Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mambo matano Simba dhidi ya Al Ahly

Simba X Ahly 2 2.jpeg Mambo matano Simba dhidi ya Al Ahly

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jicho la mwewe nikiwa nimelitazama pambano la Simba dhidi ya Al Ahly nikiwa Houston Marekani. Wakati Lady Jay Dee ameimba kuhusu mambo matano mimi niliambulia mambo sita katika pambano hili la Ijumaa usiku.

Simba bado ipo mikononi mwa wenyewe

Hiki ni kitu cha kwanza nilichokiona. Nilikitazama kikosi cha Simba kilichoanza. Wachezaji wageni kikosini walikuwa Che Malone na Fabrice Ngoma. Wengine wote walikuwa wale wale tu. Ni tofauti na timu nyingine ambazo wachezaji wapya wanakuja kukipa nguvu kikosi.

Ni tofauti na watani wao ambao wameingiza wachezaji wengi waliokwenda kuisaidia timu moja kwa moja. Tulipigiwa kelele kuhusu mchezaji anayeitwa Willy Onana lakini kama ilivyo kwa mchezaji anayeitwa Skudu Makudubela kule kwa watani wao na yeye amegeuka kuwa Simba wa mapambano.

Hesabu wachezaji wapya ambao hawachezi Simba. Shaban Chilunda, Hussein Kazi, Hamis Athuman, David Kimeta ‘Duchu’ wote hawa wameshindwa kuingia kikosi cha kwanza cha Simba. Ni kama wamekuja kuongeza idadi Simba.

Luis Miquissone muda unakimbia

Tulimpeleka Luis Miquissone akiwa lulu pale kwa Mafarao halafu wao wakaturudishia garasa. Mara ya mwisho Al Ahly kufungwa Uwanja wa Mkapa walifungwa na yeye. Ijumaa jioni Miquissone alikuwa anakimbiza kivuli chake mwenyewe. Watu wa Simba watachoka kumsubiri. Haitapita muda mrefu.

Mwanzoni ilitajwa mwili wake ulikuwa umeongezeka nyama nyingi. Akazikata nyama hizo. Amerudi kuwa na mwili ule ule alioondoka nao lakini hana maajabu uwanjani. Simba walimrudisha kwa ajili ya mechi kama hizi lakini hakufikia walau robo ya uwezo wake aliouonyesha katika pambano la mwisho dhidi ya Al Ahly ambalo lilifanya Mafarao hao walipe kiasi kikubwa cha pesa kumchukua.

Miquissone anaiangusha timu. Yeye ni miongoni mwa wachezaji walioipa Simba hadhi hii ya sasa. Najua kutoka katika vyanzo vya ndani Simba wametumia pesa kubwa kumrudisha klabuni pengine kuliko kwa mchezaji yeyote katika historia yao. Kwa sasa wanamwonea aibu lakini inabidi aamke.

Kibu ni staa mpya Simba

Kibu Dennis alikuja kama mchezaji wa kawaida Simba. Vyanzo vyangu vinaniambia gharama iliyotumika ilikuwa kubwa kumnasa Kibu lakini haikuwa gharama ya kweli. Kama vile kulikuwa na upigaji fulani hapo katikati. Sawa hakuwa na thamani hiyo lakini Kibu anakaribia thamani halisi kwa sasa. Anaibeba timu. Ni mchezaji muhimu.

Watu walimkebehi sana baada ya kupewa uraia wa Tanzania kutokana na kukulia katika kambi za wakimbizi pale Kigoma. Kila alipopoteza pasi yake au angekosea basi watu wangekebehi “Hivi huyu kweli ndiye mchezaji wa kupewa uraia?”. Kibu aliziba masikio na sasa amegeuka mchezaji bora klabuni.

Kama nilivyozungumza hapo awali kuna wachezaji wameletwa pale Simba na ilitazamiwa hawa kina Kibu wakae nje lakini hadithi imekuwa tofauti. Zimepigwa sana kelele za kina Osamba Onana wakati usajili ukiendelea lakini leo Onana anakaa nje na Kibu anacheza. Kwa nini? Anajituma. Sio kwamba ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, hapana, lakini anatoa jasho kwa ajili ya timu. Bao la kusawazisha alilofunga Ijumaa lilimuacha akitibiwa jeraha kichwani. Hawa ndio wachezaji ninaowakubali.

Mpira mchezo wa maajabu

Waliokuwepo uwanja wa Mkapa na ambao tulitazama katika televisheni tumeendelea kuamini mpira ni mchezo wa maajabu. Inawezekana hakuna mtu ambaye amechukua pesa nyingi wiki hii kama ‘mganga wa Simba’. Ilikuaje Al Ahly wakawa wanakosa mabao yale? Inashangaza. Mganga lazima amejisifu.

Mpaka mapumziko Simba ilikuwa wawe nyuma kwa mabao manne. Kwenda mapumziko wakiwa wamefungwa bao moja ni jambo la kushangaza kidogo. Wangeweza kufungwa mabao mengi zaidi. Na haikuwa kwa sababu ya kipa Ally Salim. Al Ahly walikuwa wanakosa mabao wao wenyewe. Bila ya sababu zozote za msingi.

Ingekuwa nafasi zile wanakosa wachezaji wa Simba tungejisemea “pale Al Ahly hawakukosi”. Lakini hapa Al Ahly wenyewe ndio walikuwa wanakosa. Walikuwa na wachezaji wa hali ya juu lakini walikuwa wanakosa wenyewe mabao ya wazi. Hadi wakati tunakwenda mapumziko usingeamini pambano lingemalizika kwa sare ya 2-2. Al Ahly walionekana wangefunga zaidi huku Simba wakionekana hawakaribii kufunga.

Aishi anahitajika ofisini haraka

Kuna mabao unaweza kudhani ni ya kawaida kwa sababu ya mtu mwenyewe aliyepo langoni. Lakini kama anakuwepo kipa mwingine ndio unajua angeweza kufanya kitu tofauti. Ni kama inavyotokea Old Trafford. Kuna nyakati ‘saves’ za David de Gea walikuwa wanazichukulia poa. Ni mpaka alipokuja Andre Onana ndio wamegundua De Gea alikuwa anawaokoa sana.

Ally Salim amechangamka langoni lakini bado anawagharimu Simba. Kulikuwa na makosa mengi katika bao la pili la kusawazisha la Simba lakini Ally akafanya kosa la mwisho kushinda kuudaka mpira ambao kipa hodari angeweza kuudaka. Nilimkumbuka Aishi. Kama angekuwepo langoni si ajabu hadithi ingekuwa tofauti.

Simba walitazamiwa kuushikilia uongozi wao wa mabao 2-1 walau kwa dakika 10 ili Robertinho na benchi lake la ufundi wajipange lakini haikuwa hivyo. Ndani ya dakika moja tu uongozi wao ulipotea. Ally alipaswa kufanya vyema zaidi. Ngoja Aishi arudi aendelee kujifunza namna makipa bora wanavyofanya katika mechi kama hizi.

Yanga kazi wanayo Temeke na Cairo

Yanga kazi wanayo kweli kweli katika kundi lao walilopangwa na Al Ahly. Haitakuwa rahisi. Ijumaa walikuwa wamekaa katika makochi yao wakisubiri kuona Mnyama akipigwa nyingi Kwa Mkapa. Ni kweli angeweza kupigwa nyingi lakini haikutokea. Na sasa baada ya pambano la leo la marudiano la Simba pale Cairo kesi itawageukia wao.

Mpaka sasa naamini Yanga wana ubora kuliko Simba lakini Simba wanakuwa bora katika mechi za kimataifa kuliko wao. Msimu uliopita Yanga wamefanya kitu tofauti kwa kwenda fainali ya michuano ya Shirikisho. Wameshinda mechi nyingi ugeninini na kuweka rekodi ambayo hakuna timu ya Tanzania imewahi kufikia.

Hata hivyo, wana mechi mbili ngumu dhidi ya Al Ahly hasa ile iliyocheza kipindi cha kwanza Ijumaa jioni. Al Ahly ya kipindi cha pili inaweza kupigwa na Yanga lakini ile ya kipindi cha kwanza ilikuwa ya moto sana. Itakuwa kipimo kizuri cha Yanga hii ambayo imeanza kujinasibu kumudu mechi za kimataifa.

Nilimwona kocha Miguel Gamondi akitazama pambano hilo uwanjani. Hakwenda kujifurahisha. Alikwenda kutazama kazi ambayo inamkabili katika mechi mbili za kundi lao. Haitakuwa kazi nyepesi. Kama watamudu kupata walau pointi tatu au moja watakuwa katika nafasi nzuri ya kupita kwa sababu Al Ahly pia atakwenda kuadhibu na wengine.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: