Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga ni miamba kwelikweli!

Yanga Oklll Yanga ni miamba kwelikweli!

Wed, 3 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya danadana nyingi hatimaye sasa mambo yanaelekea kufika mwisho baada ya wababe waliotinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kuwa hadharani.

Katika michuano hii mikubwa barani Afrika ilionekana kama kuna baadhi ya timu ambazo hazina rekodi kubwa kwenye michuano zinaweza kupenya kwenye hatua hiyo, lakini mambo yamekuwa tofauti baada ya maji na mafuta kujichuja.

Miamba minne ambayo imefuzu kwenye hatua ya nusu fainali ni wale wenye michuano yao yaani ambao wamekuwa wakifanya vizuri huko mara kwa mara, lakini pia ni timu ambazo zimewekeza mkwanja mkubwa kwenye vikosi vyao, wakiwa wanakwenda kutafuta bilioni 5.8 ambayo atapewa bingwa wa michuano ya mwaka huu.

Timu zilizokwenda kwenye hatua hiyo ni Al Ahly, Wydad Casablanca, Es Tunis pamoja na Mamelodi Sundowns ambayo inaonekana ndiyo timu ndogo kimafanikio kwenye michuano hiyo kuliko nyingine zote.

Wydad ndiyo timu pekee ambayo imeonekana kufuzu kwenye hatua hii kibahatibahati baada ya kulazimika kwenda kwenye mikwaju ya penalti na Simba baada ya matokeo ya jumla ya bao 1-1.

Al Ahly ambao wameshatwaa ubingwa huu mara 10 wameingia kwenye hatua ya nusu fainali mara sita mfululizo baada ya kuwachapa Raja Casablanca kwa mabao 2-0, nyumbani kwao na kwenda ugenini ikalazimisha suluhu.

Hii ni mara ya pili kwa Raja ambao wameshatwaa ubingwa huu mara tatu wanatolewa na Ahly baada ya kutupwa nje tena kwenye hatua hiyo msimu uliopita. Ahly sasa wanakwenda kukutana na Es Tunis ikiwa inatajwa kuwa ni nusu fainali ya Waarabu wenye rekodi zao kwenye michuano hiyo.

Faida kubwa kwa Ahly ambao wamekuwa bora sana nyumbani kwao ni kwamba wataanzia ugenini nchini Tunisia Mei 12 na kwenda kumalizia nyumbani Mei 19.

Es Tunis ambayo imetwaa ubingwa huu mara nne ikiwa ilitwaa mara ya mwisho 2019 ikiwachapa Wydad, ilifuzu bila jasho kubwa baada ya kukutana na JS Kablie ambapo walishinda bao 1-0 ugenini na kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani kwao.

Timu zote hizi zimeonekana kuwa na vita kubwa zinapokutana kwenye hatua muhimu kama hii na ndizo zinazoongoza kwa kutwaa ubingwa huu kwa zile zilizobaki.

Kumbukumbu inaonyesha kuwa Es Tunis walikutana na Al Ahly kwenye fainali ya mwaka 2012 na kulala kwa jumla ya mabao 3-2 na sasa watakuwa na wakati wa kutaka kulipiza kisasa kwenye mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka la Afrika.

Hata hivyo, Tunis watakuwa na kazi kubwa ya kuwakaba Al Maaloul ambaye ndiye kinara wa kupiga pasi za mwisho kwenye michuano hii hadi sasa akiwa amepiga pasi tano huku Percy Tau akitoa asisti nne.

Mamelodi ambayo mara ya kwanza kuonja ubingwa huu ilikuwa mwaka 2016 ilipowachapa Zamalek kwenye mchezo wa fainali.

Tangu hapo hawajaonekana kuamka tena hadi msimu uliopita na msimu huu ambao wamefanya vizuri kwenye michuano hiyo mikubwa.

Tangu msimu huu umeanza, Mamelodi wameonekana kuwa mahiri kwenye michuano hii ikiwa timu ya mwanzo kabisa kufuzu kwenda robo fainali.

Faida kubwa kwao kwa sasa ni kwamba wanaanzia ugenini Morocco, Mei 12 na watarejea kwenye uwanja wao wa nyumbani Mei 19 sehemu ambayo wamekuwa wakifanya vizuri kwenye michuano hii.

Katika hatua hii macho ya mchezo huu yatakuwa kwa vinara wa mabao, Mamelodi kinara wao ni Peter Shilalule ambaye ana mabao matano, lakini atakuwa na vita na Bouly Sambou ambaye ameshapachika mabao manne hadi sasa.

KOMBE LA SHIRIKISHO Baada ya timu kumaliza harakati zake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hatimaye kwenye Kombe la Shirikisho napo kulikamilisha timu nne zilizotinga nusu fainali juzi usiku.

Huku kulikuwa na mabadiliko makubwa baada ya timu nyingine ambazo zilikuwa hazipewi nafasi kubwa ya kufuzu kwa hatua hii kupenya.

Yanga pamoja na Marumo Gallattis mwanzoni mwa michuano hii zilikuwa hazipewi nafasi ya kufika nusu fainali kutokana na uchanga wao kwenye michuano ya Kombe la Shrikisho Afrika.

Yanga ilifuzu baada ya kuwatupa nje Rivers United kwa jumla ya mabao 2-0, baada ya kushinda ugenini nchini Nigeria na kutoka suluhu nyumbani. Hii ni mara kwanza Yanga wanafika kwenye hatua hii lakini watakutana na timu ambayo nayo ni mara yao ya kwanza kufika hapa ikiwa changa zaidi.

Marumo haifanyi vizuri kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini ikiwa katika nafasi ya 14 kwenye ligi kwa sasa wakiwa na pointi 28 baada ya michezo yao mitano ya mwisho wamefanikiwa kushinda michezo miwili tu wametoka sare michezo mitatu.

Hii inakuwa nafasi ya kocha wa zamani wa Simba, Dylain Kerr kutua tena hapa nchini kwani ndiye kocha mkuu wa timu hiyo ya Afrika Kusini.

Timu hii ni changa zaidi kwenye michuano yote kwani imeanza kushiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini hivi karibuni, walianza kucheza msimu uliopita ambapo walimaliza katika nafasi ya 10.

Kuingia kwao kwenye Kombe la Shrikisho kulitokana na wao kufika fainali ya Kombe la Nedbank ambapo walichapwa kwenye fainali na Mamemodi Sundowns.

Rekodi zao na Yanga kama zinafanana Yanga hawajapoteza nyumbani kwenye Kombe la Shirikisho, lakini mastaa hawa hawajapoteza kwao wakiwa wameshinda michezo minane nyumbani na kutoka sare mmoja.

Mchezo wa kwanza wa timu hizo utapigwa Mei 10 kwenye Uwanja wa Mkapa na kumaliza wa pili nchini Afrika Kusini Mei 17, mashabiki watakuwa na nafasi ya kuwatazama washambuliaji wawili hatari kwenye mechi hii, Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao matano ambaye analingana na Ranga Chivaviro wa Marumo ambaye naye yupo kileleni na mabao matano.

Mechi nyingine ya Shrikisho itawahusisha Asec Mimosas ambao watavaana na USM Algier ya Algeria ambao walifuzu baada ya kuwatupa nje FAR Rabat kwa mabao 4-3.

Asec ambao wana historia ya wastani kwenye michuano hii wanakwenda wakiwa wanamtengemea mshambuliaji wao Aubin Kramo Kouamé ambaye ana mabao manne kwenye michuano ya mwaka huu.

Lakini kwa upande wa Algier wao watamtegemea sana Zineddine Belaïd ambaye ameshapachika mabao matatu hadi sasa.

FAR Rabat wanaingia kwenye hatua hii wakiwa ni wababe zaidi kwa timu zilizobaki kwa kuwa ndiyo pekee ambao wameshatwaa ubingwa huu mara moja mwaka 2005 na kufika fainali mwaka 2006 huku timu nyingine zote zikiwa hazina makombe na hivyo ni nafasi ya yeyote kutikisa msimu huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: