Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cadena kiroho safi Simba

Cadena Simba Nm Cadena kiroho safi Simba

Sat, 18 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba ipo kwenye maandalizi ya mechi ya awali ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakapoialika Asec Mimosas ya Ivory Coast, huku kaimu kocha mkuu, Daniel Cadena akisema anapokiangalia kikosi hicho na morali iliyopo anaamini mambo yatakuwa mazuri tofauti na timu iliyocheza mechi za Ligi Kuu.

Wekundu wa Msimbazi ambao msimu uliopita waliishia robo fainali ya michuano hiyo, watakuwa wenyeji wa Asec katika mchezo utakaopigwa Novemba 25 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni wiki kadhaa tangu walipowatibua mashabiki kwa kufungwa mabao 5-1 na Yanga katika dabi ya Ligi Kuu.

Cadena anayeendelea kukinoaa kikosi hicho na msaidizi wake Seleman Matola, aliliambia Mwanaspoti baada ya kipigo cha Yanga na sare ya 1-1 dhidi ya Namungo, morali ya wachezaji ilishuka na alipokabidhiwa timu jambo la kwanza alipambana kurudisha ari ya upambanaji na sasa wapo tayari kuionyesha Afrika ubabe.

“Morali ilikuwa chini kutokana na matokeo yalivyokuwa, ilibidi tuanze kwa kuhakikisha wanarejea kwenye ari nzuri na sasa tuko vizuri. Simba ina timu nzuri, na wachezaji wetu wamejifunza kutokana na makosa na kwa sasa wapo tayari kuendelea kuipambania timu kuhakikisha inafikia malengo,” alisema Cadena na kuongeza;

“Tuna mechi ya kimataifa hivyo maandalizi yetu ni kuhusu mchezo huo, kila mchezaji yupo vizuri na baadhi yao wapo timu zao za taifa. Naamini hadi kufika muda wa mechi, tutakuwa tumekamilika na tayari kwa kutoa burudani.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Iman Kajula alisema, timu hiyo bado haijapoteza muelekeo, mashabiki wake wanapaswa kutulia na kuendelea kuipa sapoti timu yao kwani watarejea kwa kasi ya ajabu.

“Upepo huu hauwezi kutuyumbisha, hakuna asiyejua ubora wa Simba hususani linapokuja suala la mechi za kimataifa, tupo imara na tunaenda kufanya vizuri katika mechi zijazo kama ilivyokuwa kawaida yetu,” alisema Kajula.

Mfungaji bora wa ligi msimu uliopita, Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ alisema kila mchezaji anatambua umuhimu wa mechi ijayo dhidi na Asec na wapo tayari kurejesha burudani Msimbazi.

“Simba ni timu kubwa na bora Afrika, tutathibitisha hilo kwenye mechi zijazo za kimataifa kwani tumekuwa na rekodi nzuri huko lakini pia kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa mechi hizo,” alisema Saido.

Licha ya kufanya siri, lakini Mwanaspoti linajua Simba itacheza mechi moja ya kirafiki wikiendi hii ili kutathimini maendeleo ya kikosi chake kabla ya kuivaa Asec.

Mastaa Clatous Chama, Aishi Manula, Saido, Kibu Denis na Mzamiru Yassin walio katika timu zao za taifa wanatarajia kujiunga na kikosi cha Simba, Novemba 22, mwaka huu, siku tatu kabla ya mechi hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: