Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga SC yaisubiri Simba kumtangaza Chama

Realclatouschama Yanga SC yaisubiri Simba kumtangaza Chama

Tue, 25 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Yanga inatarajia kuingia rasmi mkataba na kiungo mshambuliaji Clatous Chama Juni 30, mwaka huu na kutangazwa Julai Mosi, sababu kubwa ikielezwa kuisubiri Simba.

Pamoja na Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, kudai kuwa mchezaji huyo amemaliza mkataba, lakini taarifa zinaeleza kuwa unamalizika Juni 30, mwaka huu na ndipo atakuwa kwenye wakati mzuri wa kusaini Klabu ya Yanga kama walivyokubaliana.

"Kelele zote hizi bado Chama hajasaini mkataba na Yanga, ila makubaliano kati ya pande zote mbili yalifikiwa tangu Januari mwaka huu, mkataba unatarajiwa kusainiwa Juni 30, na inawezekana atatangazwa kuanzia Julai Mosi, katika Klabu ya Yanga, atakuwa ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi ukiondoa Stephane Aziz Ki," kilisema chanzo kutoka ndani ya Klabu ya Yanga.

Chanzo hicho kimesema Yanga imeshindwa kumsainisha mkataba rasmi na kumtangaza mapema kwa hofu kuwa tarehe ya kumalizika kwa mkataba na klabu yake haijamalizika, na hawataki kuingia matatizoni.

"Kama Simba wangekuwa wamempa barua ya kuagana naye sawa, lakini kwa sababu hawajampa, hawawezi kufanya hivyo," alisema mtoa taarifa wetu.

Maneno haya yanafanana na aliyosema, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, akidai wanachelewa kutangaza walioachwa na watakaosajili kuwa kutokana na baadhi ya klabu kuchelewa kuwapa barua ya kuachana na wachezaji wao kwa hofu ya kuhamia kwao.

"Kuna mchezaji mmoja anamaliza mkataba, lakini jamaa hawataki kumpa barua, wana hofu atakuja kwetu, wampe tu kijana wa watu ili aje kwenye klabu ya ndoto yake, na hilo ndilo limetufanya mpaka sasa tuahirishe au tuchelewe kuwapa 'thank you' tutakaoachana nao na kutangaza wachezaji ambao tumewasajili, lakini tutaanza kufanya hivyo Julai Mosi," alisema Kamwe siku chache zilizopita bila kutaja jina la mchezaji.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed, alisema mkataba wa Chama na Simba umemalizika.

"Niseme tu kuwa Chama amemaliza mkataba wake ndani ya Simba, hivyo ndivyo ninavyofahamu, sasa anaongeza, haongezi, tuwape nafasi viongozi wetu wanaoshughulika nalo, wakishakuwa kwenye nafasi nzuri watatuambia nini kimetokea, watanieleza niwaambie kitu gani kinaendelea.

"Chochote kitakachofanyika ni kwa maslahi ya Simba, maamuzi yatakayoamuliwa yatakuwa kwa maslahi ya klabu, hapa tunachoangalia ni namna gani timu inaweza kusonga mbele, tukiamua abaki, aondoke itakuwa ni kwa maslahi ya klabu. Wanachama na mashabiki wa Simba subirini, msiwe na mashaka tutafahamu mbivu na mbichi," alisema.

Jana kwenye mtandao wake wa instagram, amewaambia wanachama na mashabiki wa Simba kuwa ili nyumba ijengwe ni lazima kwanza ibomolewe. "Msishtuke kuona nyumba yenu inabomolewa ili ijengwe mpya, imara na nzuri zaidi," aliandika Ahmed.

Taarifa zingine zilizopatikana kutoka vyanzo ndani ya Klabu ya Simba zinasema bado viongozi wa klabu hiyo wanahaha kumbakisha na wanaendelea na mazungumzo kwa siku hizi zilizobaki na yamefikia mahala pazuri.

"Hao wataendelea kumsajili kama ambavyo tumezoea. Ahmed anaongea taarifa rasmi ambazo mpaka apewe na viongozi na bado hajazipata, ila Chama ataendelea kuvaa jezi za Simba, watangoja 'thank you ' ya Chama watasubiri sana," alisema mtoa taarifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: