Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mkude kasepa Simba bila deni

Mkude Bukoba Jonas Mkude

Thu, 6 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imetoa Thank You kwa nyota wake kadhaa. Alianza Augustine Okrah. Kiungo mshambuliaji kutoka Ghana. Kisha wakafuata wengine akiwamo Victor Akpan, Nelson Okwa, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Jonas Mkude na kipa Beno Kakolanya.

Hakuna aliyehoji juu ya kuachwa kwa nyota wa kigeni waliosajiliwa Simba msimu uliopita. Hakuna aliyepinga kutemwa kwa Nyoni wala Gadiel, japo kwa Kakolanya kuliibua maswali kutokana na kujiuguza kwa kipa namba moja, Aishi Manula. Hata hivyo kwa vile ilishajulikana Kakolanya alishaaini mapema Singida Big Stars, kabla hata ligi haijamalizika, hivyo alichukuliwa poa.

Tayari Simba wenyewe walishamwekea makunyazi usoni kiasi cha kushindwa kumtumia kwenye mechi muhimu za mwishoni mwa msimu uliomalizika hivi karibuni, zikiwamo zile za ASFC na CAF.

Ishu imekuja kwa Mkude. Kiungo huyo fundi wa mpira, ameshtua baadhi ya wadau kwa namna Simba ilivyomuacha kihuni. Kwa namna Mkude alivyoichezea Simba kwa muda mrefu, ilidhaniwa alistahili kuagwa kwa heshima hata kabla ya kupewa 'Thank You'.

Manchester City ilimpa heshima kubwa kiungo mshambuliaji wao, Ilkay Gundogan aliyejiunga nayo mwaka 2016 tu kwa kumpa unahodha kwenye fainali mbili tofauti ikiwamo wa FA na UEFA ikiwa ni njia ya kumuaga kwa heshima kabla ya juzi kati kutua Barcelona ya Hispania.

Kelele za baadhi ya wadau, zimefanya mabosi wa klabu hiyo kujishtukia na kudai itamuaga kwa mechi maalumu.

Achana na tetezi zinazoendelea kwamba kiungo huyo mgumu anajiandaa kuhamia mtaa wa pili kwa kupewa mkataba wa mwaka mmoja, Mkude anaondoka Msimbazi akiwa hata deni lolote analodaiwa na wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu ya Simba.

MIAKA 13 YA HESHIMA

Mkude amejianza kucheza kwenye timu ya vijana wa Simba mwaka 2010 kabla ya 2011 kupandishwa timu ya wakubwa na kuwa msimu wa kwanza kwake katika Ligi Kuu Bara. Tangu lipoingia Simba hakuwahi kutoka, licha ya misukosuko kadhaa aliyokumbana nayo wakati mwingine kutokana na ishu za utovu wa nidhamu.

Katika miaka hiyo 13 Mkude, ambaye kuna wakati flani alikuwa nahodha wa kikosi hicho kabla ya kuvuliwa kitambaa akiwa kambi ya maandalizi ya msimu nchini Afrika Kusini, ametwaa mataji ya kujivunia ambayo kuna abaadhi ya wachezaji waliodumu kwa muda mrefu kwenye vikosi vyao hawajawahi kutwaa.

Ndio Mkude kabeba kila kila ukiondoa taji la michuano ya CAf kwa ngazi ya klabu, lakini kwa hapa ndani kakomba kila kitu kuanzia Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC), Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi na mengineyo yaliyoibuliwa na kufa. Rekodi zinaonyesha kuwa msimu wa kwanza wa kuichezea Simba alibeba taji la Ligi Kuu Bara tena kwa kishindo kwani alikuwepo kwenye kikosi kilichoinyoa Yanga kwa mabao 5-0. Kwa waliosahau, dogo aliingia kipindi cha pili kumpokea kaka yake, Mwinyi Kazimoto wakati vijana wa Jangwani wakipigwa kama ngoma na Wekundu wa Msimbazi iliyokuwa chini ya Mwenyekiti, Ismail Aden Rage.

Kisha akatwaa mengine manne mfululizo kuanzia msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021, pia amebeba Ngao ya Jamii mara nne kuanzia 2012, 2018, 2019 na 2020 kabla ya Yanga kutibua misimu miwili mfululizo iliyopita.

MATAJI MATATU ASFC Mkude pia kabeba ASFC mataji matatu ya msimu wa 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021 kabla ya mataji hayo kuahami Jangwani anakotajwa kuwa mbioni kujiunga nako, wakati kwa Kombe la Mapinduzi mwamba kabeba mara tatu kati ya mataji manne iliyotwaa Simba. Mkude katwaa nao mwaka 2011, 2015 na 2022, taji alilolikosa ni lile la mwaka 2008 kwani wakati huo alikuwa yupo Mwanza na huenda hakufikiria kama angekuja kuichezea Simba kwa mafanikio hayo.

Taji jingine alilobeba kiungo huyo ni kile la Simba Super Cup lililoibuliwa ghafla ya klabu hiyo, lakini aliwahi kubeba taji la Uhai Cup akiwa na kikosi cha Simba B 2010, kisha mwaka 2012 timu hiyo ilibeba BancABC Super8 ikitumia kikosi cha vijana akiwamo waliocheza sambamba na Mkude, kama Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Edward Christopher, Abdallah Seseme na wengine, lakini kiungo huyo yeye hakujumuishwa moja kwa moja kama wenzake.

HUKO CAF BALAA Achana na michuano ya ndani, huko kimataifa Mkude pia ameweka heshima yake ya kuwepo kwenye kvikosi vilivyofika hatua ya robo fainali tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu wa kwanza kuibeba Simba ilikuwa ni 2018-2019 akishiriki kufunga moja ya mabao yaliyoivusha timu kucheza makundi mbele ya Nkana FC ya Zambia, hiyo ilikuwa mara ya kwanza wa timu hiyo tangu ilitinga hatua hiyo mwaka 2003 kwa kuivua ubingwa Zamalek ya Misri. Msimu wa pili ulikuwa 2020-2021 na kuweka relodi ya kumaliza kama kinara wa Kundi A mbele ya watetezi Al Ahly, ila ikaenda kukwamisha na Kaizer Chief kwenye mechi za robo fainali na kumaliza mwendo katika hatua hiyo ya robo fainali kwa msimu wa pili.

Mkude alikuwa alikuwa kwenye kikosi cha Simba kilichofika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2021-2022 baada ya kuangushwa kwenye Ligi ya Mabingwa na Jwaneg Gallax na huko Wekundu hao walikomaa kuanzia hatua ya play-off hadi makundi na kukwama robo mbele ya Wasauzi wengine, Orlando Pirates kwa mikwaju ya penalti baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1.

Msimu uliomalizika hivi karibuni, Simba iliandikisha tena jina kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kukwama mbele ya watetezi, waliokuwa watetezi Wydad Casabalanca iliyoenda nusu kwa mikwaju ya penaltui na hatimaye kufika fainali na kufungwa na Al Ahly

SIMBA DAY SASA Kama hujui ni kwamba Mkude ndiye mchezaji aliyeshiriki matamasha mengi ya Wiki ya Simba maarufu kama Simba Day iliyoasisiwa mwaka 2009, kwani kati ya matamasha 14, mwamba ameshiriki 12 kuonyesha hana deni lolote aliloliacha kwa mashabiki wa klabu hiyo. Ameshiriki matamasha ya 2011, 2012, 2013, 2014, 2015, 2016, 2017, 2018, 2019, 2020, 2021 na 2022 na kushuhudia wachezaji mbalimbali wa ndani na wale wa nje ya nchi wakiingia na kutoka Msimbazi, kabla ya kutemwa hivi karibuni na kulikosa Simba Day mwa mwaka huu itakayofanyika Agosti 8.

Wasifu:

Jina: Jonas Mkude

Kuzaliwa: Desemba 3, 1992

Nchi: Tanzania

Urefu: Mita 1.79

Nafasi: Kiungo

Timu: Huru

Alikopita: Mwanza Utd, Hananasif FC, Simba U20, Simba

16 Mataji aliyobeba Jonas Mkude tangu alianza kuichezea Simba ya wakubwa mwaka 2011.

2022 Januari mwaka jana Mkude alishinda tuzo ya mwisho ya Mchezaji Bora wa Mashabiki wa Simba.

30 Miaka aliyonayo Mkude aliyezaliwa Desemba 3, 1992 na kuanza kucheza akiwa kijana mdogo.

2012 Mwaka Mkude alianza kutumika Taifa Stars, akiwa pia sehemu ya kikosi kilichoiua Yanga 5-0.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: