Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washambuliaji walivyokaukiwa mabao

Saido X Mayele TFF Wafungaji Bora NBC Ligi 2022/23

Sat, 24 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Fiston Mayele (Yanga) na Saidi Ntibazonkiza (Simba) wamemaliza Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa vinara wa mabao wote wakicheka na nyavu mara 17 na kugawana tuzo ya ufungaji bora.

Katika harakati za ufungaji bora, washambuliaji wengi walianza msimu vyema hasa wazawa, ambao kwa misimu miwili walitamba kwa kuchukua kiatu cha ufungaji bora, George Mpole (Geita) msimu uliopita na John Bocco (Simba) msimu wa 2020/21.

Hata hivyo, mwisho wa msimu walionekena kukata pumzi licha ya kufanya vyema msimu uliopita, Reliants Lusajo mfungaji bora wa muda wote kwenye kikosi cha Namungo amemaliza msimu na mabao nane.

Upepo umemgeka nyota huyo kwani Namungo ilicheza michezo 15 bila mshambuliaji huyo kucheka na nyavu na mara ya mwisho alifunga Novemba 4, walipolala kwa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City, baada ya hapo akafunga Februari 2 walipochapwa 3-2 na Prisons.

Middie Kagere (Singida) mfungaji bora mara mbili msimu wa 2018/19 kwa mabao 23 na 2019/20 akifunga mara 22, amemaliza msimu akiwa na mabao nane

Bao lake la mwisho alifunga kwa mkwaju wa penalti, wakati Singida ikiichapa Ruvu Shooting 2-1, Juni 6, na kabla ya hapo alikuwa amefunga Februari 2, wakati wakiichapa Geita 2-1.

Habib Kyombo (Simba) mwenye mabao mawili kwenye ligi mara ya mwisho alifunga Oktoba 2, wakati Simba ikiichapa Dodoma Jiji mabao 3-0 na hapo ndipo ulikuwa mwisho wake.

Danny Lyanga (Geita) msimu uliopita alimaliza ligi na mabao sita, hadi msimu huu unamalizika alikuwa amefunga mawili, kitu ambacho kilizidi kuwaumiza vichwa makocha hasa katika safu ya ushambuliaji. Mara ya mwisho alifunga Desemba 25 katika sare ya 2-2 dhidi ya Kagera.

Matheo Antony (KMC), ambaye msimu uliopita alimaliza ligi na mabao tisa lakini msimu huu amemaliza na mabao manne na mara ya mwisho alifunga Septemba 20.

Tariq Seif wa Mbeya City, ambaye timu yake inapambana kutoshuka daraja kwa kucheza hatua ya mtoano dhidi ya Mashujaa amemaliza msimu na mabao matano kama ilivyo kwa mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Charles Ilanfya.

John Tamba kocha wa Polisi Tanzania alisema kuna wakati mshambuliaji amaweza akaathirika na mfumo wa kocha hasa kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara yanayofanywa katika benchi la ufundi.

Mohamed Abdalah 'Bares' kocha wa Prisons alisema kujituma kwa mchezaji ndio mafanikio yake lakini muda mwingine anapopata majeraha akirudi uwanjani wachache wanaendelea na kasi yao.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: