Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha aipiga bao Yanga, abeba winga

Winga Benchikha Benchikha aipiga bao Yanga, abeba winga

Mon, 4 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba tayari imerejea nchini kutoka Botswana ilikoenda kulazimishwa suluhu na Jwaneng Galaxy katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, huku taarifa tamu kwa mashabiki wa klabu ni kusainishwa kwa winga anayejua kufunga na kuasisti aliyekuwa akiwaniwa pia na vinara wa Ligi Kuu, Yanga.

Winga aliyesainishwa mkataba wa miaka miwili baada ya benchi la ufundi chini ya kocha mkuu mpya, Abdelhak Benchikha kuridhia ni Ladaki Chasambi anayekipiga Mtibwa Sugar akiwa amepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana ya U20 inayoshikilia ubingwa wa Ligi ya umri huo kwa msimu wa tano mfululizo.

Usajili wa Chasambi ni wa kwanza kwa Benchikha na Simba kwa ujumla ukija kabla hata dirisha dogo la usajili halijafunguliwa, kwani kalenda inaonyesha litafunguliwa Desemba 16 na habari za ndani kutoka Mashamba ya Manungu, Turiani yalipo maskani ya Mtibwa ni kwamba dogo huyo kwa sasa ni Mnyama.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya Mtibwa, zimefichua kuwa, Simba imekubali kununua mkataba wa miaka miwili aliokuwa nao Chasambi na klabu ya Mtibwa, kisha fasta ikamalizana na Mchezaji Bora huyo wa U20 2023 ili dirisha likifunguliwa tu, aanze kukinukisha Msimbazi.

“Kuna kiasi ambacho Mtibwa ilikiweka kwa timu inayomhitaji Chasambi ili iwe tayari kumuuza. Kuna timu kadhaa ambazo zilifanya mazungumzo na mchezaji, lakini Simba ndio ambayo imeifuata Mtibwa mezani na kufanya mazungumzo,” kilisema chanzo hicho kutoka ndani ya Mtibwa (jina tunalo), aliyeongeza;

“Kile ambacho Mtibwa wamekihitaji ili kumuachia mchezaji, Simba wamekubali kukilipa na kwa upande wa maslahi ya mchezaji, wapo tayari kumpa kile ambacho anakitaka.”

Gazeti hili linafahamu, mbali na Simba, timu nyingine zilizokuwa zikimfukuzia winga huyo ambaye hivi karibuni aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars, ni Yanga na Singida Fountain Gate.

Chasambi mwenye umri wa miaka 19, anasifika kwa umahiri wake wa kumiliki mpira, kupiga chenga na kutoa pasi zenye macho, mbali na uwezo wa kufunga na kuasisti, ambapo hadi sasa katika Ligi Kuu amefunga bao moja na kuasisti mara tatu.

Katika misimu miwili iliyopita, mchezaji huyo aliibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Ligi Kuu ya Vijana U-20 akiwa na Mtibwa inayoonekana kama imejimilikisha taji la michuano hiyo, kwa kulibeba misimu mitano mfululizo ikiwamo ya msimu uliopita ilipoifunga Azam kwenye fainali.

Simba iliyopo nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ikiwa na pointi 19 bada ya kucheza mechi nane tu, inadaiwa ipo kwenye mipango ya kushusha majembe wa kuimarisha kikosi hicho chini ya Benchikha aliyechukua nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’, huku ikielezwa kocha huyo atafyeka wengine wanaoonekana kuwa mzigo.

Benchikha mwenyewe alikaririwa na Mwanaspoti akisema, anaendelea kuwasoma wachezaji kabla ya kufanya maamuzi, akizingatia ana muda mchache hadi dirisha dogo litakapofunguliwa wiki ijayo na kiu yake ni kuona Simba inafika mbali kwenye michuano ya ndani na ile ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: