Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yapewa mbinu kuimaliza TP Mazembe

Mayele X Musonda Yanga yapewa mbinu kuimaliza TP Mazembe

Sun, 19 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Saa chache kabla ya Yanga kushuka uwanjani kukabiliana na TP Mazembe ya DR Congo kwenye mechi ya pili ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika, wakongwe wa zamani wa timu hiyo, wametoa mbinu za kivita ili kuwamaliza Wakongo Kwa Mkapa.

Yanga inaikaribisha Mazembe kuanzia saa 1:00 usiku ikitoka kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 kwa US Monastir ya Tunisia, huku mashabiki wakiwa na hamu ya kuona wanafuta uteja kwa Wakongomani hao waliowafunga nje ndani kwenye mechi za michuano hiyo mwaka 2016.

Abeid Mziba ‘Tekero’ aliyetamba kwa kufunga mabao ya vichwa, alisema soka ni mchezo wa mbinu na maandalizi na anaamini Yanga ikitulia kesho Kwa Mkapa itawazima Mazembe na ubora wao.

“Lazima wachezaji watumie nafasi wanazopata uwanjani kufunga mabao mengi, wasahau matokeo ya ugenini na historia ya kufungwa na Mazembe mwaka 2016, muhimu timu icheze kwa nidhamu na kupambana kwa muda wote wa dakika 90,” alisema Mziba.

Kiungo nyota aliyewahi kukipiga Simba na Yanga, Amri Kiemba alisema hii ni mechi mpya kabisa japo majina ya timu ni yale yale na baadhi ya nyota kutoka DR Congo, hivyo itakuwa rahisi kwa Yanga kushinda.

Kiemba alisema Mazembe ya sasa sio kama ya zamani japo wapo baadhi ya wachezaji ambao ni hatari huku akiitaka Yanga kuwaheshimu wapinzani wao na waende na akili moja tu ya kwenda kupata ushindi katika mchezo huo.

“Naiona mechi ya tofauti sana kutokana na ukubwa wa mashindano, Yanga inahitaji uimara kwa sababu udhaifu wowote ukitokea unaweza kuwa mlango wa kupata maumivu kwao, kitu cha muhimu kwa wachezaji wote wapambane kwelikweli uwanjani ili kuhakikisha inashinda nyumbani,” alisema Kiemba ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka.

Hii ni mechi ya tatu kwa timu hizo kukutana CAF, baada ya awali Juni 28, 2016 kukutana kwa Mkapa na Yanga kulala 1-0 kwa bao la Merveille Bokadi na kwenye mkondo wa pili, Agosti 23, 2016 Yanga ilichapwa tena 3-1 kupitia kwa Jonathan Bolingi na Rainford Kalaba aliyefunga mawili na bao la kufutia machozi la vijana wa Jangwani liliwekwa kimiani na Amissi Tambwe.

Yanga inaikabili Mazembe ikiwa na mastaa kutoka DR Congo akiwamo kinara wa mabao wa timu hiyo, Fiston Mayele, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa na Tuisila Kisinda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: