Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Darasa kutoka African Football League

Simba Vs Ahly Cairo Misri.jpeg Darasa kutoka African Football League

Fri, 27 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashindano ya CAF ya African Football League (AFL) yalifunguliwa Tanzania. Lilikuwa tukio kubwa la kimichezo kuwahi kutokea. Ilishuhudiwa historia ya mpira wa miguu ya Afrika ikiandikwa, hasa kwa mashindano ya klabu.

Uwanja wa Benjamin Mkapa ulipokea ugeni mzito huku orodha ikiongozwa na Rais wa Fifa, Gianni Infantino na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Hussein Mwinyi na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro.

Alikuwepo pia Rais wa CAF, Patrice Motsepe, marais wa vyama vya mpira vya mataifa mbalimbali barani Afrika na wageni wengine mashuhuri kutoka Afrika na duniani kwa ujumla.

Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger na mwamuzi wa zamani, Pierluigi Collina ambao kwa sasa ni watumishi wa FIFA walikuwa ni kivutio kwa mashabiki. Tukio hili lilikamilishwa kwa mchezo wa robo fainali kati ya Simba na wageni Al Ahly kutoka Misri.

Mandhari ya uwanja na hadhi ya mchezo wa ufunguzi ilitosha kuonyesha sasa yanakuja mashindano makubwa barani Afrika.

Tayari michezo ya robo fainali imechezwa. Wawakilishi wa Tanzania na Ukanda wa Cecafa Simba wametolewa kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla ya mabao 3-3 dhidi ya Al Ahly.

Pamoja na kutolewa, bado Tanzania inayo mengi ya kujivunia na ya kujifunza kutoka katika matukio na michuano hiyo. Kuna mambo ambayo yanaweza kubadilika na kuna maendeleo yanaweza kupatikana ikiwa wadau wa mpira na taifa kwa ujumla wataamua kuchukua mafunzo tuliyoachiwa na kinachoendelea katika michuano ya African Football League.

Tukio la uzinduzi wa AFL limetoa funzo kwa Bodi ya Ligi na TFF kuhusu namna ya kuandaa matukio kwa weledi. Nakumbuka huko nyuma Fifa walikuwa wanatoa mafunzo kwa mashirikisho kuhusu uandaaji wa matukio (Event Management). Lengo lilikuwa ni kuhakikisha matukio yanayohusu mpira wa miguu yanaenda kama yalivyopangwa hasa katika ubora wake na utunzaji wa muda.

Suala la kulinda chapa za wawekezaji pia ni la kuzingatiwa katika matukio. Hapa somo linaenda pia kwa waandaji wa shughuli za kiserikali hasa zile za muhimu kama sherehe za Sikukuu ya Uhuru. Kutunza muda, kupangilia matukio na kupamba mandhari ni vitu ambavyo vikizingatiwa vitanogesha sherehe.

Afrika ya Mashariki imefanikiwa kupata uteuzi wa kuandaa michuano ya mataifa ya Afrika (Afcon) ya mwaka 2027. Maandalizi na tukio la AFL linaweza kuwa ya msaada mkubwa katika kuchota uzoefu na pia hali ya kujiamini kuwa inawezekana.

Maandalizi ya Uwanja wa Benjamin Mkapa na vingine vinavyotumika kwa michuano hiyo vinaweza kutumika kama chachu na kipimo cha namna ya uboreshaji wa miundombinu ya kuchezea mpira.

Uwanja bora ni muhimu kwa timu kucheza soka bora. Serikali imeahidi kujenga viwanja vipya na kuboresha vile vilivyopo na kama hilo litaatokea basi utakuwa mwanzo wa kukua kwa ubora wa mpira wetu.

Utaratibu wa kuuza tiketi na kuingia uwanjani ulikuwa wa kueleweka, mzuri na wa amani. Walinzi wa uwanjani waliwasaidia watazamaji na wala si kuwapiga virungu. Vyombo vinavyoangalia usalama wakati wa mchezo vina somo la kujifunza kuhusu majukumu yao.

Uwanjani kulikuwa na mengi ya kujifunza pia. Mchezo kati ya Simba ulikuwa bora kabisa ukizingatia kwamba ulikuwa unamhusisha bingwa wa Afrika mara nyingi kuliko klabu zote yaani Al Ahly.

Simba iliipa Al Ahly mchezo mgumu hapa nyumbani na ugenini na kuisha kwa sare ya jumla ya mabao 3-3. Michezo hiyo ilituonyesha mpira wa Tanzania na Ligi Kuu imepiga hatua. Kumbuka mwaka jana Yanga ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa kombe kwa kanuni dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Mchezo wa Simba dhidi ya Al Ahly na Yanga dhidi ya timu za Tunisia na Algeria na Taifa Stars dhidi ya Algeria inatoa picha ya kupungua kwa pengo kati ya mpira wetu na ule wa mataifa ya Kaskazini ambayo yametawala mpira wa Afrika.Hata hivyo, bado tuna kazi ya ziada kuweza kuwafikia hawa wenzetu hasa upande wa uwekezaji katika mpira wa vijana.

Klabu zetu kwa hatua zilipofikia zinaweza kutoa changamoto kwa klabu za Kaskazini kama zitagundua kinachopungua. Naamini Simba ikiongeza mbinu na kufanya uwekezaji wenye weledi inaweza kuhama kutoka kwenye kujivunia rekodi kwenye karatasi na kuanza kuweka mataji kwenye kabati lake.

Baada ya mchezo wa ufunguzi wa AFL kulikuwa na mchezo mwingine kati ya TP Mazembe na Esperance de Tunis ya Tunisia. TP Mazembe imechezea michezo yake ya nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kutokana na CAF kutoridhishwa na hali ya miundombinu ya mpira na masuala mengine ya kuandaa michuano ya hadhi ya AFL kule DR Congo.

Katika mchezo huo Mazembe ilishinda 1-0 kulikuwa na funzo kubwa nalo ni mapenzi ya Watanzania kwa mpira wa miguu bila kujali timu gani zilikuwa zinacheza. Ni sehemu gani ungetegemea timu zote za kigeni lakini bado uwanja unajaza mashabiki.Sioni sehemu nyingine.Ni nchi ya mpira.

Matukio ya AFL yametuonyesha hazina iliyojificha katika mpira wetu na soko la ukarimu.Mafunzo haya tukiyahamisha kwa vitendo kwenda kwenye namna tunavyoendesha matukio yetu ya mpira basi kesho na kesho kutwa hatutahitaji kutoa jasho jingi kuomba kuwa wenyeji wa mashindano mbalimbali ya mpira na hata matukio mengine ya kimataifa.

Uwepo wa Simba na Yanga, makabila mbalimbali, lugha mbalimbali, dini mbalimbali, uoto na maliasili, zote hizo ni tofauti zetu zinazotuunganisha huku zikichagiza uwepo wa amani yetu.Hakukuwa na mahali bora na salama kuzindua AFL zaidi ya Dar Es Salaam.Tujifunze na tuutumie urithi wa African Football League.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: