Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

'Fitness' imeanza kurejea wachezaji wa Simba

Simba SC Marakech.jpeg 'Fitness' imeanza kurejea wachezaji wa Simba

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha wachezaji 23 wa Klabu ya Simba, tayari kimeondoka kwenda Casablanca nchini Morocco kwa ajili ya mechi ya raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kundi B dhidi ya Wydad Casablanca utakaochezwa Jumamosi ijayo, huku Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha akiweka wazi kuwa amekuta wachezaji hawana utimamu wa mwili.

Kikosi hicho kilitarajiwa kuchukua usafiri mwingine wa aina hiyo kitakapotua jijini Casablanca  kuelekea Marrakech na kuanza moja kwa moja mazoezi leo kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, kabla ya safari hiyo amebainisha kuwa kazi kubwa alinayo, pamoja na kuitengeneza kuifundi kwa ajili ya kukabiliana na Wydad Casablanca, lakini pia ni kupandisha kiwango cha utimamu wa mwili ambacho kilikuwa chini mno, katika namna ambayo imemshangaza hata yeye mwenyewe.

"Wachezaji hawakuwa na utimamu wa mwili, yaani ilikuwa chini ya kiwango na ndiyo eneo ambalo nimewekeza nguvu kweli kweli, kiufundi Simba ina wachezaji wazuri sana, levo ya utimamu wa mwili ndiyo inawasumbua, na nimemwachia kazi mwalimu mwenzangu Kamal Boujdjenane anaifanya kazi hiyo," alisema kocha huyo raia wa Algeria aliyechukua nafasi ya Roberto Oliveira.

Alisema anadhani ndiyo sababu inaonekana kama baadhi ya wachezaji wameshuka viwango, au wana umri mkubwa unaowafanya washindwe kukabiliana na mikikimikiki.

"Nadhani ndiyo ilionekana kama wachezaji wanaonekana kama viwango vyao vimefikia ukingoni, lakini kwa sasa inaanza kuongezeka na itaongezeka zaidi, kwa sasa tunahitaji angalau asilimia 50 tu ya ufiti wa wachezaji iweze kuwa kwenye ushindani unaotakiwa," alisisitiza kocha huyo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo alisema timu iliondoka na wachezaji 23 tu na iliyowaacha ni kwa sababu za kiufundi na si majeruhi.

"Mungu akitujalia kufika siku ya Jumatano kama tunavyotegemea, moja kwa moja tutafanya mazoezi, Alhamisi tutaendelea na Ijumaa pia, kabla ya kucheza mechi yetu Jumamosi kwa ajili ya kupigania pointi tatu dhidi ya timu hiyo.

Wachezaji ni 23, na watakaobaki ni wale ambao hawatokuwa kwenye mipango ya kocha, watabaki kwa sababu za kiufundi na si za kimajeraha," alisema.

Ahmed pia amewasifu makocha hao kwa kuonekana kurudisha kiwango cha utimamu wa mwili wachezaji wa timu hiyo.

"Kwanza nimeona utimamu wa mwili umeongezeka sana ni moja kati ya vitu ambavyo vimetusumbua kwa muda mrefu, nadhani tumpe pongezi zake huku mwalimu mpya Benchikha wa viungo Kamal, kwa siku hizi zilizobaki, wamesema ndiyo eneo linalofanyiwa sana kazi, nadhani huko mbele timu itakuwa tishio," alisema.

Simba mpaka sasa ina pointi mbili kwenye Kundi B, ikiwa kwenye nafasi ya tatu ya msimamo wa Kundi B linaloongozwa na Asec Mimosas ya Ivory Coast yenye pointi nne sawa na Jwaneng Galaxy ya Botswana huku Wydad ikiburuza mkia bila pointi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: