Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vitasa vya msimu ndo hivi hapa bana

IMG 4175.jpeg Vitasa vya msimu ndo hivi hapa bana

Sun, 28 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sir Alex Ferguson alisema, washambuliaji wanashinda mechi - mabeki wanakupa mataji. Gwiji kasema. Haina mjadala. Utahitaji washambuliaji wafunge mabao mengi kuliko mpinzani ili kushinda mechi. Lakini, utahitaji mabeki wako walinde mabao hayo yaliyofungwa yasirudi ili kukusanya pointi ambazo mwishoni zitaleta ubingwa.

Waulize Arsenal wanafahamu kilichowakuta msimu huu baada ya beki wao William Saliba kuwa majeruhi. Washambuliaji wao walikuwa wanafunga mabao, lakini mabeki wakawa hawawezi kulinda na matokeo yake wamepoteza fursa ya kuwa mabingwa.

Ndiyo hivyo. Kukaba kwenye soka kunaweza kuwa ni sanaa ya daraja la juu sana, licha ya kwamba imekuwa haipewi kipaumbele na mashabiki.

Lakini, katika soka la kisasa, mabeki wanapewa thamani kubwa inayostahili kutokana na umuhimu wao na ndio maana zimekuwa zikilipwa pesa nyingi sana kunasa huduma zao, pengine kuzidi hata wachezaji wa safu ya ushambuliaji.

Kwenye Ligi Kuu England, Newcastle United na Manchester City kwa msimu huu zimekuwa na safu imara sana ya mabeki na matunda ya hilo yameonekana. Timu moja imebeba ubingwa na nyingine imekata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Hata hivyo, kwenye Ligi Kuu England msimu huu kumejitokeza mabeki mmoja mmoja waliokuwa kwenye viwango bora kabisa vinavyostahili sifa.

10. Tyrone Mings (Aston Villa)

Tangu kocha Unai Emery alipochukua mikoba ya kuinoa Aston Villa, beki Tyrone Mings ameunda ukuta mfumu sana na mwenzake Ezri Konsa. Mavitu makini ya Mings ndani ya uwanja yaliifanya Aston Villa kucheza mechi nane bila ya kuruhusu bao katika 18 za mwisho. Mings alikuwa hatari pia aliposogelea goli la timu pinzani kwa maana amekuwa tishio kwenye kufunga na kuasisti. Ni mzuri pia kwenye mipira ya juu.

9. Lewis Dunk (Brighton)

Ameitwa kwenye kikosi cha England. Lewis Dunk ni bonge la beki na kazi yake matata uwanjani ndiyo iliyofanya Brighton kuwa timu ngumu kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Dunk ndiye mchezaji aliyepiga pasi nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England msimu huu, 3,202. Amewafunika mastaa kibao kwa pasi akiwamo Rodri na Virgil van Djik. Dunk ni tishio pia akipanda mbele kushambulia mipira ya adhabu.

8. Trent Alexander-Arnold (Liverpool)

Hakuwa kwenye kiwango chake bora sana msimu huu, lakini kile ambacho alifanya Trent Alexander-Arnold tangu kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia ni balaa kubwa uwanjani. Beki huyo aliirudisha Liverpool kwenye ndoto za kufukuzia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku akichagiza ushindi wa Liverpool katika mechi saba mfululizo. Ameasisti mara nane.

7. Pervis Estupinan (Brighton)

Beki mwingine wa Brighton aliyepenya kwenye orodha hii ni Pervis Estupinan ambaye amefurahia msimu wake wa kwanza kwa kucheza kwenye ubora mkubwa sana akitokea Villarreal. Estupinan amekuwa mchezaji muhimu katika mafanikio ya Brighton msimu huu akitamba kutokea kwenye beki ya kushoto, ambapo amekuwa akishambulia kama winga vile. Muda wote yupo kwenye boksi la timu pinzania wakati yeye ni beki.

6. Ruben Dias (Man City)

Pep Guardiola amekuwa akifanya vizuri sana katika kuwabadilishabadilisha wachezaji wake ili kuhakikisha wote wanakuwa bora kutimiza malengo yao ya kubeba mataji matatu msimu huu. Wapo vizuri katika kuelekea kutimiza hilo na moja ya sababu kubwa ni kuwapo kwa huduma ya beki makini kama Ruben Dias. Dias amecheza mechi 26 za Ligi Kuu England msimu huu na akiwa sambamba na John Stones wagumu sana kupitika.

5. Lisandro Martinez (Man United)

Wakati Lisandro Martinez alipowasili Manchester United akitokea Ajax majira ya kiangazi mwaka jana, mashabiki wengi sana walitia shaka.Hata Jamie Carragher alidai kwamba kimo cha beki huyo hataweza kucheza kwenye Ligi Kuu England kwenye washambuliaji wengi warefu. Lakini, Martinez amewanyamazisha watu kutokana na mzigo aliopiga kwenye ligi sambamba na pacha wake wa uwanjani Raphael Varane.

4. Sven Botman (Newcastle)

Newcastle United ndiyo timu iliyoduwaza wengi kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Msimu uliopita walimaliza nafasi ya 11 kwenye ligi, lakini msimu huu wamekamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa maana ya kuwamo ndani ya Top Four. Moja ya sababu kubwa ni kuwapo kwa huduma ya beki katili Sven Botman, ambaye alijiunga na timu hiyo akitokea Lille. Botman amekuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.

3. Luke Shaw (Man United)

Baada ya kuwekwa benchi na nafasi yake kuchukua Tyrell Malacia mwanzoni mwa msimu, Luke Shaw alimeza mate ya akili na kumwonyesha kocha Erik ten Hag kwamba yeye si mtu wa kukaa benchi kutokana na kile alichofanya ndani ya uwanja. Shaw amekuwa chaguo bora la beki kwa kocha Ten Hag hadi kufikia hatua ya kumtumia kama beki wa kati wakati Varane na Martinez walipokosekana. Amekuwa kwenye ubora mkubwa.

2. William Saliba (Arsenal)

Maisha ya Arsenal yalikuwa mazuri sana hadi hapo William Saliba alipoumia. Wakati beki huyo Mfaransa alipokuwa akicheza, Arsenal ilikuwa na jeuri ya kupiga soga za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England. Lakini, baada ya kuumia kwake tu, kila kitu kilitibuka huko Emirates na Arsenal ikapoteza uongozi wake wa pointi kibao na kupitwa na Manchester City kwenye mbio za ubingwa, sasa wakiambilia nafasi ya pili.

1. Kieran Trippier (Newcastle)

Kieran Trippier haina mjadala amekuwa beki bora zaidi kwenye Ligi Kuu England msiku huu na ndio maana hata jina lake limejumuishwa kwenye orodha ya wachezaji wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu kwenye ligi hiyo. Trippier alikuwa vizuri kwenye kukaba na kushambulia akitokea kwenye beki ya kulia, ambapo kwa msimu huu amefunga bao moja na kuasisti mara saba. Huduma bora kabisa kwa beki.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: