Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha wa Onana ana kazi ngumu Msimbazi

Onana Simba Vs Jwaneng Galaxy.jpeg Benchikha wa Onana ana kazi ngumu Msimbazi

Mon, 4 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Abdelhak Benchikha, kocha mpya wa Simba ana kazi sio kidogo. Sijajua sana kuhusu alikotoka lakini hii inaweza kuwa moja kati ya kazi yake ngumu aliyowahi kuifanya tangu awe kocha. Namuonea huruma kiasi. Pengine hakujua ambacho angeweza kukutana nacho.

Simba walikuwa Gaborone Jumamosi jioni kukabiliana na Jwaneng Galaxy, wakati watani zao Yanga walikuwa Temeke kucheza na Al Ahly. Labda tukitazame kibarua ambacho kinamkabili Benchikha ndani na nje ya uwanja.

Amerithi kikosi ambacho hakina makali katika maeneo mengi ya uwanja. Simba hawana kasi, hawana uamuzi wa haraka, sio wazuri wakiwa hawana mpira. Bahati nzuri wakakabiliana na timu ambayo ndani ya dakika kumi wote tulijiuliza walipataje ushindi wa bao moja dhidi ya Waydad Casablanca halafu ugenini.

Wenyeji wao walikuwa wakipoteza mipira ovyo. Hawakuwa na umiliki wa mpira. Hawakuwa na ufundi katika kujilinda. Hawakuwa na jipya. Mechi waliyoshinda dhidi ya Wydad ugenini iliwafanya wenyeji wao waamini kwamba Jwaneng walikuwa wametumia ushirikina kushinda mechi. Ni mechi ambayo wenyeji walifika langoni na kupiga mashuti zaidi ya 21 yaliyolenga lango.

Tofauti ya Simba na Wydad ni kwamba Simba waliharibu muvu zao wenyewe kwa sababu ya kukosa umakini na kutoonana kwa haraka. Sijui kama ni jambo ambalo litatibika kwa haraka chini ya Benchikha. Simba walionekana kutawala mechi kutokana na ubovu wa wapinzani wao lakini wakashindwa kutengeneza nafasi na kuzitumia.

Nani alimleta Willy Essomba Onana? Pepo ataisikia tu. Tulishangazwa kuona Kocha Benchikha ameamua kumuweka benchi Clatous Chama na kumpanga Onana. Alikuwa ameona nini kutoka kwa raia huyu wa Cameroon? Alikuwa ameona kitu gani mazoezini katika siku chache ambazo amejiunga na Simba kama kocha mkuu?

Chochote ambacho alikuwa amekiona sisi hatujakiona tangu Onana atue nchini. Baada ya kufunga bao zuri katika pambano lake la kwanza dhidi ya Power Dynamos, Onana amekuwa akila mshahara wa bure kama tulivyoona pale Gaborone. Mzito, anapenda kukaa na mpira huku uwezo wa kukaa nao ukiwa ni mdogo.

Hatujaona ubora wake katika maeneo mengi. Anacheza kibishoo zaidi na sio mpambanaji. Sijui ilikuwaje akawa Mfungaji Bora Rwanda. Ligi ya Rwanda imeanza kunipa shaka kila ninapotazama uchezaji wake na kisha kujikumbusha kwamba alikuwa staa katika ligi hiyo. Sidhani kama ana maisha marefu Msimbazi. Timu zetu hazioni hasara kupata hasara.

Halafu kuna Jose Luis Miquissone. Sijui kimemtokea nini. Zamani katika mechi kama hii, Miquissone alitazamiwa kuwa mtu wa kuiteketeza Galaxy. Leo anaingia uwanjani dakika ya 70 na bado hakuna anachofanya. Alipokuja mwanzoni ilitajwa kwamba alikuwa ameongezeka kilo katika mwili wake.

Miquissone wa sasa amerudi kuwa na umbo lile lile, lakini anashindwa hata kutuliza mpira uwanjani achilia mbali kukokota. Imekuwa, ghafla sana na sasa tunajiuliza kama kweli ataweza kurudisha makali yake yaliyowahi kuifanya Al Ahly kutoa kiasi kikubwa cha pesa kupata huduma zake miaka michache iliyopita.

Simba walilia arudi lakini hadi sasa hawaamini wanachokiona. Kama uongozi utaamua kuachana naye mwishoni mwa msimu sidhani kama kuna Mwanasimba ambaye atapigwa na butwaa. Amekuwa miongoni mwa wageni mizigo katika klabu hii ambayo ilimtambulisha zaidi barani Afrika.

Naanza kupatwa na wasiwasi na Jean Baleke. Ni kweli anaibeba Simba kwa kutupia mabao, lakini nje ya mabao hana mchango mkubwa uwanjani. Inabidi abadilike kama kweli anataka kuibeba Simba. Asisubiri mabao ya kugusa tu mpira uende wavuni.

Faraja nzuri katika mechi hii ni namna ambavyo walinzi wa Simba wakiongozwa na Henock Inonga walivyoweza kuzima mashambulizi ya Jwaneng ambao walikuwa wanatumia zaidi kasi ya miguu yao kupitia mipira mirefu iliyokuwa inatoka nyuma. Inonga, Che Malone, Mohammed Hussein na Shomari Kapombe walifanya kazi nzuri katika ulinzi.

Kipa Ayoub Lekred anaonekana kuwa imara langoni tangu alipotikisika kule Lusaka katika pambano la Power Dynamos. Walau unaweza kumuamini kwa kiasi kikubwa kuliko Ally Salim. Anajua kujipanga na anajua kusambaza mipira kuanzia nyuma. Wote waliokuwa na wasiwasi wameanza kumuamini wakati huu Aishi Manula akiwa bado hajawa timamu kimwili.

Na sasa Benchikha anakabiliwa na kazi tatu. Ya kwanza ni kuifanya Simba icheze kitimu zaidi. Kipindi cha kwanza cha pambano hili tuliona dalili. Pia ana kazi ya kuinua viwango vya wachezaji mmoja mmoja. Wachezaji wa Simba viwango vyao vipo chini. Kama hataweza kufanya hivi anaweza kuuamuru uongozi wa Simba kuachana na kundi kubwa la wachezaji, hasa wale wa kigeni.

Yote haya inabidi ayafanye huku akijaribu kuepuka aibu ya kuwa kocha wa kwanza katika miaka ya karibuni atakayeshindwa kuipeleka Simba robo fainali. Sawa, anguko la Simba halijaanzia kwake, lakini Benchikha anaweza kujikuta akiwa muathirika. Nafasi ya Simba kwenda robo fainali imeanza kuwa ngumu zaidi.

Simba wameambulia pointi mbili katika mechi zao mbili za mwanzo. Na sasa wana safari ya kukabiliana na Wydad pale Morocco. Mechi mbili zijazo watacheza na hawa jamaa wa Afrika Kaskazini wakianzia na pambano la ugenini ambalo litakuwa la machozi jasho na damu kwa wenyeji.

Tayari Wydad wamepoteza mechi mbili. Moja nyumbani dhidi ya Jwaneng nyingine wamepoteza juzi Jumamosi dhidi ya ASEC Mimosas. Pambano hili dhidi ya Simba watalitumia kwa kujaribu kuwafuta machozi mashabiki wao. Hawatataka kufungwa mechi ya pili mfululizo nyumbani, au mechi ya tatu mfululizo katika kundi. Simba wana kazi.

Kama Simba wataweza kufanya vema katika mechi mbili zijazo dhidi ya Wydad, huku ASEC na Jwaneng wakipunguzana wenyewe kwa wenyewe inaweza kuwasaidia. Tatizo ni kwa Simba ipi? Hii ya Onana? Benchikha ana kazi kubwa ya kufanya. Tusubiri tuone!

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: