Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha hesabu kali CAF

Simba Vs Mashujaa.jpeg Benchikha hesabu kali CAF

Mon, 18 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya mapumziko mafupi waliyopewa walipotoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa, mastaa wa Simba ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa, wanarejea kambini leo Jumatatu, huku kocha mkuu wa timu hiyo ya Msimbazi, Abdelhak Benchikha akipiga hesabu kali za kuimaliza Al Ahly katika robo fainali ya CAF.

Simba inatarajiwa kuwapokea mabingwa watetezi hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika mechi ya mkondo wa kwanza wa robo fainali itakayopigwa kuanzia saa 3:00 usiku siku ya Machi 29 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana wiki moja baadaye jijini Cairo, Misri.

Katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa chepesi katika mechi hizo mbili, kocha Benchikha amepiga hesabu kali mbili, ikiwamo kutaka timu ikajichimbie kambi fupi mjini Unguja, Zanzibar kabla ya kuwapokea Al Ahly Kwa Mkapa, akiamini utulivu utawasaidia wachezaji kupokea mbinu atakazowapa.

Inaelezwa kocha huyo amewaeleza mabosi wa klabu anataka kambi yenye utulivu zaidi ili awalishe madini mastaa wa timu hiyo kabla ya kumliza Mwarabu, akiamini kambi hiyo itasaidia kujenga umoja wa timu na kupunguza makosa ambayo wachezaji hufanya wanapofanya mazoezi wakitokea makwao.

Mmoja wa viongozi wa Simba (jina tunalo) ameliambia Mwanaspoti kuwa jambo hilo litajadiliwa na muafaka unaweza kutolewa leo kama timu iende Zenji au isalie Dar es Salaam katika kambi yenye utulivu mkubwa kama anavyotaka kocha Benchikha.

Mbali na hilo inaelezwa Benchikha na mabosi wa Simba wanapiga hesabu ya kuhakikisha wachezaji wote walioitwa kwenye timu zao za taifa ikiwamo Taifa Stars ya Tanzania kwa ajili ya mechi za kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya Fifa wanarahisishiwa usafiri ili kuwawahi wenzao mapema kwa mchezo huo.

Mastaa saba wa Simba, Aishi Manula, Kibu Denis, Kennedy Juma na Mohamed Hussein ‘Zimbwe JR’ wameitwa Taifa Stars, huku Mzambia Clatous Chama akiitwa Chipolopolo na Mrundi Saidi Saido Ntibazonkiza akiitwa kwenye kikosi cha Intamba mu Rugamba.

Kutokana na ratiba za mechi za mataifa wanayochezea wachezaji hao zinaonyesha kila taifa litakuwa uwanjani Machi 25, hivyo kurejea kikosini Simba itakuwa kuanzia Machi 27, ikiwa ni siku mbili kabla ya kuvaana na Al Ahly Kwa Mkapa.

Bosi huyo wa Simba, amesema mbali na ombi la kocha kutaka wachezaji hao kuwahi mapema kambini, lakini hata wao viongozi wa juu walishajipanga mapema kufanya utaratibu wa kuyaomba mashirikisho ya soka wanapotoka nyota hao kuwaruhusu wasalie Simba badala ya kujiunga na timu za taifa.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema hatma ya kila kitu kitafahamika leo Jumatatu baada ya viongozi na wachezaji kukutana.

“Baada ya mechi na Mashujaa (Ijumaa), timu ilikuwa na mapumziko. Kesho (leo) ndio tunarejea kazini.

Kila jambo litafahamika leo ikiwemo kambi na hilo la wachezaji walioitwa timu zao za taifa na tutatoa taarifa kamili,” alisema Ahmed.

Simba iliyotinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya nne kati ya misimu sita iliyoshiriki baada ya kushika nafasi ya pili katika Kundi B lililoongozwa na Asec Mimosas ya Ivory Coast ambayo imepangwa kukutana na Esperance ya Tunisia katika mchezo wao wa robo fainali hizo.

Kocha Benchikha aliyetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akiwa na USM Algers ya Algeria na CAF Super Cup kwa kuinyoa Al Ahly kabla ya kutua Simba amepania kumaliza mechi nyumbani kabla ya marudiano ili kuivusha timu nusu fainali ikirejea rekodi ya mwaka 1974.

Mwaka huo Simba ilicheza nusu fainali na kufungwa na Mehalla El Kubra ya Misri kwa mikwaju ya penalti 3-0 baada ya kila moja kushinda mechi ya nyumbani kwa bao 1-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1 na kwenye penalti mambo yaliwaendea mrama Wekundu na kutolewa na Wamisri.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: