Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Babacar Sarr: Walichokiona Mapinduzi hakijafika hata nusu ya kiwango changu

 Babacar Sarr Dimba.jpeg Kiungo mpya wa Simba, Babacar Sarr

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo mpya wa Simba, Msengal Babacar Sarr amewasikia mashabiki wa klabu hiyo ambao walijadili kiwango alichokionyesha kwenye mechi mbili za michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na kuwatumia salama akiwatoa hofu akiwahakikisha anakuja kuwapa burudani mara michuano itakaporejea mwezi ujao.

Sarr alisajiliwa kwenye dirisha dogo na mara alipotambulishwa aliwahishwa Zanzibar kwa ajili ya mechi za Mapinduzi na kushindwa kuwakuna mashabiki ambao walimjadili, lakini akiwa mapumzikoni Senegal, kiungo huyo aliliambia Mwanaspoti anakuja kuwapa raha mashabiki kwani anakiamini kipaji alichonacho.

Kiungo huyo aliyetua Msimbazi kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na US Monastir ya Tunisia, alisema mashabiki wa soka nchini hawajashuhudia hata nusu ya ubora wake kwani mechi mbili za Mapinduzi alizocheza alikuwa hajafanya mazoezi na timu pia alikuwa na uchovu kiasi.

“Nipo mapumziko, lakini siku chache zijazo nitakuwa Tanzania, nakuja kufanya kazi. Najua mashabiki wengi wanasubiri kuona nini nitafanya, niwatoe hofu tu kuwa walichokiona kwenye mechi zile mbili hakifiki hata nusu ya ubora nilionao, nilikuwa na uchovu pia ugeni kikosini, nakuja kuwapa furaha,” alisema Sarr na kuongeza;

“Najua Simba nini inataka kutoka kwangu na nipo tayari kufanya hivyo kwa manufaa ya klabu, nitafanya kila ninaloweza ili kuhakikisha timu inafikia malengo huku nikiwa miongoni mwa waliofanikisha hilo kutimia.”

Kiungo huyo aliyewahi kuzichezea timu za AS Pikine, Wallydann, Mbour PC, Teungueth FC zote za Senegal pamoja na Olympique Beja na Monastir za Tunisia alisema hamhofii kiungo yeyote kwani anajiamini na anaijua vyema kazi yake.

“Kila mchezaji ana ubora wake uwanjani na nawaheshimu wote lakini siwahofii, siwezi kuongelea zaidi ubora wa viungo wengine kwani sijawaona vyema, tusubiri nipate muda wa kucheza kisha tofauti itaonekana uwanjani,” alisema Sarr aliyewahi kumkaba staa wa soka duniani Cristiano Ronaldo kwa dakika 90 katika michuano ya Kombe la Klabu za Kiarabu iliyomalizika kwa Al Nassr ya Ronaldo kushinda 4-1 dhidi ya Monastir ya Sarr.

MSIKIE KIEMBA

Kiungo wa zamani wa Simba, Amri Kiemba alisema Simba ilihitaji kiungo mkabaji mwenye uzoefu na kama Sarr atakuwa na ubora katika eneo hilo basi ataisaidia timu kufikia malengo.

“Muda mrefu Simba ilikuwa ikimkosa kiungo mkabaji asilia, nadhani Sarr ndio eneo lake, hivyo kama atakuwa na ubora unaohitajika atakuwa msaada kwa timu, nadhani tumpe muda tuone anakuja na nini cha ziada,” alisema Kiemba aliyewika pia na timu za Yanga, Azam, Kagera Sugar pamoja na Taifa Stars.

Sarr ni miongoni mwa nyota sita waliosajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo la msimu wa 2023/2024 wengine ni washambuliaji Muivory Coast Freddy Michael Kuoablan, Mgambia Pa Omar Jobe na viungo Edwin Balua, Ladack Chasimba na Saleh Karabaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: