Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam sasa yampeleka Prince Dube Simba

Prince Dube 1 Prince Dube

Thu, 14 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Habari mpya ni kwamba Azam FC imewaruhusu Simba na Al Hilal ya Sudan kuzungumza na Prince Dube. Staa huyo aliandika barua ya kuvunja mkataba na Azam hivi karibuni, japo klabu hiyo ilimkomalia kwamba afuate masharti.

Azam ilitaka mchezaji huyo kuilipa kiasi cha Dola za Marekani 300,000 ambazo ni zaidi ya Sh700 milioni za Kitanzania lakini yeye akawaendea mezani akitaka kutoa dola 200,000 ambazo ni kama Sh510 milioni ili wamalizane kishikaji.

Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Azam imepokea ofa nono kutoka kwa Simba na Hilal baada ya kusikia sekeseke la mshambuliaji huyo aliyesajiliwa tangu mwaka 2020 na leo wameweka wazi kuwa, wametoa ruhusa kwa klabu hizo mbili kuzungumza na mchezaji ambaye amekuwa akihusishwa zaidi na Yanga.

"Tumepokea ofa mbili kutoka Simba na Hilal ya Sudan na tumewaruhusu kuzungumza na mchezaji, ofa zao zimekidhi matakwa yetu," alidokeza mmoja wa vigogo wa Azam.

Mwanaspoti linajua kwamba Simba imekubali kutoa dola 300,000 lakini italipa kwa awamu, ingawa Hilal wako tayari pia kuweka mzigo kama huohuo jambo ambalo huenda likaweka ugumu kwa Yanga ambayo awali ilikuwa ikihusishwa na mchezaji huyo ingawa haijapeleka ofa rasmi.

Mwanaspoti linajua kuwa sehemu kubwa ya Wakurugenzi wamekubaliana kwamba Dube aondoke wakikerwa na 'kitrendi' chake cha kuandika barua ghafla bila kusema chochote kwao hapo kabla kama kuna jambo haliendi vizuri.

Wengi wao wanaona kama alionyesha dharau kubwa na hakuna kingine zaidi ya kumruhusu aondoke ndipo siku chache zilizopita alirudisha vitu vyote vya Azam na kwenda kuishi hotelini akisubiri mchakato wake umalizike.

Awali, kabla ya taarifa ya leo ya Azam, Mwanaspoti liliripoti kwamba kuna vyanzo vitatu vinatajwa kama sababu ya Dube kuomba kuondoka, ikiwemo Yanga, Ihefu na timu za Zimbabwe, lakini vyanzo vya kuaminika vikasisitiza kwamba kuna kitu kinaendelea kimyakimya njiapanda ya Jangwani. Je, wataweka ofa ya kuwazidi Simba na Hilal mezani?

SIMBA

Wekundu hao wanaamini kwamba Dube ana uzoefu wa kutosha kwenye ligi ya ndani kuliko mastraika wote waliopo Msimbazi kwa sasa ambao ni Fred Michael na Pa Omar Jobe ambao wamesajiliwa kwenye dirisha dogo la Januari.

Awali, Simba iliwapiga chini Moses Phiri na Jean Baleke kwa nia ya kupata mastraika wengine bora zaidi yao lakini takwimu za wapya hao bado hazijawaridhisha viongozi wala mashabiki.

Rekodi za michuano mbalimbali zinaonyesha kwamba Dube amekuwa akiwafunga zaidi Simba kila anapokutana nao. Msimu huu amewafunga kwenye ligi mara mbili.

YANGA

Wanahitaji sana huduma yake. Wanaamini Prince Dube anaweza kuwa mtu sahihi wa kuziba nafasi ya Fiston Mayele ambaye hana furaha ndani ya Pyramid FC.

Inadaiwa kwamba Yanga wamekuwa wakihangaika kumshawishi mchezaji huyo kwa muda mrefu kutua katika kikosi hicho kutokana na uwezo wake.

Hivi karibuni wakati Azam FC ikiwa mikoani kwa mechi za Ligi Kuu, Dube alionekana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa akishuhudia mechi ya Yanga ambayo ilishinda mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad.

Dube hakusafiri na Azam kwa sababu ni majeruhi ambapo amekosa michezo kadhaa hadi sasa.

Nyota huyo hajacheza mechi ya Azam FC tangu Februari 19 alipoingia kipindi cha pili dhidi ya Tabora United.

Hakusafiri na timu katika mechi mbili za mikoani - Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons na Mwanza dhidi ya Singida Fountain Gate.

Lakini Mwanaspoti linajua kwa kawaida Azam FC husafiri na wachezaji wake hata kama ni majeruhi kama sehemu ya kujenga umoja. Hata hivyo, Dube hakufuatana na wenzake ikisemekana alikataa kusafiri kama sehemu ya shinikizo ili aachwe huru.

Habari za ndani ni kwamba inasemekana kuna mfanyakazi mmoja wa Yanga ambaye hapo kabla alikuwa Azam ndiye anayechora ramani ya Dube kuhamia Yanga ingawa kitendo cha Simba kupeleka ofa kinaweza kuwaweka ugumu.

IHEFU

Inaweza kuwa sapraizi lakini bado ni kwa asilimia ndogo. Wamiliki wapya wa Ihefu wanataka kumnasa mchezaji huyo kwa gharama yoyote wakiamini atawasaidia kurahisisha safari ya mafanikio ingawa hawajapeleka ofa.

Kwa mujibu wa habari za ndani kutoka kwa watu wa karibu na Dube, mabosi wa Ihefu ambao zamani walikuwa wakiimiliki Klabu ya Singida United iliyopanda daraja mwaka 2017, walitaka kumsajili wakati ule sambamba na Tafadzwa Kutinyu.

Lakini Dube alichagua kwenda Afrika Kusini ambako, hata hivyo, hakufanikiwa na kuamua kurudi Zimbabwe.

Lakini sasa wakiwa na timu mpya, mabosi wale wamerejea tena kwa Prince Dube na kuivuruga akili yake kwa ‘mzigo mrefu’ waliomuwekea mezani. Lakini akili yake haipo Ihefu anataka kucheza Dar es Salaam.

NYUMBANI ZIMBABWE

Habari kutoka Zimbabwe zinasema timu mbili za nchini humo zinaweza kutuma ofa muda wowote kumrudisha kijana wao.

Mwanaspoti linaijua Highlanders FC, timu aliyokulia Dube ambayo kwa sasa ina wamiliki wapya wenye 'mpunga mrefu' ambao wangependa kumrudisha nyota wao huyo kipenzi cha mashabiki wa timu.

Pia klabu ya Yadah FC ambayo hivi karibuni ilinasa saini ya nyota Khama Billiat nayo iko katika harakati za kumnasa Dube. Timu hizo mbili zinaitesa akili ya Dube, lakini Simba, Yanga zinawacheki tu.

Lakini taarifa nyingine zinasema Dube anaamini majeraha yanayomuandama pale Chamazi yanatokana na mambo ya nje ya uwanja hivyo anataka kuondoka ili kujiepusha nayo.

Mchezaji huyo alijiunga na Azam FC 2020 akitokea Highlanders ya Zimbabwe - timu yake ya utotoni.

Aliyaanza maisha ya Chamazi kwa furaha kubwa kabla hajaumia kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Novemba 25, 2020 na tangu hapo hakurudi kuwa Dube wa kabla ya kuumia.

Hadi anavunja mkataba Dube alishacheza dakika 734 katika jumla ya dakika 1800 za mechi 20 za Azam FC msimu huu. Dakika hizo alizocheza ni katika mechi 12.

Kwa kifupi ni kwamba Dube amecheza chini ya nusu ya dakika za jumla kama angecheza mechi zote msimu huu na hii ni kutokana na pancha za hapa na pale ambazo kimsingi zimekuwa zikimuandama katika misimu yote.

Katika dakika hizo 734 za mechi 12 ambazo amecheza amefunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao.

Mkataba wa Dube na Azam FC unatarajiwa kumalizika ifikapo Juni 2026, ikiwa na maana kwamba bado ana misimu miwili na nusu mbele.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: