamua kuhoji kama kuna tatizo kwanini wahusika hawawajibishwi. Pia alisema wachezaji wenzao wamevunjika moyo kwa tuhuma hizo na kusababisha kuwaangusha wenzao kikosini,” kilisema chanzo kutoka kikaoni ambaye pia ni mchezaji aliyeongeza;

“Jamaa alihoji wamezuiwa chumbani hadi usiku mwingi wakati walitakiwa waende makwao kupunguza stresi za matokeo kwa kuziona familia zetu, akifunguka pia tabia ya baadhi ya viongozi kuwaogopa mastaa hasa wenye majina makubwa. Kifupi kikao kilikuwa moto na kiliisha usiku kabla ya timu kutakiwa kambini, kwa nia ya kusubiri kocha (Abdelhak) Benchikha tuliyeambiwa ataingia leo (jana) ili azungumze nasi kabla ya safari ya Botswana.”

Mbali na hilo taarifa nyingine kutoka kwenye kikao hicho kinasema kuwa, matokeo hayo ya sare yameongeza kasi ya panga linalotarajiwa kupitishwa na mabosi kupitia dirisha dogo litakalofunguliwa Desemba 16, japo wengine watapona kutokana na mikataba waliyonayo.

Kikao hicho kilichokuwa chini ya ulinzi mkali wa makomandoo wa Simba waliokuwa wamekaa kila kona ili kuzuia mtu yeyote asiyehusika kusikia kinachozungumzwa, kilikuwa na lengo la kuamsha morali kwa wachezaji, huku wenyewe wakitaka waletewa mtu wa Saikolojia.

“Kilikuwa ni kikao kizito aisee, viongozi kila mmoja alitoa picha kamili ya jinsi timu ilivyo na presha iliyopo nje na ndani ya uwanja, wengine kwenda mbali na kusema lazima maamuzi magumu yafanyike siku chache zijazo,” kilisema chanzo hicho kingine (jina tunalo).

“Wachezaji nao walisema wanahisi wanaangushwa na wenzao, pia wapo wanaoona wanaonewa na waliokuwa tayari kuvunja mikataba waondoke. Yaani unavyoona presha kwa mashabiki ndivyo ilivyo na kwa wachezaji,” kilieleza chanzo hicho na kuongeza;

“Matokeo haya yamemvuruga kila mtu na viongozi wapo tayari kumuondoa yeyote anayeonekana kukwamisha malengo ya timu, dirisha dogo sio chini watu 10 au nane wanafyekwa.”

Inaelezwa hata hivyo, hatma ya wachezaji hao itategemea kikao cha kocha Benchikha baada ya kutua na kufanya tathmini na mapendekezo ya nani atoke na nani abaki, kisha lipite panga hilo.

Miongoni mwa wanaodaiwa kukalia kuti kavu kwa sasa ni mastaa 14 akiwamo nahodha John Bocco, Luis Miquissone, Mohamed Mussa, Jimmyson Mwanuke, Shaaban Chilunda, Clatous Chama, Saidi Ntibanzokiza, Shomari Kapombe, Aubin Kramo, Hussein Abel, David Kameta ‘Duchu’, Nassoro Kapama, Abdallah Ismail na Ayoub Lakred, ila wanasubiri mchujo, muda na ripoti ya kocha.

Hakuna kiongozi yeyote wa Simba aliyepatikana kuthibitisha taarifa za kikao hicho kilichofanyika Kwa Mkapa na kwenda kumalizikia kambini kwani simu zao zilikuwa zikiita tu bila kupokelewa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: