Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dalali apewe maua yake Simba

Dalali Pic Data Hassan Dalali

Fri, 4 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba inafanya tamasha la 14 mwaka huu, tangu lianzishwe 2009 na aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali, limekuwa na mafanikio makubwa na linatumika kutambulisha mastaa wao kwa msimu mpya.

Kabla ya kilele cha Simba day kufanyika wikiendi ijayo awamu hii wakitumia kauli mbiu ya ‘Simba Unyama Mwingi’, Mwanaspoti limefanya mazungumzo na muasisi wa tamasha hilo na mastaa wa zamani wa klabu hiyo.

Dalali anasema anajisikia faraja kuona kitu alichokianzisha kinafanywa na nchi nzima na kimevuka malengo ambayo awali ilikuwa ni kujenga uwanja wa Bunju ambao kwa sasa umepewa jina la Mo Simba Arena, huku akiweka wazi kitu anachotamani ni kuona unakamilika angali yupo hai.

“Tukafanikiwa kununua uwanja nilisaidiana na aliyekuwa katibu wangu, Mwina Kaduguda na viongozi wengine, tulijitoa kwa hali na mali, mechi ya kwanza kwenye tamasha hilo ilikuwa dhidi ya Villa ya Uganda, sasa naona timu nyingine zinaiga na si kitu kibaya ni kizuri kwasababu kinawaweka watu pamoja,”anasema.

Anafurahishwa anavyoona viongozi wanafanya ubunifu zaidi kwenye tamasha hilo, akitarajia kuona makubwa Agosti 6, akisisitiza hawezi kukosa kwasababu starehe yake kubwa ni kuishabikia Simba na kuona inafanya makubwa ndani na nje.

“Mashabiki wa Simba wajitokeze kwa wingi kufurahia kukutanika kwa pamoja na kuwapa moyo wachezaji wetu, kwani watajisikia raha sana wakitambulishwa mbele ya umati na itawapa nguvu ya kujituma kwa bidii wakijua wapenzi wa Simba wanahitaji furaha,” anasema Dalali na kuongeza”

“Sina shaka na viongozi najua watakuja na mambo makubwa zaidi, hivyo tunatakiwa kuungana kwa pamoja kuhakikisha kinafanyika kitu cha kuacha historia yenye mafunzo kwa wengine na ikumbukwe sisi ndio waanzilishi wa tamasha hilo nchini.”

Anasema kwa mara ya kwanza tamasha hilo walipata Shilingi 70 milioni, ambapo Milioni 20 aliipeleka kwenda kununulia uwanja wa Bunju, jambo ambalo anaona uongozi wake uliacha alama kubwa itakayokumbukwa milele.

“Kwa sasa tamasha hilo linaipa Simba pesa nyingi, ndio maana nasema ni jambo la kujivunia, kikubwa nilitamani Simba iwe mfano wa klabu ya kuigwa Afrika kwa kumiliki vitu mbalimbali ikiwemo uwanja,”anasema.

Staa wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel anasema kila anapolitazama tamasha hilo, anaona kuna haja ya kumfanyia kitu kikubwa Dalali ambaye ndiye muasisi.”Kiukweli Dalali alistahili heshima ya kipekee,kuanzia siku ya tamasha na ikiwezekana kumpa alama ambayo akiitazama itakuwa inampa faraja ya kazi yake.

“Lazima tumpe sifa zake akiwa hai, Dalali alifanya matawi yawe na nguvu, alianzisha Simba Day kwa ajili ya kununua uwanja, hivyo viongozi waliopo lazima wajue mchango wa huyo mzee kama tunavyojua sisi wapenzi wa Simba na mashabiki kwa ujumla,” anasema.

Mchezaji mwingine wa zamani wa timu hiyo, Mussa Hassan Mgosi anasema Dalali alibuni kitu kikubwa kinachowakutanisha Wanasimba pamoja na kufanya wafurahie kuona mastaa wao, anafurahishwa kuona kila mwaka viongozi wanakuwa na ubunifu mkubwa.

“Nafurahia kuona nilikuwa kwenye kikosi cha kwanza kilichocheza Simba day 2009 dhidi ya Villa ya Uganda, hivyo nimeingia kwenye historia ya tamasha hilo, kwa sasa limekuwa kubwa na limeigwa na timu nyingine,”anasema.

Kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibaden anasema kuna haja wazee ambao waliitumikia Simba kwa moyo mmoja na kuvuja jasho lao wapewe heshima yao angali wapo hai, “Simba tumeifanyia mengi lazima kuwepo na haja ya kuwatambua wazee wote ambao walitumika kwenye klabu.

“Mfano kuna ambao walijenga jengo la Kariakoo, muasisi wa tamasha hilo, wachezaji walioacha historia zao,” anasema.a

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: