Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watajuta kuja kwa Mkapa

Yanga Msad.jpeg Kikosi cha Yanga

Sun, 28 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Leo Jumapili nchi itasimama kwa dakika 90 ili kufuatilia pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika linalozikutamisha Yanga ya Tanzania na USM Alger ya Algeria.

Hii ni mechi ya kwanza ya fainali ya CAF kupigwa nchini tangu Simba ilipofanya hivyo miaka 30 ilipotinga hatua hiyo kwenye Kombe la CAF (kwa sasa halipo kwani liliunganishwa na Kombe la Washindi na kuzaliwa michuano ya sasa ya Shirikisho Afrika kuanzia mwaka 2004).

Macho, akili na masikio ya Afrika nzima leo hii yameelekezwa kwenye Uwanja Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kuanza saa 10:00 jioni ili kushuhudia Yanga itakayokuwa wenyeji wa USM Alger katika mchezo huo wa kwanza wa fainali hiyo kabla yua kurudiana nao wiki ijayo jijini Algers.

Hakuna kingine kingine ambacho Yanga inakihitaji zaidi ya ushindi mnono nyumbani kabla ya kwenda ugenini ili kujiandikia historia tofauti, huku rekodi zikiibeba msimu huu katika michuano hiyo ikicheza Kwa Mkapa, lakini hata ikicheza mechi za ugenini.

Takwimu bora za Yanga na wachezaji wake mmojammoja katika michezo iliyopita ya michuano hayo kuanzia ile ya makundi hadi ya nusu fainali, ni kitu kinachotoa matumaini makubwa kwamba timu hiyo itapeperusha vyema bendera ya nchi leo na kupata ushindi ili kuiweka pazuri kubeba taji.

Yanga inashika nafasi ya pili kwa kucheza mechi nyingi bila kuruhusu bao ikifanya hivyo mara sita, ipo pia katika nafasi hiyo kwa kutengeneza nafasi nyingi ambazo ni 22, lakini inashika nafasi ya sita kwa kupiga pasi sahihi ikiwa na wastani wa pasi 320.5 kwa mechi.

Licha ya takwimu hizo bora, Kocha Nasreddine Nabi amewatahadharisha wachezaji kwa kuwataka wanacheza kwa nidhamu kubwa kimbinu dhidi ya USM Alger ili waandike historia, lakini akisisitiza atawapangia busta nzima kwenye mechi hiyo ili kuwa na kazi rahisi ugenini.

"Nimewasisitiza wachezaji wangu kuhakikisha wanacheza kwa umakini mkubwa katika mechi hii. Tunapaswa kumalizia vizuri kazi tuliyoianza. Malengo yetu ni kutwaa ubingwa wa michuano hii na kila mmoja wetu analifahamu hilo," alisema Nabi aliyebeba pia taji la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo kabla hata ligi hiyo haijamaliza, huku akiwa na Ngao ya Jamii aliyoitetea pia mapema.

MKWANJA NJE NJE

Yanga ikifanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, itavuna kiasi cha Dola 2 Milioni (Sh4.7 bilioni) ambacho kinatolewa na CAF kwa timu inayokuwa bingwa wa Kombe la Shirikisho ambayo ni ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika baada ya Ligi ya Mabingwa.

Awali kiasi cha fedha kilichokuwa kikitolewa kwa bingwa wa michuano hiyo kilikuwa ni Dola 1.25 milioni (Sh2.9 bilioni) lakini mwaka jana, Rais wa CAF, Patrice Motsepe alitangaza kuongeza fedha za zawadi kwa washindi wa mashindano mbalimbali yaliyo chini ya shirikisho hilo.

Kama Yanga ikishindwa kuibuka Bingwa, haitotoka patupu kwani itapata kiasi cha Dola 1 milioni (Sh2.3 bilioni).

Mbali na fedha hizo za CAF, Yanga itashuka uwanjani ikiwa na mzuka wa Sh 20 Milioni kwa kila bao itakalofunga kwenye mchezo huo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye pia alinunua tiketi 5000 ili kuhamasisha mashabiki kujitokeza kwa wingi kesho Kwa Mkapa.

Ahadi hiyo ya Sh 20 Milioni ya Rais ilitolewa kwenye hatua ya nusu fainali baada ya awali kwenye makundi kutoa Sh 5 Milioni kwa kila bao kabla ya kuongeza dau na kwenye mechi za nusu Yanga ilivuna Sh 80 Milioni kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 dhidi ya Marumo.

AUCHO ASHTUA

Yanga katika mchezo huo itamkosa kiungo wake tegemeo, Khalid Aucho ambaye anatumikia adhabu ya kukosa michezo miwili kutokana na kukusanya kadi tano za njano kwa makosa yanayojirudia.

Aucho amekuwa mhimili wa Yanga kwenye safu ya kiungo na kuthibitisha hilo, amecheza mechi 11 kati ya 12 za Yanga kwenye mashindano hayo kwa dakika 760.

Hata hivyo, nyota huyo wa Yanga amewataka mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi na kukosekana kwake na amewaomba waisapoti vilivyo timu.

"Kwa mashabiki wote wa Yanga, tujitokeze wote kwa wingi Jumapili kusapoti vijana wetu kwa sababu tunaweza kutimiza kama tutapata sapoti yenu ya kutosha," alisema Aucho.

MECHI YA WAZI

Ni mchezo unaozikutanisha timu mbili ambazo zimekuwa zikihusudu kucheza soka la kushambulia kwa muda mwingi wa mechi jambo ambalo limezifanya ziwe zinatengeneza nafasi nyingi za mabao na hata kufunga idadi kubwa ya mabao.

Yanga katika mashindano hayo imekuwa ni mwiba katika kushambulia kwa haraka pindi inapopokonya mpira kutoka kwa timu pinzani ambapo huwa inapiga pasi chache kuelekea langoni mwa adui na wachezaji wake kukimbia kwa kasi kubwa ili kuvunja mistari ya ulinzi ya timu pinzani.

Katika aina hii ya mashambulizi, Yanga imekuwa ikiwategemea zaidi washambuliaji wake, Fiston Mayele, Tuisila Kisinda, Kennedy Musonda na Bernard Morrison ambao kasi na uwezo wao wa kushambulia nafasi umekuwa mwiba kwa timu pinzani.

USM Alger sio timu ambayo imekuwa ikipenda kumiliki sana mpira na mara nyingi imekuwa ikitumia mipira mirefu katika ujenzi wa mashambulizi, ikiwatumia zaidi wachezaji wake wanaoshambulia kutokea pembeni, kutengeneza nafasi na kufunga mabao.

Kuthibitisha hilo, kuanzia hatua ya makundi hadi sasa, USM Alger inashika nafasi ya pili kutoka mwisho katika chati ya timu zilizopiga pasi nyingi sahihi ambapo ina wastani wa pasi 261.5 tu kwa mechi.

WENYE MECHI YAO

Bila ya shaka Fiston Mayele ndiye mchezaji atakayechungwa zaidi na USM Alger katika mechi hiyo kutokana na uwezo mkubwa wa kufunga mabao, kutengeneza nafasi, pia hata kasi na umiliki wake wa mpira ambao umekuwa ukiwapa tabu walinzi wa timu pinzani.

Straika huyo ndiye kinara wa mabao wa michuano hiyo akiwa amepachika mabao sita, sawa na Ranga Chivaviro wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini iliyong'olewa na Yanga kwenye nusu fainali, huku akiwa na asisti tatu zinazomuweka juu akiwa amehusika na mabao tisa ya timu hiyo hadi sasa.

Saad Redouani wa USM Alger anapaswa kupewa jicho la ziada na nyota wa Yanga, kwani ndiye tegemeo la timu hiyo kwenye michuano hiyo kwa uwezo mkubwa wa kufunga kwa mashuti ya mbali, kupiga pasi za mwisho na kutoa pasi sahihi hasa zile zinazoelekea mbele.

Beki huyo wa kulia mwenye umri wa miaka 28 amehusika na mabao matano ya USM Alger, akifunga mawili na kupiga pasi tatu za mwisho.

REFA HUYU HAPA

Jean-Jacques Ndala Ngambo kutoka DR Congo ndiye refa aliyepangwa kuchezesha mechi hiyo akisaidiwa na Zakhele Siwela wa Afrika Kusini na Olivier Kabene (DR Congo) huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Ahmad Heeralall kutoka Mauritius.

Refa Ngambo amekuwa na bahati na klabu za Tanzania kwani katika mara tatu tofauti alizozichezesha kwenye mashindano ya klabu Afrika, ziliibuka na ushindi mara na kupoteza moja.

USM ALGER UBARIDI

Kikosi cha USM Alger kimetua nchini juzi kimya kimya, huku mabosi wao wakificha makucha kwa kile kinachodhania ni presha kubwa ya kukutana na Yanga Kwa Mkapa huku ikiwa ya moto tofauti na ile ya mwaka 2018 ilipokutana kwenye makundi na kupasuka 2-1, baada ya awali kushinda kwao 4-0.

Wanafainali hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2015 iliponyooshwa na TP Mazembe, wamekaririwa wakisema wanakutana na timu ngumu kwenye fainali, lakini wakatomaa.

“Tuna furaha na kujivua kwa kupata nafasi hii ya fainali. Haitakuwa kazi rahisi kwani mpinzani wetu ni wazuri," alisema kocha mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha na kuongeza;

“Tulishaanza mapema kuisoma Yanga. Ni timu nzuri, lakini tunajiandaa kwa lengo la kushinda kwa niaba ya Waalgeria wote."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: