Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha kumaliza kazi Dar

Benchikha Morocco.jpeg Benchikha kumaliza kazi Dar

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Simba usiku wa juzi kilikuwa kikimalizana na Mashujaa katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini unaambiwa kocha mkuu wa timu hiyo aliyerejea majuzi kutoka Algeria kwenye mafunzo, amepania pambano la robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri kulimaliza Dar es Salaam.

Kocha huyo amesema anataka kutumia muda uliosalia na wakati ligi imesimama kuisoma upya Al Ahly kabla ya kukutana nayo katika mechi ya mkondo wa kwanza itakayopigwa Ijumaa ya Machi 29 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kwenda kurudiana nao wiki moja baadae jijini Cairo.

Mshindi wa jumla wa mechi hizo atavuka kwenda nusu fainali na kukutana na kati ya TP Mazembe ya DR Congo au Petro Atletico ya Angola, ambazo zitapapatuana katika mechi nyingine ya robo fainali.

Wekundu hao jana usiku walikuwa wakimalizana na Mashujaa katika mechi ya Ligi Kuu Bara kabla ya ligi kusimama kupisha mechi za kimataifa kwa timu za taifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA na kocha Abdelhak Benchikha amesema atautumia muda huo wa mapumziko kuisoma zaidi Al Ahly anaokutana nao baada ya kuwatoa nishai katika mchezo wa CAF Super CAF akiwa na USM Alger ya Algeria kabla ya kusajiliwa na Simba Novemba mwaka jana.

Simba imepania kuvunja unyonge wa kuishia robo fainali ya michuano ya CAF, ikikwama hapo mara nne katika misimu mitano iliyopita, mara tatu kwenye Ligi ya Mabingwa na mara moja katika Kombe la Shirikisho Afrika na wachezaji wa timu hiyo ambao hawajaitwa timu za taifa, watapewa mapumziko ya siku nne kabla ya Machi 20 kuungana kuanza kujifua kujiwinda na mechi hiyo ya CAF.

Hadi kufika jana Saido Ntibanzokiza kutoka Burundi, Clatous Chama wa Zambia na Aishi Manula, Kennedy Juma, Mohammed Hussein na Kibu Denis wa taifa Stars ndio walikuwa wameitwa kwenye timu za taifa.

Kocha Benchikha aliyerejea juzi akitokea Algeria alikoenda kusoma kozi fupi ya siku tano, alisema mechi ya Al Ahly ni kubwa na muhimu hivyo wanajianda kuhakikisha wanaimaliza mapema nyumbani kwa kushinda.

“Tunaenda kujiandaa na mechi kubwa dhidi ya Al Ahly, tutajipanga vizuri ili tushinde nyumbani kabla ya marudiano kwani ni mechi ngumu. Bahati nzuri nawajua nilishakutana nao hivi karibuni, lakini nataka nipate muda wa kuwasoma vizuri,” alisema Benchikha na kuongeza;

“Tutahakikisha tunafanya hivyo na tunawaomba mashabiki wetu kuja kutusapoti na sisi tutapambana na kuhakikisha hatuwaangushi.”

JEURI IKO HAPA

Pamoja na Al Ahly kuwa bingwa mara nyingi zaidi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hilo haliiogopeshi Simba na imeendelea kuwa na jeuri ikiamini inawamudu mafarao hao wa Cairo, Misri.

Rekodi za mechi zilizopita baina ya timu hizo kwa miaka ya hivi karibuni ndizo zinaipa zaidi jeuri Simba kwani imekuwa ikiitikisa Ahly kila wanapokutana.

Kwa miaka ya hivi karibuni timu hizo zimekutana mara sita ambapo kila timu imeshinda mechi mbili na kutoa sare mara mbili, sare ambazo ni za Oktoba mwaka jana kwenye mechi za African Football League (AFL), ambapo mchezo wa kwanza ulipigwa kwa Mkapa na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 na mechi ya marudiano kutwangwa Misri na kuisha moja moja.

KANOUTE, KIBU

Eneo lingine ambalo Simba inapata jeuri kutamba ni kwa wachezaji wake ambao wameitungua Al Ahly na karibu wote bado wapo kikosini.

Simba katika mechi sita za mwisho timu hizo zilipokutana, Simba imefunga jumla ya mabao matano ambapo kiungo Sadio Kanoute ‘Putin’, ndiye ameongoza kuwatungua waarabu hao akiwafunga mara mbili.

Mastaa wengine walioifunga Al Ahly ni Kibu Denis na Luis Miquissone ambaye aliuzwa kwa waarabu hao lakini baadae akarejea Msimbazi. Mwingine aliyeifungia Simba bao dhidi ya Al Ahly ni Meddie Kagere ambaye kwa sasa anakipiga Namungo.

Mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Jamuhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema Simba inahitaji kucheza kwa kujiamini mechi ya nyumbani na hesabu zote izifungie kwa Mkapa. “Waarabu wakiwa kwao wanamambo mengi yanayowabeba na kupata ushindi. Simba inalijua hilo kwani imekutana nao zaidi ya mara mbili,” alisema Julio ambaye kwa sasa ni kocha wa Singida Fountain Gate.

“Simba inatakiwa kucheza mechi ya nyumbani kama fainali, inatakiwa hesabu zake zote izimalizie kwa Mkapa kabla ya kwenda ugenini,” alisema.

Kwa upande wa kocha wa Dodoma Jiji, Francis Baraza alisema kikosi cha Simba kina kila sababu ya kuiondosha Al Ahly.

“Simba inawachezaji wengi bora na wazoefu, Al Ahly sio timu inayoweza kuitisha sana. Kikubwa wajipange kikamilifu pia wasiwe na presha kwani hii ni zamu yao,” alisema Baraza, raia wa Kenya.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: