Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha: Ubingwa unakuja, awaachia goma Freddy, Jobe

Jobe X Freddy Benchikha: Ubingwa unakuja, awaachia goma Freddy, Jobe

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa kikosi cha Simba, Abdelhak Benchikha amezungumzia nyota njema anayoiona kwenye kikosi chake baada ya kikao kizito na nyota wake na kwamba kiwango chao katika mechi iliyopita ndio kiwango cha timu inayotaka ubingwa.

Kabla ya mechi dhidi ya Tabora kocha huyo alizungumza na washambuliaji wake wapya Pa Omar Jobe na Freddy Michael Koublan akiwapa mbinu za namna ya kucheza bila presha.

Aliwaeleza Simba ni timu kubwa yenye mashabiki wengi na ushindani mkubwa hivyo lazima watulize presha na kutokufuatilia mambo ya mitandao.

Kikao hicho kilicholeta matokeo baada ya mechi dhidi ya Tabora United ambapo wekundu hao waliuwasha moto na kuwaachia kipigo kizito cha bao 4-0, na kikubwa ni kwamba wafungaji katika timu hiyo wamezidi kuongezeka.

Mabao hayo yaliyofunguliwa na mshambuliaji mpya Jobe dakika ya 18 kufuatiwa na Sadio Kanoute, beki Che Malone Fondoh na kumaliziwa dakika za mwisho na mgeni kutoka Ivory Coast, Freddy.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa na furaha kubwa kocha huyo alieleza kuwa, kiwango kilichooonyeshwa na kila mchezaji katika mchezo huo kimemfurahisha sana.

Alisema mechi ziko karibukaribu, hivyo ili waendelee kucheza kwa nguvu na ubora uleule, atagawa mechi kwa nyota wake wakiwamo kina Jobe, Freddy na wengineo ili kila mmoja aonyeshe alichonacho katika kuipigania timu, lakini hiyo itategemea na ushindani watakaouonyesha kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi.

“Kile walichokionyesha wachezaji wote kimenipa furaha kama kocha kwani kila mmoja ametendea haki nafasi aliyopewa na kuonyesha shauku ya kuwa kwenye namba nzuri katika ubao wa msimamo wa ligi.

“Sasa waanze safari ya kwenda mbele kupigania mataji kuanzia hapa hawatakiwi kurudi nyuma kwa kucheza vibaya bali waimarike kwa kucheza vizuri zaidi,” alisema Benchikha.

Mashabiki wa timu hiyo wanaonekana kutaka kuona uwezo wa washambuliaji wao wapya baada ya kuondoka kwa Jean Baleke aliyekuwa na mabao manane msimu huu, sawa na alivyofunga msimu uliopita. Simba pia iliachana na Moses Phiri aliyekuwa na mabao 10 msimu uliopita na huu akicheza muda mwingi akitokea benchini na kuondoka akiwa amefunga mabao matatu.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: