Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Coulibaly awatisha mabeki Ligi Kuu

Freddy Michael Kouablan (17).jpeg Freddy Michael Kouablan

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba inaendelea kujifua kambini Simba Mo Arena, Bunju Dar es Salaam ikijiandaa na mechi za ASFC, Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mastaa wapya wakianza kuwasha moto mbele ya Kocha mkuu, Abdelhak Benchikha, ila mashabiki wakisubiri kwa hamu kujua hatma ya mataji yaliyosalia kwa msimu huu.

Simba inamiliki Ngao ya Jamii iliyoivua Yanga kwenye mechi ya fainali iliyopigwa Mkwakwani, Tanga huku ikiyapigia hesabu makombe ya Ligi Kuu na ASFC na tayari imeshaongeza mashine mpya sita, wakiwamo watatu wa kigeni na wengine kama hao wazawa.

Wachezaji wa kigeni ambao tayari wameanza kuwasha moto mazoezini Bunju ni Freddy Michael Kouablan kutoka Ivory Coast aliyewahi mapema kambini, Pa Omary Jobe kutoa Gambia na Babacar Sarr wa Senegal, hata hivyo kuna beki mmoja wa zamani wa Simba amefichua, Simba ilivyolamba dume kwa kumsajili Freddy.

Beki huyo Zana Coulibaly ametuma salamu akisema mshambuliaji Freddy Kouablan sio mtu mzuri kwa wapinzani na kutoa tahadhari mapema kwa mabeki na makipa kujiandaa na kazi mbele ya nyota huyo aliyesajiliwa kutoka Zambia.

Coulibaly ametoa kauli hiyo akikoleza mzuka wa mashabiki wa Simba ambao kwa kupitia picha za mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast akiwa mazoezini wakiona msuli na mwili ulivyokaa kimazoezi kisha kimo chake kizuri wakajikuta wanakaa mkao wa subira kujua kama yaliyomo yamo.

Coulibaly ambaye ni raia wa Ivory Coast amewaambia mashabiki wa klabu yake hiyo ya zamani kwamba kama walikuwa wanamsubiri mshambuliaji anayejua kufunga basi Freddy ni mtu wa kazi hiyo.

Beki huyo wa kulia alisema, Simba itachekelea ubora wa mshambuliaji huyo atakapoanza kazi lakini akaongeza kuwa kwa timu pinzani ujio wa Freddy sio taarifa njema, akiwataka mabeki wanaokaba bila hesabu kuijiandaa na makali yake.

“Namjua Freddy (Kouablan) najua amekuja huko Tanzania, waambie mashabiki wa timu yangu (Simba) wamepata mshambuliaji wa kazi ya kufunga, watafurahia kazi yake,” alisema Coulibaly ambaye sasa anaichezea Africa Sports ya Ivory Coast.

“Ana uzoefu mkubwa amecheza Angola, Msumbiji na sasa ametokea Zambia, hapo Tanzania napajua mabeki wanakaba kwa vurugu sana sasa huyu watapambana naye na wasipokuwa makini atawafunga sana kwa kuwa ana akili pia akijua kuwakimbia mabeki na kukaa maeneo ya kufunga,” alisema Coulibaly aliyeichezea Simba kwa msimu mmoja wa 2019-2020 kabla ya kuibukia AS Vita ya DR Congo aliyeongeza;

“Nimempongeza sana (Freddy) kwa kujiunga na Simba nimemwambia amejiunga na timu kubwa Tanzania ina mashabiki wanaoipenda timu yao na watampenda kama ataanza kwa kasi. Nimefurahi kusikia Chama (Clatous) bado yuko Simba na kaka yangu Kapombe (Shomari) hawa ni wachezaji ambao wanajua kuwapa pasi za mabao washambuliaji.”

Freddy amejiunga na Simba katika dirisha dogo akitokea Green Eagles ya Zambia aliyoichezea mechi 18 na kufunga mabao 14 na kuasisti manne katika msimu huu ili kuchukua nafasi ya Jean Baleke aliyerudishwa TP Mazembe kabla ya kula shavu kupelekwa Al Ittihad ya Libya. Baleke aliachwa pamoja na Moses Phiri ambaye nafasi yake inatarajiwa kuzibwa na Pa Jobe kutoka Gambia ambaye naye alisajiliwa pia dirisha dogo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: