Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

African Football League ni utajiri mkubwa

Ali Kiba AFL African Football League ni utajiri mkubwa

Fri, 20 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jiji la Dar Es Salaam, lililo katika Pwani ya Bahari ya Hindi juma hili litakumbwa na shamshamra za uzinduzi za mashindano ya CAF African Football League. Yawezekana litakuwa tukio kubwa la kimichezo kuwahi kutokea Dar es Salaam. Watakaokuwepo watashuhudia historia ya mpira wa miguu ya Afrika, hasa kwa mashindano ya klabu, ikiandikwa.

Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika (CAF) chini ya malezi ya Fifa limeanzisha mashindano makubwa kabisa ya klabu barani Afrika yanayojulikana kama African Football League (AFL).

Ligi hii ilianzishwa kwa jina la African Super League, lakini hata kabla filimbi ya kwanza haijalia, jina hilo likabadilishwa na kuwa African Football League katika kile kilichoonekana kama kukwepa kufananishwa na ligi iliyokuwa imependekezwa kutokana na uasi wa klabu kubwa za Ulaya.

Mwaka 2021, klabu za Ulaya kama Real Madrid, Barcelona, Arsenal, Chelsea, Spurs na klabu kubwa za Manchester zilikuja na wazo na kuanzisha ligi ya pekee ya Super League kinyume na utashi wa shirikisho la mpira la Ulaya (Uefa) na Fifa.

Mradi huo ulikufa, baada ya Uefa kutishia kuviondoa kwenye mashindano inayoyaandaa. Suala la Fifa kupingana na Super League ya klabu za Ulaya na kuiunga mkono kwa nguvu zote Super League ya Afrika limezua mjadala miongoni mwa wafuatiliaji wa mpira lakini tofauti ni kwamba haya ya Afrika yameanzishwa na kubarikiwa na CAF wakati yale ya Ulaya ulikuwa ni mradi wa klabu kubwa.

Pia, sheria ya ushindani ya Ulaya hairuhusu ligi kuwa na mfumo ambao unaweza kutoa viti maalumu kama ambavyo inachezwa ligi ya kikapu ya NBA (Marekani).

Filimbi ya kwanza ya African Football League inapulizwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwa mchezo wa robo fainali kati ya Simba ya Tanzania na Al Ahly ya Misri.

Huu utakuwa mchezo wa kihistoria utakaobaki katika vitabu vya kumbukumbu kwa muda mrefu lakini pia itakuwa ni rekodi katika vitabu vya fedha vya klabu ya Simba kwani itaingiza kiasi cha dola za Marekani milioni moja sawa na shilingi za Tanzania bilioni mbili na nusu bila kujali imeshinda au imepoteza.

Mchezo huo utahudhuriwa na viongozi wa juu wa Serikali ya Tanzania, Fifa, Caf, wageni mashuhuri na pia mashabiki kutoka ndani na nje ya nchi. Michezo mingine ya robo fainali itakuwa ni kati ya TP Mazembe ya DRC na Esperance ya Tunisia, Enyimba FC ya Nigeria na Wydad ya Morocco, Petro Luanda ya Angola na Mamelodi Sundown ya Afrika ya Kusini.

TP Mazembe ya Congo itacheza mchezo wake wa nyumbani jijini Dar Es Salaam kwa sababu zilizotajwa kama ukosefu wa miundo mbinu sahihi kwa mashindano haya nyumbani kwao DRC.Hii itakuwa ni neema nyingine kwa Tanzania.

Kifedha, African Football League inakuja na kapu kubwa kabisa kupita yote katika mashindano ya klabu Afrika. Pamoja na pesa za maandalizi ambazo zimetolewa kwa klabu nane zilizoteuliwa kuanzisha mashindano haya, klabu hizi pia zitapewa Sh.2.7 bilioni kwa kushiriki mchezo wa robo fainali.

Dau litaongezeka katika nusu fainali na fainali ambako bingwa ataibuka na kitita cha Sh.29 bilioni. Taasisi ya utalii ya Saudi Arabia (Visit Saudi Arabia) limeingia uba kama mdhamini mkuu wa mashindano haya huku makampuni mengine na televisheni kutoka sehemu mbalimbali duniani zikitarajiwa kuingia katika mlolongo wa udhamini.

Kumekuwa na maswali ya kwanini Football League inahusisha timu nane tu? Je mashindano haya yatakuwa na uendelevu au ni suala la msimu mmoja? Je, mashindano haya yatakuza mpira wa Afrika? Ni nini mustakabali wa mashindano yaliyopo kama ligi ya mabingwa?

Kwa mujibu wa CAF, mashindano haya yatatumia timu nane teule kwa msimu huu wa uzinduzi kisha kurudi kwenye mfumo uliopendekezwa awali wa klabu 24 zitakazokuwa zinashindana zikiwa na mtindo wa kupanda na kushuka daraja kutegemea na ufanisi.

Wasiwasi kuhusu uendelevu wa mashindano haya haujapata jibu la moja kwa moja. Hakikisho kubwa kwa CAF ni kwa sababu mashindano haya yana uungwaji mkono wa Rais wa Fifa Giani Infantino. Mpaka sasa mdhamini mkuu ambayo ni taasisi ya utalii ya Saudia imeingia mkataba wa mwaka mmoja. Mafanikio au mwelekeo utakaoonyeshwa na mshindano ya mwaka huu ndio utaweza kumshawishi mdhamini huyu na wengine kuendelea huko mbeleni.

Nafasi ya mashindano haya katika kukuza mpira wa Afrika imeelezwa bayana kwamba mapato ya mashindano haya tajiri yatachangia ukuzaji wa soka la vijana, vituo vya kukuzia vipaji na ujenzi wa miundombinu ya mpira hasa viwanja ambalo ni tatizo kubwa hapa Afrika.

Kabla ya ujio wa mashindano haya Ligi ya Mabingwa wa Afrika ndiyo yalikuwa mashindano makubwa yakishirikisha zaidi ya timu 70 huku 55 zikiwa ni mabingwa wa ligi zao. Kwa vyovyote itakavyokuwa African Football League inakwenda kuchukua nafasi ya Ligi ya Mabingwa kama mashindano makubwa tajiri zaidi ya klabu Afrika.

Angalia hadhi ya klabu zitakazoshiriki mashindano haya. Mfano katika msimu huu kuna Al Ahly Cairo, Wydad Cassablanca, Mamelodi, Esperance de Tunis, TP Mazembe na Enyimba zote zikiwa zimewahi kuchukua makombe ya Afrika pia Simba na Petro de Luanda ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Upande wa fedha unaitambulisha zaidi AFL kama ndiyo inakwenda kuwa ligi dume Afrika, mfano katika msimu huu, bingwa atakunja kitita cha Dola 11.5 milioni akiwa amecheza michezo mitatu tu. Hizi ni nje ya dola zaidi ya 2 milioni atakazokuwa amepata kwa kucheza robo fainali, nusu fainali.

Kwa sasa mshindi wa Ligi ya Mabingwa anapata kiasi cha dola 4 milioni huku akiwa ametokwa na jasho jingi kuanzia raundi za chini mpaka fainali. Mshindi wa AFL anapata dau kubwa kuliko mshindi wa mashindano ya pili kwa ukubwa katika Ulaya yaani yale ya Europa (Uefa Europa Cup) ambayo mshindi wake anapata milioni 9.5 akiwa amecheza michezo mingi zaidi.

Yote kwa yote, mashindano ya AFL ni fursa kwa maendeleo ya mpira wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.Ni mashindano ambayo yanaweza kuubadili mpira wa Afrika kuupeleka upeo wa juu kabisa hasa kutokana na uwekezaji utakaofanyika katika soka la vijana, wanawake na miundo mbinu ya soka. Safari inaanzia kwa Mkapa.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: