Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha atanii amvuta mido Mchadi, Kanoute atibua mambo

Eric Mbangossoum.jpeg Benchikha atanii amvuta mido Mchadi, Kanoute atibua mambo

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha hataki utani, kwani baada ya kukiangalia kikosi hicho alichoanza kukifundisha wiki mbili zilizopita amebaini anahitaji kiungo ‘mkata umeme’ wa kusaidia kuifanya timu kuwa na muunganiko mzuri eneo la kati hadi mbele na fasta akatoa jina la mido fundi kutoka Chad.

Benchikha aliyepewa mkataba wa mwaka mmoja na nusu alitua Msimbazi akitoka kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na CAF Super Cup akiwa na USM Alger ya Algeria aliyoachana nayo baada ya kuipa mataji hayo mawili, amependekeza kusajiliwa kwa Eric Mbangossoum na tayari mazungumzo yameanza rasmi.

Kiungo mkabaji huyo anayeichezea timu ya taifa ya Chad atakuwa mchezaji wa kwanza kwa Benchikha kumpendekeza baada ya winga mzawa, Ladack Chasambi aliyepo Mtibwa Sugar anayedaiwa tayari ameshamalizana na klabu hiyo mapema.

Habari kutoka ndani ya klabu ya Simba zinasema kwa sasa mabosi wa timu hiyo wameanza mazungumzo na Eric baada ya Benchikha kuwaeleza anamhitaji mtu huyo kikosini.

Eric Mbangossoum mwenye umri wa miaka 23 kwa sasa anaitumikia klabu ya Union Touarga ya Morocco, nchi ambayo Benchikha amewahi kufanya kazi akizinoa klabu kadhaa ikiwamo Mouloudia d’Oujda, Difaa El Jadida, Raja Casablanca na RS Berkane kabla ya kujiunga na USM Alger kisha kutua Msimbazi mwezi uliopita.

Chanzo makini kutoka ndani ya klabu ya Simba, kinasema kuwa kocha Benchikha ndiye aliyependekeza jina la kiungo huyo akisema ataifaa timu hiyo kutokana na uwezo wake wa kukaba kwa akili na kuituliza timu.

Kwa muda mrefu, Simba imekuwa na uhitaji wa kiungo mkabaji atakayeweza kuwaongezea nguvu mabeki wa kati licha ya kuwasajili na kuwatumia viungo kadhaa wa nafasi hiyo akiwamo Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin kwa nyakati tofauti.

Inaelezwa, tangu Benchikha atue kikosini hajaridhishwa na ubora wa viungo hao wanaocheza eneo hilo na haraka akawaagiza mabosi wake kumalizana na raia huyo wa Chad aliyewahi kucheza soka la kulipwa Cameroon, Guinea ya Ikweta kabla ya kuibukia Morocco anakocheza kwa sasa.

Pia inaelezwa kitendo cha kumkosa Kanoute katika mchezo ujao wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba itakaporudiana na Wydad ya Morocco kutokana na kutumia adhabu ya kupewa kadi tatu za njano, imemvuruga Benchikha na kuwasisitiza mabosi wa klabu hiyo kufanya usajili huo haraka iwezekanavyo.

Kukosekana kwa Kanoute kunaifanya Simba kusaliwa na viungo wakabaji wawili pekee Mzamiru na Ngoma ambao wamekuwa wakitumika mara kwa mara.

ERIC MBOGOSSOUM

Amezaliwa Mei 26, 2000 katika jiji la N’Djamena kuanza kucheza soka la ushindani mwaka 2017 aliposajiliwa Racing Bafoussam ya Cameroon kwa msimu mmoja kabla ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Chad akiwa na Elec-Sport mwaka 2018 na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa msimu huo.

Pia amecheza soka la kulipwa katika klabu ya Futuro Kings ya Guinea ya Ikweta na mwaka 2020 alitua rasmi Union Touarga ya Morocco aliyonayo hadi leo akisaidia kuipandisha daraja na kwenye soka la kimataifa kwa timu ya taifa alianza kuichezea tangu mwaka 2019 alipoitwa kwa mara ya kwanza 2019 na kucheza mechi ya kuwania Fainali za Kombe la Dunia chini ya Kocha Emmanuel Tregoat dhidi ya Sudan na timu hiyo kulala 3-1.

Kiungo huyo anasifika kwa kutumia miguu yote miwili, kukaba kwa kutumia akili mbali na umahiri wa kutoa pasi kiufundi na kuituliza timu pale inaposhambuliwa akisaidia ukuta wa timu ndani ya timu ya taifa na hata klabu anayoichezea kwa sasa.

PAZIA la michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 64 Bora linafunguliwa leo kwa mechi tano tofauti, huku vigogo Simba na Yanga zikiwa kwenye utata wa kucheza mechi ndani ya mwaka huu kutokana na kubanwa na ratiba ya viporo vya mechi za Ligi Kuu na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ratiba inaonyesha Cosmopolitan itakuwa wenyeji wa Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Dodoma Jiji ikikwaruzana na Magereza Dar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na Ihefu itaialika Rospa FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Highland Estate mkoani Mbeya.

Mechi nyingine za leo JKT Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kurugenzi ya Simiyu kwenye Uwanja wa Azam Complex, ilihali Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga itavaana na Greenland FC ya Kagera kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Mechi hizo zitachezwa kwa dakika 90 na ikishindikana kupatikana kwa mshindi,zitapigiana penalti ya atakayeibuka kidedea atasonga mbele kutinga hatua ya 32 Bora, huku vigogo Simba, Yanga, Mtibwa Sugar na Kagera wenye mechi za viporo vya Ligi Kuu ratiba za michezo yao ya ASFC hazijapangiwa siku.

Yanga ndiyo watetezi wa michuano hiyo ikitwaa taji msimu uliopita kwa kuitungua Azam FC kwa bao 1-0 na kwenye hatua hiyo imepangwa kucheza na Hausung ya Njombe, huku watani wao, Simba wakipangwa na Tembo ya Tabora, lakini hadi sasa kuna utata wa mechi za timu hizo kuchezwa lini kutokana na ratiba ngumu.

Ugumu upo zaidi kwa Simba kulinganisha na Yanga, japo mabosi wa klabu hiyo wameweka wazi kuwa kwa sasa wanasubiri waendeshaji wa michuano hiyo TFF kupanga wacheze lini kutokana na muingiliano wa ratiba za timu hizo.

Simba ina mechi ya Ligi Kuu itakayopigwa kesho Ijumaa kabla ya Jumanne ijayo kuumana na Wydad Casablanca ya Morocco, halafu itamalizana na KMC Desemba 23 kabla ya kusafiri hadi Kigoma kucheza na Mashujaa Desemba 26 na siku tatu baadaye itakuwa Tabora kuumana na Tabora United.

Januari Mosi, Simba itarudi Dar es Salaam kucheza mechi nyingine ya Ligi dhidi ya Azam kabla ya kusafiri hadi Zanzibar kwa michezo ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024.

Kwa upande wa Yanga itashuka uwanjani Jumamosi kuvaana na Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu kabla ya Desemba 20 kucheza na Medeama katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya Desemba 22 kuumana na Tabora United mjini Tabora na Desemba 29 itakwaruzana na Mashujaa.

Kagera yenyewe imepangwa kuumana na Dar City mjini Bukoba na Mtibwa Sugar kuialika Nyakangwe ya Geita, Uwanja wa Manungu, lakini ratiba kwa sasa bado hazijapangwa.

Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo alipoulizwa jana juu ya ratiba ya mechi za Simba na Yanga, alisema watazipanga kulingana na nafasi zitakavyopata, huku akidai kwamba hana uhakika kama mechi za vigogo hao zinaweza kuvuka hadi mwakani kwa sababu nafasi bado ipo.

Kwa upande wa maofisa habari wa Simba na Yanga, Ally Kamwe (Yanga) na Ahmed Ally wa Wekundu wa Msimbazi walisema kwa nyakati tofauti walipozungumza na Mwanaspoti kuwa wanasubiri ratiba zitakazopangwa na TFF na timu zao zitakuwa tayari kucheza, ingawa ni kweli ratiba kwa sasa zinazibana timu hizo zinazowakilisha nchi kimataifa zote zikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika zikiwa katika hatua ya makundi.

Msimu uliopita Yanga ilibeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam kwa kuifunga Azam FC katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Juni 12, mwaka huu.

Katika mchezo huo, Yanga ilibeba ndoo kwa bao lililofungwa na Kennedy Musonda katika dakika ya 16 aliyeunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na winga Tuisila Kisinda.

Kisinda alikuwa akicheza Yanga kwa mkopo kutoka Berkane ya Morocco alikorejea baada ya msimu kumalizika.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: