Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fredy ‘Fungafunga’ na Jobe ni mali au sio mali

Fredy X Jobe Mali Sio Mali Fredy ‘Fungafunga’ na Jobe ni mali au sio mali

Tue, 27 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nilipomhoji rafiki yangu Ahmed Ally, msemaji wa Simba kupitia kituo cha Wasafi kuhusu uwezo wa washambuliaji wapya wawili wa Simba, Fredy Michael na Pa Jobe alinijibu kwa mbwembwe. Nilitegemea. Ni aina mpya ya kazi zetu za wasemaji. Zamani walikuwa wanaitwa makatibu wenezi.

Aliniambia Fredy alikuwa tishio mazoezini. Yeye alimpachika jina la Fredy ‘Fungafunga’. Jobe akampachika jina la ‘Jobe mabao’. Hiki ndicho ambacho mashabiki wa Simba walikuwa wanaombea. Na hiki pia ndicho ambacho binafsi nilikuwa naombea. Inachosha kurudia kwamba Simba imekosea katika madirisha kama matano ya uhamisho mpaka sasa. Yawe makubwa au madogo.

Tukarudi uwanjani kusubiri kuona kile ambacho Ahmed alikuwa ametuahidi. Sio tu Ahmed, hata mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alikuwa ametuahidi. Alikuwa ametuahidi kwamba safari hii Simba walikuwa wanakwenda kuchukua washambuliaji mahiri na wa bei mbaya. Na kwamba hawataki kubahatisha katika soko la uhamisho la dirisha dogo.

New Content Item (1)

Nadhani rafiki yangu ‘Try Again’ na yeye amechoshwa vile namna inavyoonekana kwamba watani wao wamekuwa wanafanya vyema katika soko la uhamisho la wachezaji kwa sasa. Msimu huu tu fikiria namna Yao Kouassi, Nickson Kibabage, Maxi Nzingeli, Pacoume Zouazou wanavyofanya vyema uwanjani.

Tukarudi uwanjani kuwasubiri Fredy na Jobe. Mpaka sasa Jobe ana mabao mawili. Moja la Ligi Kuu Bara na jingine la michuano ya Kombe la Shirikisho (FA). Fredy alifunga bao moja dhidi ya Tabora United pale Tabora. Mpira wake ulikuwa dhaifu ukamgusa beki mmoja wa Tabora ukampoteza maboya kipa, ukaenda katika nyavu. Lilikuwa bao la faraja kwa mashabiki.

Hata hivyo, wote wawili hawajawaridhisha sana mashabiki hasa Fredy. Ijumaa usiku pale Abidjan aliondoka akiwa mchezaji anayechukiwa zaidi na mashabiki uwanjani na wale waliokuwa wanatazama mechi katika televisheni. Alionyesha kiwango kibovu mbele ya familia yake ambayo ilihudhuria pambano hilo.

Huku nyumbani kuna mashabiki ambao wanadai ni bora angepangwa John Bocco kuliko Fredy. Ghafla tu ndani ya mechi ya tano nchini tayari mashabiki wa Simba wamemkumbuka Bocco. Kwamba ni bora kuliko straika aliyejengeka kimisuli, Fredy Michael ‘Fungafunga’? Inasikitisha kidogo.

Simba wamekosea tena kusajili? Sina uhakika. Ni mapema. Muda utasema. Kwanza kabisa kwa wasifu wa wachezaji hawa hasa Fredy, ilionekana Simba wamelamba dume. Hata mimi ningemsajili Fredy. Kwamba alikuwa amefunga mabao 14 katika Ligi Kuu Zambia hata mimi ningemsajili. Wakati mwingine wasifu wa mchezaji unatosha ingawa unafikirisha.

Fredy anaonekana kuwa na mwanzo wa kusuasua, lakini inafikirisha kidogo. Kwamba Simba hawakufanya ‘homework’ yao kwa Fredy na Job hasa baada ya kukosea katika usajili wa kina Ismail Sawadogo? Na baada ya kujiridhisha kiasi kwamba naamini ningeweza pia kumsajili Fredy, basi tuamini kwamba Ligi Kuu Zambia ni nyepesi kuliko ya Tanzania?

Pale Rwanda naweza kuamini. Baada ya kuambiwa namna Michael Sarpong na Andre Onana walivyotamba Rwanda na kisha kuangalia namna viwango walivyoonyesha Tanzania unaweza kuamini kwamba Wanyarwanda wapo chini yetu kidogo kwa sasa. Huku wawili hawa hawajatisha sana kulinganisha na viwango tulivyowasikia Rwanda.

Zambia? Wametuzidi kisoka. Inawezekana hawajaweka pesa nyingi katika klabu, lakini wametuzidi kisoka. Haina siri. Kwamba mchezaji anaweza kuwa tishio Zambia halafu Tanzania akawa mchezaji wa kawaida, sidhani kama tumefikia hatua hiyo. Tuliona kwa kina Davis Mwape, Clatous Chama, Larry Bwalya na wengineo. Mpira wa Taifa hauwezi kuwashinda kwa urahisi.

Lakini sasa mkononi tuna Fredy aliyetokea huko. Hapa ndipo tunapolazimika kufunga breki za katuni. Fredy ni mali au sio mali? Tunalazimika kusubiri kidogo. Tumewahi kuwaona wachezaji walioingia kimyakimya katika ligi yetu halafu baadaye wakatuziba midomo. Wapo. Mifano ipo mingi.

Wachezaji hawa hawapatikani Tanzania tu. Wanapatikana katika ligi nyingi. Mchezaji anaingia kawaida halafu anaondoka shujaa. Inategemeana na mambo mengi ambayo mchezaji ameshindwa kukabiliana nayo wakati huo. Akizoea anajikuta akirudi kuwa tishio kama alikotoka. Kila mahala wachezaji wageni wanakabiliana na hali hiyo.

Kuna ambaye anachemka katika siku zake za kwanza kutokana na aina ya uchezaji wa ligi yenyewe. Kuna ambaye anashindwa kung’ara kutokana na uchezaji wa timu yake. Vyote hivi vinahitaji kitu kinachoitwa kuzoea. Wazungu wanaita ‘adaption’.

Kuna wale ambao wanashindwa kuonyesha makali kwa sababu ya upweke. Kitu hiki kinaitwa ‘loneliness’. Ilimkuta rafiki yetu, hayati Jose Antonio Reyes alipohamia Arsenal akitokea Hispania. Hakuelewa kitu. Alikuwa peke yake na mkiwa. Alishinda ndani akilia. Hakuwa na marafiki na muda wote London mvua ilikuwa inanyesha tofauti na kwao Hispania ambako kuna hali ya hewa nzuri.

Alijaribu kuonyesha makeke yake Arsenal, lakini baadaye mpira ulimshinda na Arsene Wenger akaamua kumpeleka kwao Hispania akacheze kwa mkopo Real Madrid. Kuna mambo mengi ambayo yanamfanya mchezaji kushindwa kuonyesha makeke pindi akihamia timu mpya.

Lakini subiri kwanza. Sio zote hizi zinaweza kuwa sababu. Wakati mwingine mnaweza kujikuta mmesajili mchezaji ambaye hana tu uwezo mkubwa. Unaweza kumpa muda na kila kitu, lakini ukagundua kwamba umepigwa. Iliwahi kutokea kwa Yikpe na Yanga.

Kitu cha msingi ni kwamba muda unabaki kuwa hakimu mzuri tu. Ni muda ndio ambao unaweza kuamua kama Fredy ni mali au sio mali. Ni muda ndio ambao unaweza kuamua kama Jobe ni mali au sio mali. Ni muda ndio ambao uliamua Peter Banda na Ousmane Sakho ni mali au sio mali. Binafsi naamini hawakuwa mali.

Natamani Fredy na Jobe wawe mali kwa sababu wasipokuwa mali maisha yatakuwa magumu kwa rafiki yangu Try Again. Najua siasa nyingi za mpira ambazo zinaendelea Msimbazi. Kuna watu wanatamani afeli. Wakati mwingine maadui zako wa mpira huwa hawachagui sana silaha. Wanaweza kukusakama kwa msimamo wa ligi au usajili unaoufanya.

Lakini zaidi ni mlinganisho wa usajili wako na usajili wa watani. Kule kwa watani huwa wanafeli katika usajili katika miaka ya karibuni lakini bahati yao huwa wanapatia sana pia. Angalia usajili wa hao kina Pacome na wenzake ulivyoleta madhara chanya katika msimu huu. Tayari wapo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo imewashinda kwa miaka nenda rudi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: