Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanasubiriwa kwa hamu Jangwani

Mastaa Wapya Yanga Skudu X Pacome Wanasubiriwa kwa hamu Jangwani

Sat, 22 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Leo ndio leo. Yanga wanawasha mitambo kwenye siku yao. Mambo yote yatakuwa hadharani kwenye Uwanja wa Mkapa wakikiwasha na Kaizer Chiefs inayojipanga upya kwa msimu mpya.

Hata kama ulimisi zile mashine mpya zilizotambulishwa usiku, leo zitakuwa hadharani kuanzia saa 10 jioni halafu saa 1 usiku watakiwasha kwenye nyasi.

Mategemeo ya mashabiki wa Yanga kuona ufundi wa sura mpya zilizoingia kikosini ambazo wamekuwa wakizisikia tu na kuziona kwenye mitandao ya kijamii.

Ni nafasi kwa mashabiki kuwaona kwa mara ya kwanza ndani ya uwanja wakiwa kwenye jezi za timu yao, wachezaji saba walionaswa na timu hiyo katika dirisha linaloendelea la usajili ambao ni Gift Fred, Yao Atohoura, Maxi Nzengeli, Jonas Mkude, Nickson Kibabage, Scudu Makudubela na Pacome Zouzoua.

Uwepo wa nyota hao hapana shaka unaweza kuifanya Yanga iwe na muonekano wa kitofauti leo tofauti na ule ambao mashabiki waliuzoea msimu uliopita. Inaweza kuwa Yanga ya kasi sana haswa kupitia pembeni.

Kule upande wa beki wa kulia kuna sura mpya. Yupo Atohoura aliyetoka Asec Mimosas atatumika akibebwa na uwezo wake mkubwa wa kupandisha mashambulizi na kuilinda timu. Pale kati sasa. Nafasi ya viungo wawili wa kati wanaocheza mbele ya mstari wa mabeki,kuna sura mbili ngumu hazitakuwepo. Yannick Bangala mmoja wapo. Gamondi ataingiza mtu wa kazi kucheza na Aucho ambaye anaweza kuwa Jonas Mkude, Sure Boy, Mudathir Yahaya ama Zawadi Mauya.

Kuna mtu anaitwa Zouzoua (Zuzwaa) anampa Gamondi uhakika wa kutumia mfumo anaoupendelea wa 4-2-3-1 ambapo kiungo huyo mtaalam wa kupiga pasi za mwisho anaweza kucheza nyuma ya mshambuliaji, nafasi ambayo mara kwa mara msimu uliopita alikuwa akipangwa Stephane Aziz Ki.

Achana na makali ya Kaizer lakini ni mechi ambayo inaweza kuwapa ladha ya mpira wa kuvutia kwani kocha Gamondi ni muumini wa timu yake kucheza soka la pasi na kuruhusu wachezaji kuonyesha ujuzi wao, tofauti na Nabi ambaye amekuwa akipendelea zaidi wachezjai wake kujikita katika mbinu zaidi.

Yanga inaonekana itatumia zaidi wachezaji wake wa nafasi za pembeni katika kujenga mashambulizi na nafasi za mabao, huku wale wa katikati wakiwa na jukumu kubwa la kutawanya mipira kwenda katika pande tofauti za uwanja.

Ukiachia mbali wachezaji, leo kwa mara ya kwanza pia wataanza maisha na Kocha wao mpya, Miguel Gamondi na benchi lake la ufundi. Walishazoea matokeo makubwa kwenye mabadiliko ya jioni ya Kocha aliyepita, leo wataanza kujifunza kuzoea maisha mapya.

Tofauti na Nabi ambaye huwa sio mzungumzaji wa mara kwa mara pindi anapokuwa analiongoza benchi la ufundi lakini pia amekuwa na utulivu wa hali ya juu, Gamondi ni aina ya mwalimu ambaye amekuwa akipendelea kuwakumbusha wachezaji wake mara kwa mara na amekuwa akizunguka mara kwa mara kuhakikisha anakifikisha kwa wakati na kinafanyiwa kazi kile ambacho anawaelekeza wachezaji wake. Ni leo hapo Kwa Mkapa.

Ukiondoa Gamondi, Yanga itakuwa na sura mpya nyingine kwenye benchi lake la ufundi ambayo ni kocha msaidizi, Moussa Ndaw kutoka Senegal lakini pia mashabiki kwa mara ya kwanza watamshuhudia mtaalam wa mazoezi ya viungo, Taibi Lagrouni.

WOTE WATACHEZA LEO

Gamondi ametoa uhakika kwamba kila staa wa timu hiyo aliyesawa kiafya atacheza mechi hiyo labda asiwepo nchini akisema anataka kuona kila mchezaji anapata muda wa kuonyesha kipaji chake.

Gamondi raia wa Afrika Kusini akafichua kuwa katika maamuzi yake hayo anataka kuona kila mchezaji anacheza kwa uhuru kumuonyesha uwezo wake ili amjue kipi alichonacho kabla ya kuingia kambini rasmi kwa maandalizi siriazi zaidi ya kuanza kutengeneza timu.

Tayari mastaa wapya wa timu hiyo wameshaanza kujaribiwa kuanzia mazoezini kila mmoja kucheza nafasi yake halisi anayotaka ili awe huru kuonyesha ubora wake mbele ya mashabiki wao.

"Hii ni siku ya furaha kwa mashabiki wetu, kucheza dhidi ya Kaizer haina maana tunatakiwa kujua nani mshindi, hii ni mechi ya kuwafurahisha mashabiki wetu, nimewaambia wachezaji wajiandae kila mmoja kucheza.

"Nataka kuona kila mchezaji anapata muda wa kunionyesha kile kipaji alichonacho, lakini pia ni nafasi kwa mashabiki wetu kuona ubora wa wachezaji wao kuna hawa wapya na wale ambao walikuwepo, tukimaliza tukio hili ndio tutaingia kambini rasmi kujiandaa na msimu mpya kwa ukamilifu."

AUCHO, DIARRA, KI NDANI

Stephanie Aziz KI na Djigui Diarra waliwasili nchini alfajiri Alhamisi kisha jioni yake wakajiunga na kambi ya timu hiyo sambamba na kiungo Khalid Aucho.

Wachezaji hao waliingia kambini sambamba na kiungo mpya wa timu hiyo, Pacome Zouzoua ambaye ametua klabu hiyo akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

MECHI YA UFUNGUZI NA BURUDANI

Mchezo wa kwanza wa soka kwenye tamasha hilo utakuwa kati ya Yanga Princess watakaopambana na Geita Gold Queens.

Mchezo wa pili utawakutanisha mabosi wa Yanga nao wataingia uwanjani wakiwa na mchezo wa marudiano dhidi ya wapinzani wao Bongo Fleva ambao tamasha lilopita walipokea kipigo.

Kuanzia asubuhi hiyo ya saa 4:00 burudani za muziki zitakuwa zinapishana ndani ya uwanja huo ambapo jumla ya wasanii 17 watalishambulia jukwaa kuwaburudisha mashabiki uwanjani.

Wasanii ambao watafanya shoo ni pamoja na Chobis Twins, Kassim Mganga,Linex, Sir Jay,Madee, Bilnass,Mzee wa Bwaxx,Christian Bella, G-Nako,Mavokali,Sholo Mwamba, Dulla Makabila, Fid Q,Chino Wana Man.

Wengine ni Marioo, Rayvanny, Jux huku kabla ya mchezo huo kama kawaida Yanga wanaweza kufanya shoo yao ya kupiga mafataki hewani ambayo hunogesha matamasha yao. Sherehe hizo kama kawaida zitaendelea kuwakutanisha washereheshaji watatu Dacota De la vida, Maulid Kitenge na Babu Zembwela huku kwa mara ya kwanza msimu huu DJ atakuwa Ally B. Tukutane Kwa Mkapa. Usilale ndani.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: