Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Aishi Manula anapotazamwa kama malaika na shetani

Manula Arudi Langoni.jpeg Aishi Manula

Mon, 11 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nadhani mpaka sasa rafiki zangu Simba hawajui washike lipi kuhusu Aishi Manula. Ni malaika au shetani? Sijui. Ninachojua ni kwamba wanaishi katika mahusiano yenye mashaka mengi.

Labda kulikuwa na matukio kadhaa huko nyuma, lakini tangu Aishi aruhusu mabao matano katika pambano dhidi ya watani uhusiano wa mashabiki wa Simba na Aishi sio mzuri sana. Sio wa kujivunia kama ilivyokuwa hapo awali. Kuna mashabiki wa Simba wanaamini kwamba kama Ayoub Lakred angedaka siku ile, basi wasingefungwa mabao matano.

Kuna ambao wanakwenda mbali na kuamini kwamba kama Ally Salim angedaka siku ile basi yasingefika mabao matano. Kila nikirudia mabao yote matano sioni kosa la Aishi, lakini mashabiki wanaona lipo. Wakati mwingine inabidi ukubali tu kwamba labda tulikuwa tunatazama mechi mbili tofauti.

Achana na ukweli kwamba hakukuwa na bao lolote lililotokana na kosa la moja kwa moja kutoka kwa Aishi, lakini hakukuwa na sababu yoyote ya kumpanga Aishi. Alikuwa ametoka katika majeraha ya muda mrefu na asingeweza kuwa fiti kwa ajili ya mechi ya watani wa jadi.

Ni hapo tu unapoamua kukubali kwamba kuna wakati Simba wanamuona Aishi kama malaika na kuna wakati wanamuona kama shetani.

Kwamba kuelekea katika mechi ile ngumu dhidi ya watani hawakumuamini Ayoub. Walimuona Aishi kama malaika, lakini mara baada ya pambano kumalizika wakamuona Aishi kama shetani. Sidhani kama ulikuwa uamuzi wa Robertinho kumpanga Aishi. Klabu zetu zina mambo mengi ya ajabu kuelekea pambano la watani wa jadi, au pindi pambano lenyewe linapomalizika.

Wiki iliyopita Aishi alifungwa mabao mawili na Prisons pale Morogoro. Bao la kwanza lilikuwa la Aishi. Samson Mbangula alivuta mpira mrefu ambao Aishi alishindwa kupima kwamba Mbangula alikuwa amekokota vibaya mpira ule. Angeweza kuutokea na kuuosha, lakini akaamua kubaki langoni kwake na mfungaji akafunga kwa urahisi. Kwangu naamini lilikuwa kosa lake.

Bao la pili la Prisons likafungwa tena na Mbangula. Katika 'angle' ngumu ambayo Aishi alikuwa ameibana Mbangula akampiga tobo na kufunga.

Mara nyingi tunayaona haya mabao Ulaya. Ni rahisi kumfunga kipa palepale alipo. Akili yake inakuwa imegawanyika. Hajui alinde posti aliyopo au atanue mguu wake zaidi kuzuia mpira usiingie kwa ndani. Kwa wafungaji wazuri inakuwa rahisi kufunga kwa tobo.

Hili bao la pili halikuwa na lawama kwa Aishi. Bao la kwanza ndilo lilikuwa na lawama. Bahati mbaya nyingine kwa Aishi. Mashabiki wanapata mashaka juu yake. Ujinga wa mashabiki wetu ni kwamba huwa hawaoni kuwa kipa amefungwa kwa makosa ya kibinadamu. Huwa wanaona kwamba 'anatuhujumu' kwa makusudi.

Wakati mwingine huwa hawaoni kwamba huenda kiwango chake kimeshuka baada ya majeraha ya muda mrefu pamoja pia na benchi ambalo amekuwa akikalia baada ya kupona kutoka katika majeraha yake. Hapana. Jibu linalokuja ni kwamba anatuhujumu. Hizi timu zina lawama zilizopitiliza.

Lakini hapohapo wakati unamuona kuwa Aishi ni shetani ghafla unakumbuka kwamba huenda akawa ni malaika pia. Kwanza amefanya mengi katika jezi ya Simba. Haina ubishi. Lakini pili hauwezi kumuamini Ayoub kwa asilimia mia kiasi cha kumpuuza Aishi. Ayoub amekuwa na makosa yake mengi licha ya uhodari wake. Mfano ni bao alilofungwa na mtakatifu Lucas Kikoti, Jumamosi iliyopita jioni.

Lile bao kama angefungwa Aishi kungekuwa na maneno mengi. Ayoub alitoka nje ya eneo lake bila sababu za msingi. Kama angekuwa ametulia katika eneo lake Kikoti asingefunga. Bahati nzuri ni kwamba Simba walikuja kushinda baadaye. Bahati nzuri zaidi ni kwamba langoni hakuwepo Aishi kwa hiyo ikasamehewa kwa haraka.

Na sasa Aishi amebaki kuwa malaika na shetani. Kama kungekuwa na kipa wa pili ambaye ni hodari kama alivyo Aishi si ajabu kelele zingekuwa nyingi zaidi. Lakini tunachokiona hapa ni kwamba Simba hawana furaha sana na Aishi huku pia wakiwa na wasiwasi pindi anapokosekana langoni.

Lakini hapohapo pia wanajikumbusha mema mengi aliyowafanyia huku pia akiwa fahari yao linapokuja suala la timu ya taifa. Aishi ni Tanzania One.

Sijui mpaka lini Simba wataendelea kuwa na uhusiano wa mashaka na Aishi, lakini ninachodhani ni kwamba Aishi hana furaha Simba. Sio kwa sababu ya kusakamwa, bali ni kwa sababu pia amedondokea kuwa kipa wa pili wa Simba kwa sasa baada ya kocha Abdelhak Benchikha kuonekana kuwa na imani zaidi na Ayoub kuliko Aishi.

Ukifuatilia mwenendo wa lango la Simba ni wazi kwamba Ayoub ni kipa namba moja. Kwa mfano, Aishi alicheza dhdi ya Asec Mimosas ugenini kwa sababu Ayoub alikuwa na kadi mbili za njano. Wakati mwingine Aishi huwa anacheza kwa sababu Ayoub anakuwa na majeraha.

Tangu alikamate lango la Simba na timu ya Taifa, Aishi hajawahi kuishi katika mashaka kama anayoishi sasa hivi.

Kuna vitu viwili muhimu ambavyo inabidi vifanyike. Cha kwanza ni kwa Aishi mwenyewe kuwa mchezaji wa kulipwa haswa. Aipiganie nafasi yake katika lango la Simba.

Wachezaji wa kulipwa huwa wanapitia mambo mengi mojawapo likiwa hili ambalo Aishi anapitia. Unapochezea timu hizi haupaswi kuwa na moyo laini.

Lakini hapohapo mashabiki wa Simba wanapaswa kusimama nyuma ya Aishi. Mara nyingi mashabiki wa timu zetu wanapenda kuwaua wachezaji wao bila ya sababu ya msingi. Ni tofauti na mashabiki wa nchi nyingine zilizoendelea kisoka.

Sisi tunawaua wachezaji wetu kwa sababu za kipuuzi tu. Kuna wakati tunaamua kudai kwamba mchezaji fulani anatumika na wapinzani. Kuna wakati tunaamua tu kuamini kwamba mchezaji fulani amepitwa na umri. Kosa lilelile ambalo anaweza kufanya Henock Inonga huwa tunaweza kulitetea kwamba ni bahati mbaya. Kosa hilohilo akilifanya Saido Ntibanzokinza huwa tunasema kwamba ni kwa sababu ya uzee. Matokeo yake tumewafukuza wachezaji wengi uwanjani kabla ya umri wao.

Nadhani ni Simba wenyewe ndio ambao wanashikilia hatima ya Aishi. Wakitaka kumuua kisoka wanaweza. Wakitaka aendelee kuwa kipa namba katika lango la Msimbazi na timu ya taifa bado wanaweza. Nadhani Aishi anahitaji upendo tu. Hakuna kipa asiyefanya makosa duniani. Lakini hapohapo kitu cha msingi zaidi ni kutomtazama kwa jicho baya.

Tumeharibu wachezaji wengi katika siasa za soka za nchi hii kwa kuwatazama wachezaji kwa jicho baya. Unaweza kuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao kila siku wanatazamwa kwa jicho baya na mashabiki wa timu yao, kwamba wanatumika kumbe wanafanya makosa ya kibinadamu.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: