Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haijaisha hadi iishe

Kumekucha Mapinduzi Cup! Simba, Yanga Ndani! Haijaisha hadi iishe

Mon, 1 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wikiendi ilikuwa ya moto kwa mashabiki wa soka nchini kutokana na kile kilichozikumba timu za Simba na Yanga katika michezo ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Simba ilianza kutupa karata Ijumaa na kulala bao 1-0 mbele ya Al Ahly na juzi ilikuwa zamu ya Yanga iliyojitutumua na kulazimisha suluhu mbele ya mabingwa wa AFL, Mamelodi Sundowns na sasa zina kubarua kigumu kwa mechi za marudiano zitakazopigwa Ijumaa hii jijini Cairo na Pretoria mtawalia.

Licha ya matokeo hayo yasiyoridhisha kwa timu hizo, lakini makocha wa timu zote wameweka bayana kwamba mechi hizo hazijaisha hadi ziishe kwani wana dakika 90 nyingine za kutafakari ili kuamua hatma ya kwenda nusu fainali au zikubali yaishe na kurudi kucheza michuano ya ndani.

Michezo hiyo miwili ya robo fainali ilichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, huku ikizua maswali mengi juu ya kitu kilichozizuia timu hiyo kupata ushindi licha ya kuwabana wageni kwa sehemu kubwa ya dakika 90 kwa kila mmoja.

Mashindano ya Afrika mara nyingi timu zimekuwa zikifaidika zaidi zinapocheza kwenye uwanja wa nyumbani, tofauti na zilivyo timu za Ulaya, hivyo kwa sasa Simba itakuwa na kazi jijini Cairo, Misri kusaka rekodi mpya ya kushinda mbele ya Al Ahly ikiwa kwao, hali ilivyo pia kwa Yanga pale jijini Pretoria, Afrika Kusini itakapoikabili Mamelodi ambayo rekodi kwa mechi za nyumbani ni nzuri kwao.

Hapa chini ni baadhi ya mambo yaliyojitokeza kwenye mechi hizo na kuibua maswali, lakini mwisho ni kwamba timu zote za Simba na Yanga zina kila sababu ya kujipanga upya ili kwenda kupambana kumalizia dakika 90 zilizosalia kwa kila mmoja kwani hizi mechi hazijaisha hadi ziishe.

MASHABIKI FRESHI

Jambo pekee ambalo unaweza kufanya ni kuwapongeza mashabiki wa timu zote kuhakikisha Uwanja wa Mkapa unajaa na wote walionekana kuwa na nia moja ya kuziunga mkono timu zao.

Simba viingilio vyao vilianzia Sh5,000 hadi Sh250,000 na ikaujaza Uwanja wa Mkapa, hivyo kwa hali ya kawaida timu hiyo itakuwa imekusanya fedha ndefu, wakati Yanga haikuwa na kiingilio kwenye eneo la mzunguko ambalo lina zaidi ya watu 45,000 lakini katika VIP A iliweka kiingilio cha Sh30,000, VIP B Sh20,000 na VIP C Sh10,000.

USAJILI TATIZO

Katika michezo yote miwili, bado wachezaji ambao walisajiliwa kwenye dirisha dogo ili kuzisaidia timu hizo kwenye michezo hii muhimu hawakuwa na faida.

Simba kwenye dirisha dogo iliwasajili wageni, Fred Michael, Pa Omar Jobe kwenye eneo la ushambuliaji pamoja na Babacar Sarr katika eneo la kiungo.

Hata hivyo, ni Sarr pekee ndiye ameonekana kupata nafasi kwa kocha wa Simba, Abdelhack Benchikha, huku Fred na Jobe wakiwa hawana faida.

Benchikha alimtumia Jobe katika dakika 10 za mwisho pamoja na kwamba timu hiyo uwanjani haikuwa na mshambuliaji asilia, lakini aliwaweka wawili hao nje kwenye mchezo ambao timu yake ilihitaji mabao mengi.

Lakini kwa upande wa Yanga, kocha Miguel Gamondi hajaona faida ya wachezaji wake wawili ambao aliwasajili kwenye dirisha hilo, Joseph Guede na Augustine Okrah ambao waliingia mwishoni.

Kwa uhalisia, Yanga ilihitaji ushindi kwenye mchezo huu na hivyo kama washambuliaji hao wangekuwa na ubora basi wangeanza kwenye mechi hiyo ambayo Yanga ilikuwa na kundi kubwa la wachezaji wenye majeraha.

Kama makocha hawa ndiyo waliwapendekeza wachezaji hao, basi kosa ni la kwao, kama sio ni viongozi wajitafakari.

YANGA MATATU, SIMBA MOJA

Kitendo cha Simba kupoteza kwa bao 1-0 kinazidi kuiweka timu hiyo kwenye wakati mgumu kwa kuwa itatakiwa kuibuka na ushindi kama huo ugenini ili iende kwenye matuta, lakini suluhu ya Yanga inaweza kuwa na faida kubwa kwao kwa kuwa inaweza kukaa nyuma na kuhakikisha timu yao hairuhusu bao lolote na kwenda kwenye mikwaju ya penalti.

Hivyo kwa Yanga wana mambo matatu ambayo ni faida kwao ambayo ni; sare ya mabao yoyote na ushindi, hivi vyote vitawapeleka nusu fainali wakati la tatu la kulazimisha suluhu nyingine ambayo itawapeleka kwenye kupigiana matuta, huku Simba ikilazimika kuwa na jambo moja tu ambalo ni ushindi.

MBINU ZA WAGENI

Staili ya kucheza kwa Mamelodi ilionyesha dhahiri kuwa waliiheshimu Yanga lakini wakiwa wanafahamu ni kitu gani wanataka, ndiyo maana muda mwingi walikuwa wakicheza kwenye eneo lao la ulinzi bila wasiwasi wowote ikiwataka Wananchi waende kufukuzia mpira, lakini Wanajangwani walionekana kutambua kuwa huo ulikuwa ni mtego.

Pamoja na kwamba Mamelodi imeongoza kwa umiliki wa mpira, lakini faida hiyo wameipata kwenye eneo lao na siyo lile la Yanga kwa kuwa ndiyo sehemu ambayo walikuwa inawapa uhuru wa kukaa na mpira kwa muda mrefu.

Vivyo hivyo, hata upande wa Simba, baada ya Ahly kufunga bao waliiachia Simba mpira na kurudi nyuma kujilinda.

Kilichoonekana kwenye mchezo huo ni tofauti ya ubora wa klabu hizo na hata kwa mchezaji mmoja mmoja huku uzoefu ndio ulioamua mechi, kwani Simba ilitengeneza nafasi nyingi, lakini ilishindwa kuzitumia na wenzao waliitumia moja na kuwatosha kutoka na ushindi wa kwanza ugenini dhidi ya Mnyama katika mechi zote za CAF walizowahi kukutana kuanzia mwaka 1985.

VAR ILIKUWA LIKIZO

Kwenye michezo yote miwili yaani dakika 180, hakuna mwamuzi hata mmoja ambaye aliondoka kwenda kwenye eneo la usaidizi wa waamuzi yaani VAR ikiwa ni nadra sana kutokea kwenye michezo mingine kama hiyo.

Ajabu ni kwamba katika mechi ya Simba kulikuwa na matukio mawili yalistahili kwenda kuangaliwa katika VAR na kufanyiwa uamuzi ikiwamo kitendo cha mabeki wa timu zote kuwaangusha wachezaji wa timu pinzani ndani ya eneo la hatari, lakini mwamuzi Abongile Tom wa Afrika Kusini hakuwa na taimu.

INAWEZEKANA JAPO NGUMU

Simba na Yanga zote zinaweza kuibuka na ushindi kwenye michezo ijayo kama zitafanya maandalizi mazuri kwenye kipindi cha wiki moja ambacho kimebaki kwa kuwa hakuna kinachoshindikana kwenye soka.

Kocha Benchikha wa Simba na Miguel Gamondi wa Yanga wamekiri mechi za nyumbani zilikuwa ngumu na hata za ugenini hazitakuwa rahisi, lakini wanaenda kujipanga na kurekebisha kila dosari ili wapindue meza ugenini kwani mechi hizo hazijaisha licha ya matokeo ya Kwa Mkapa.

Hata hivyo, Simba na Yanga zinapaswa kurekebisha kila dosari zilizoonekana kwenye mechi hizo za nyumbani, kwani ugenini kunaweza kuwa kugumu kwa rekodi na aina ya soka linalochezwa na timu wenyeji wanapokabiliana na wapinzani wakiwa nyumbani.

Mamelodi katika mechi tisa za CAF tangu Aprili mwaka jana imeshinda saba nyumbani na kutoka sare mbili bila kupoteza, ikifunga mabao 13 na kufungwa matatu tu, lakini Al Ahly tangu Mei mwaka jana katika mechi za mashindano yote ilizocheza haijapoteza zaidi ya kushinda 19 na sare tano.

Hata hivyo, mechi pekee iliyochezwa Saudi Arabia ikiwa ni ile ya Caf Super Cup wao wakiwa wenyeji ndio walipoteza kwa bao 1-0 mbele ya USM Alger ya Algeria iliyokuwa ikinolewa na Benchikha ambaye baada ya mchezo huo alijiuzulu na kuibukia Simba.

TUIKATAE BURE

Ni dhahiri kuwa Yanga inatakiwa kutazama tena utaratibu wa kuwaacha mashabiki wakaingia uwanjani bure kwa kuwa ni jambo linaloleta usumbufu kwa wale ambao wamekuwa wakinunua tiketi, lakini inapoteza ile heshima ya mechi kubwa kama hiyo.

Pamoja na kwamba Yanga ilijaza Uwanja wa Mkapa lakini kumekuwa na malalamiko makubwa kwa baadhi ya mashabiki ambao walikata tiketi zao kwa ajili ya kwenda kutazama mchezo huo baada ya kukosa nafasi hiyo.

Baadhi ya mashabiki ambao walikuwa na tiketi za Sh10,000 walishindwa kuingia uwanjani baada ya kuelezwa kuwa uwanja umejaa, lakini pia hali hiyo ilisababisha askari watumie nguvu kubwa kuwatoa wale waliokuwa wamejaa kwenye geti wakilazimisha kuingia. Matumizi ya mabomu ya machozi yaliwazuia wengine walionunua tiketi kuiona timu yao.

Hatua ya robo fainali kwa Yanga ambayo ina mastaa wakubwa kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Aziz Ki, Djigui Diarra na hata Dickson Job haihitaji mashabiki kuelezwa kuwa kiingilio ni bure, bali wenyewe wangekata tiketi ya kwenda bila kusukumwa, inaonekana kama itatokea hivi tena basi utaratibu mzuri uwekwe.

SIMBA KADI 17

Simba ndiyo timu inayoonekana kuwa na nidhamu mbovu zaidi baada ya kukusanya kadi za njano 17 hadi sasa kuanzia hatua ya makundi, huku kiungo wake Sadio Kanoute akiwa nazo nne.

Hii sio ishara nzuri ya nidhamu klabuni, lakini jambo la ajabu ni kwamba mechi ijayo zinakutana timu ya kwanza kwa kadi na ya pili kwa kuwa Ahly nayo inazo 14, ikiwa nafasi ya pili kwa nidhamu mbovu.

YANGA JUU YA MAMELODI

Yanga imeonekana kucharuka ghafla na sasa inaongoza kwenye timu iliyopiga mashuti mengi kuanzia hatua ya makundi ikiwa ina wastani wa mashuti matano, nafasi ya pili inashika Mamelodi ikiwa na mashuti manne.

Lakini Mamelodi ikiongoza vipengele vingine viwili muhimu baada ya mechi ya juzi, kipengele cha pasi nyingi ina wastani wa pasi 493 ikifuatiwa na Ahly 398, huku kwenye kipengele cha wastani wa umiliki ikiwa nao 65.8 katika nafasi ya kwanza.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: