Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barua ya hisia kwa Shomari Kapombe

Kapombe Simba G Shomari Kapombe

Tue, 30 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mambo yangeweza kuwa tofauti kama stori niliyoisikia inaweza kuwa kweli. Juzi Shomari Kapombe alikuwa akisheherekea siku yake ya kuzaliwa. Januari 28. Angeweza kuwa anasheherekea siku hii akiwa Abidjan na wenzake wa timu ya taifa akijiandaa kurudi nchini baada ya michuano ya mataifa ya Afrika pale Ivory Coast.

Haikuwa hivi. Shomari amesheherekea katika kambi ya Simba. Mtandao unaonyesha ana umri wa miaka 32. Wakati fulani yeye na mlinzi mwenzake wa pembani wa Simba, Mohammed Hussein waliachwa katika kikosi cha timu ya taifa cha kocha, Adel Amrouche. Kulizuka maneno mengi ya mashabiki ambao hawakukubali.

Baadaye mwenzake akarudi lakini yeye hakuitwa. Maneno yalitulia kwa sababu hapo katikati upepo uliwaendea ovyo wote wawili huku mashabiki wa timu yao wakigeuka kwa kuamini kwamba hawakuwa katika ubora wao na huenda walikuwa wamechoka.

Lakini sasa Shomari hayupo kabisa na mashabiki wameridhika. Mashabiki wameridhika pia na namna ambavyo Taifa Stars ilivyocheza katika michuano ya mataifa ya Afrika. Inaashiria mwisho wa Shomari kikosini? Siamini. Wachezaji huwa wanazama na kuibuka.

Lakini labda pia Shomari anaelekea mwisho. Inawezekana. Miaka 32 ya Pasipoti sio haba. Tuachane na habari ya miaka ya ukweli. Nimeikumbuka bethidei ya Shomari kwa mambo mawili. Yote haya yanatokana na namna ambavyo kwa sasa anatajwa kama mzee lakini pia hayupo katika kikosi cha Stars.

Lakini pia nimekumbuka kwa sababu huenda sasa hivi ndio anafunga hesabu zake za mwisho mwisho za masuala ya kipato wakati huu akisubiri labda kusaini mkataba mmoja mkubwa wa mwisho kama Simba itakuwa haijapata mrithi wake.

Nimekumbuka namna ambavyo Shomari alipoteza nafasi ya kucheza soka la kulipwa ulaya akianzia katika klabu ya Cannes ya Ufaransa. Ni takribani miaka 10 iliyopita sasa. Ilikuwa mwaka 2013. Nasikia Shomari alikubalika lakini klabu ilimpa muda wa kuzoea Ulaya na kuendelea kufanya mazoezi kabla haijaendelea na mipango mingine.

Wakati ule alikuwa kinda. Ulaya ilikuwa mpya kwake na si ajabu alipata ule ugonjwa wanaoupata wachezaji wengi wa Kitanzania wanapokwenda nje. Ugonjwa wa kukumbuka sana nyumbani (Home sickness). Hata raia wa kawaida huwa tunaupata huu ugonjwa tunaposafiri kwenda ugenini.

Unakuwa unafurahi siku ya kwanza na ya pili. Baada ya wiki unaanza kukumbuka nyumbani. Unawakumbuka washkaji. Unamkumbuka mpenzi wako. Unakumbuka chakula. Unakumbuka kila kitu kuhusu nyumbani na mazingira.

Inawezekana Shomari alikumbwa na hili. Azam wakatumia nafasi kumrudisha nyumbani na akaipokea haraka. Tena kwa mikono miwili. Huku akaunti pia ikinona. Hapa ndio ilipo tofauti kati ya wenzetu wa Afrika Magharibi na sisi. Hapa ndipo ilipo tofauti kati ya wenzetu wa Amerika Kusini na sisi.

Kwa wenzetu huwa wanapenda kuutumia ule msemo wa Yanga wa ‘daima mbele nyuma mwiko’. Sisi ni waoga wa maisha na hatupigi hesabu za mbali. Hatupigi hesabu za uvumilivu na namna ya kujenga maisha kupitia soka.

Katika umri wa miaka 32 kama Shomari angekuwa anachezea CSKA Moscow au Parma ya Italia bado angekuwa mchezaji lulu katika kikosi cha timu ya taifa. Sidhani hata kama kungekuwa na majungu yoyote kutoka kwa kocha.

Kule nje kadri unavyocheza ndivyo unavyozidi kuimarika na kuepuka mambo mengi ndani na nje ya uwanja. Matibabu safi, afya bora, viwanja bora, huduma bora, mshahara mzuri na mengineyo. Haya yanadumisha zaidi ubora wa mchezaji anayecheza nje kuliko anayecheza Tanzania.

Katika umri huu pia, ndani ya miaka 10 Shomari angekuwa amekusanya euro nyingi kuliko shilingi alizokusanya Tanzania. Hizi ndio hesabu za wenzetu. Lakini pia ndani ya miaka 10 Shomari angekuwa mwanadamu aliyekomaa kiakili zaidi kuliko ilivyo leo.

Wenzetu wanaoishi katika nchi zilizoendelea huwa kama vile wapo darasani. Wanaona vitu vingi, wanajua vitu vingi, wanajifunza vitu vingi, wanakuwa na ubunifu mwingi. Haishangazi kuona Mnigeria mpira ukimshinda ughaibuni anaendelea kuishi huko huko mpaka kieleweke.

Kabla hatujafika huko ni lazima tuweke wazi kwamba Shomari asingeshindwa kutamba Ulaya. Mpaka sasa nakaa katika televisheni kuna walinzi wachache wa barani Ulaya ambao wangefikia uwezo wa Shomari kama angeongezewa mambo kadhaa barani Ulaya.

Shomari ana kasi, ana akili ya mpira, anajua kushambulia, anajua kukaba na zaidi ya kila kitu anajituma. Ambacho wazungu wangemuongezea awe kama walinzi wengine wa Ulaya ni misuli, ufahamu zaidi kuhusu soka uwanjani na mengineyo. Katika kipaji wasingeongeza chochote au kupunguza chochote kwa sababu amezaliwa nacho.

Kilichohitajika ni uvumilivu na mipango zaidi kutoka kwake. Kilichohitajika zaidi ni kuwa na menejimenti ya kumsimamia na kujua anataka nini katika maisha. Hata hivyo, majaribu ya kurudi Tanzania yalikuwa makubwa kuliko kubakia Ulaya.

Lakini hadi leo nina uhakika Shomari atakuwa na majuto fulani katika moyo. Anapotazama ligi mbalimbali za Ulaya anajua fika kwamba kuna wachezaji wengi wa nafasi yake hawana kipaji kama yeye. Basi tu ni Utanzania wetu na ukosefu wa ujasiri ndivyo vilivyomfanya aamue kurudi zake nyumbani.

Vinginevyo kila la kheri kwake. Kwa mpira wetu bado anaweza kumalizia miaka miwili mitatu iliyobaki. Bado pia ana nafasi kubwa kurudi katika kikosi cha Taifa Stars kwa sababu sioni maisha marefu hapa nchini kwa kocha aliyemkataa, Adel Amrouche.

Kinachoweza kummaliza ni mashabiki wa Simba tu ambao wamepungukiwa na imani naye kwa kiasi kikubwa na wanasubiri zaidi akosee wamlaumu kuliko kumtia moyo. Akiamua kuwapuuza akajitunza anaweza kuendelea kudumu kidogo. Hata hivyo, nafasi ya dhahabu kwake ilikuwa ile ya Cannes. Asingerudi nyuma.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: