Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuna 'SAPRAIZI' inakuja Yanga, mjipange

Yanga Sapraizi ZNZ Kuna 'SAPRAIZI' inakuja Yanga, mjipange

Tue, 17 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya Yanga wikiendi iliyopita kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya CBE katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mastaa wa timu hiyo wameonekana kutoamini kilichotokea huku ikitajwa sapraizi kwenda kutokea pale Zanzibar.

Wakati mastaa wakiwa katika hali hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesisitiza kwamba walipaswa kumaliza kazi Ethiopia na wala hawana sababu ya kuficha.

Mchezo huo wa hatua ya kwanza uliochezwa Uwanja wa Abebe Bikila uliopo Addis Ababa nchini Ethiopia, umewapa Yanga matumaini makubwa ya kufuzu makundi kutokana na ushindi.

Matumaini hayo ya Yanga haimaanishi kwamba kazi itakuwa rahisi bali hata CBE wanaweza kufanya jambo kwani walionyesha hali hiyo katika mchezo uliopita nyumbani kwao.

CBE ambayo hii ni mara ya kwanza kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imekuwa ni timu inayocheza soka la kushambulia popote pale iwe nyumbani au ugenini.

Wahabeshi hao walifanya hivyo walipocheza dhidi ya SC Villa ya Uganda ambapo mchezo wa kwanza ugenini walikwenda na hesabu za kushambulia wakafanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1. Ushindi huo wa ugenini ulitokana na CBE kuanza kufunga mabao mawili dakika ya 20 na 55, ndipo wenyeji SC Villa wakapata moja dakika ya 69.

Waliporudiana nchini Ethiopia, CBE waliulinda ushindi wao kwa sare ya 1-1 ambapo pia walianza kufunga dakika ya 68, SC Villa wakasawazisha dakika ya 78 kwa penalti. Matokeo ya jumla CBE wakashinda 3-2 na kufuzu hatua ya kwanza ambapo tayari wamecheza na Yanga nyumbani kwao wakafungwa 1-0, bado marudiano.

Sasa katika mchezo huo uliochezwa wikiendi ambao Prince Dube alifunga bao pekee dakika ya 45+1, Yanga walikosa nafasi zaidi ya saba za wazi ambazo kama wangezitumia vizuri basi wangerudi wakiwa na mtaji mkubwa wa mabao ambao ungewasaidia kuifanya kazi rahisi watakaporudiana wikiendi hii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Ukimuweka kando Dube, pia Maxi Nzengeli, Clatous Chama, Clement Mzize na Stephane Aziz Ki nao walikosa nafasi kadhaa za kufunga ambazo zilionekana kuwa ni za wazi.

Kukosa huko nafasi kwa Yanga kunaweza kuwa ni faida kwa CBE ambao watapambana ili kuwafanyia sapraizi wenyeji wao watakaporudiana, lakini pia rekodi nzuri ya Yanga nyumbani dhidi ya Wahabeshi zinawabeba.

Yanga katika michuano ya CAF dhidi ya timu za Ethiopia, haijawahi kupoteza nyumbani mara tatu ilizocheza nazo huku mbili ikipata ushindi mnono zaidi.

Kwa mechi za nyumbani pekee dhidi ya Wahabeshi, mwaka 1969 Yanga iliichapa St. George mabao 5-0, kisha ikashusha dozi ya 6-1 dhidi ya Cofee, ikaifunga Welaita Dicha 2-0. Pia ikatoka sare ya 4-4 na Dedebit.

Rekodi hiyo nzuri ya mabao inaweza kuwabeba Yanga kuelekea mchezo wa Jumamosi lakini pia wachezaji wameapa kutumia vizuri nafasi kitu ambacho kinawapa jeuri ya kuwasapraizi CBE kwa kuiwashushia mvua ya mabao.

Aziz Ki ambaye alitoa pasi ya bao lililofungwa dakika ya 45+1 na Prince Dube, alisema lazima waongeze umakini mchezo wa marudiano ili kusahahihisha makosa.

“Muhimu ni kuja kucheza Tanzania iwe Zanzibar au Azam Complex Chamazi. Tuko nyumbani, kazi yetu ni kucheza na kuhakikisha tunashinda, hilo ndilo muhimu ingawa tunapaswa kuongeza umakini katika kutumia nafasi,” alisema Ki, akionyesha imani mashabiki wao watakuwa na nafasi ya kushuhudia ushindi mwingine.

Naye Maxi alisema mchezo wa nyumbani unawapa faida kubwa huku akiahidi timu itapambana kwa ajili ya mashabiki wao ambao wamekuwa wakiwaunga mkono kwa dhati.

“Bado mechi haijamalizika lakini kuwa kwetu nyumbani ni faida, tutapambana kwa ajili ya Wananchi. Kilichotokea mechi ya kwanza kimeshapita, tunaahidi makosa hayawezi kujirudia,” alisema Nzengeli kwa kujiamini.

Yanga, ambao msimu uliopita waliishia hatua ya robo fainali katika michuano hiyo, wanahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ili kujikatia tiketi kwa msimu wa pili mfululizo kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nahodha Msaidizi wa Yanga, Dickson Job, amesema kuwa wanayo nafasi ya kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza ili kuwa bora zaidi katika marudiano.

“Naamini tutaendeleza kile tulichokianza kwani tutakuwa na kila sababu ya kushinda mbele ya mashabiki wetu.”

Mchezo wa mkondo wa pili kati ya Yanga na CBE umepangwa kuchezwa Zanzibar ikiwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kucheza mchezo wa kimataifa wa hatua hii visiwani humo, jambo ambalo limeongeza hamasa kwa wachezaji na mashabiki.

Mashabiki wa Yanga wanaamini kuwa timu yao iko kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya makundi kwa mara nyingine tena.

Ushindi katika mchezo wa mkondo wa kwanza umewapa mashabiki hao matumaini ya kuona timu yao ikifanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa msimu huu.

Gamondi na wasaidizi wake wamekuwa wakitazama video za mchezo wa kwanza na kufanya tathmini ya maeneo yanayohitaji kuboreshwa huku kocha huyo akissema wazi kwamba walipaswa kumaliza kazi ugenini.

“Tulikuwa na nafasi ya kumaliza kazi yetu Ethiopia, lakini hatukuzitumia vizuri nafasi tulizozipata,” alisema Gamondi.

Maandalizi ya Yanga yanalenga kuhakikisha kuwa Yanga inajitokeza kwa nguvu zote na kucheza kwa kiwango cha juu katika dakika zote tisini.

Wakati huohuo, wapinzani wao CBE hawatakiwi kubezwa. Ingawa walifungwa nyumbani, bado wana kikosi chenye wachezaji wenye uzoefu na wanaoweza kuleta madhara kwa Yanga. Hii inamaanisha kuwa Yanga italazimika kucheza kwa umakini na kujiepusha na makosa yoyote ambayo yanaweza kuwapa nafasi wapinzani.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: