Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usajili Simba usitengeneze ubaunsa

Image 162.png Usajili Simba usitengeneze ubaunsa

Thu, 13 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Umeshawahi kuwaona watu wanaoitwa mabaunsa? Wengi wao wana sifa moja kubwa ambayo ni kutanuka zaidi kuanzia kiunoni kwenda juu kwenye miili yao lakini chini wanakuwa wembamba.

Yaani ukubwa wa miili yao juu huwa sio sawa na chini na kufanya maumbile yao yasiwe na muonekana mzuri au balansi sahihi.

Natazama mchakato wa usajili unaoendelea katika timu ya Simba, unaanza kunipa wasiwasi kuwa unaweza kuifanya timu hiyo ikawa kama mwili wa baunsa msimu ujao. Kwa nini?

Kwa sababu inaonekana kuweka nguvu na msukumo mkubwa katika usajili wa wachezaji wanaocheza katika nafasi za ushambuliaji huku wale wa nafasi ya kiungo na ulinzi wakiwa sio kipaumbele kikubwa.

Hadi sasa, Simba imeshatambulisha wachezaji watatu wote wakiwa wa kigeni ambao ni beki, Che Fondoh Malone, winga Aubin Kramo pamoja na mshambuliaji Willy Onana.

Kusajiliwa kwa Onana na Kramo, kunaifanya Simba hadi sasa iwe na wachezaji 11 wanaocheza nafasi za ushambuliaji ambao ni Jean Baleke, Onana, Kramo, Jimmyson Mwanuke, Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, John Bocco, Pape Sakhjo,Kibu Denis, Peter Banda na Mohamed Musa.

Hii inamaanisha kuwa nafasi za ukipa, mabeki pamoja na viungo wa ulinzi zinapaswa kuwa na wachezaji 19 tu ili kutimiza idadi ya wachezaji 30 wa kikosi cha Simba msimu ujao.

Katika msimu uliomalizika, hayo ni maeneo ambayo Simba ilionesha kuwa na uhitaji mkubwa wa sio tu wa namba bali pia ubora ili kulipa wigo mpana wa uteuzi benchi lake la ufundi katika upangaji wa kikosi katika mashindano ambayo yalikuwa yakiikabili.

Na wakati huu wa dirisha la usajili, maeneo hayo yamezidi kupata upungufu zaidi kutokana na kupewa mkono wa kwaheri kwa wachezaji wengi wanaocheza katika nafasi hizo huku pia kukiwa na majeruhi.

Nafasi ya kiungo wa ulinzi, imeondokewa na Jonas Mkude na Erasto Nyoni, mabeki watatu wameondoka ambao ni Joash Onyango, Gadiel Michael na Mohamed Ouattara huku pia kipa Aishi Manula yeye akipata majeraha.

Haya ndio yalipaswa kupewa kipaumbele zaidi na Simba katika dirisha hili linaloendelea la usajili badala ya kujikita na usajili wa wachezaji wa nafasi za mbele ambako haikuonyesha uhitaji mkubwa.

Wakati msimu uliopita unaendelea, Simba ilionyesha uhitaji wa beki wa kimataifa wa kati ambaye angeweza kuwapa ushindani Enock Inonga na Joash Onyango ambao ndio walikuwa wakipangwa katika nafasi hiyo.

Kwa vile Onyango na Ouattara wameondoka, Simba ilipaswa kusajili wachezaji wawili wa kigeni ili kuziba nafasi zao lakini imemnasa Malone pekee huku ikionekana haina mpango wa kusajili beki mwingine wa kati wa kigeni na ina wachezaji watatu tu wa kucheza katika nafasi hiyo, vipi kama ikitokea inamkosa mmojawapo, wawili au wote watatu kutokana na majeraha au adhabu ya kukosa mechi?

Imeondokewa na viungo wawili wa ulinzi na imebaki na wawili wenye ubora wa kiushindani wa kumudu mashindano yaliyo mbele yake ambao ni Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute, inakumbuka kuhusu hilo au inawaza kutanua kifua cha baunsa tu ka kujaza mawinga na washambuliaji huku nyuma inapasahau.

Ukiangalia kwa sasa, hakuna kundi kubwa la wachezaji wa ndani wenye ubora mkubwa wa kumudu ushindani wa mechi za kimataifa ambazo Simba itashiriki hivyo kimbilio kubwa kwa sasa ni wachezaji wa kigeni, inakuwa vipi Simba inaendelea kujaza wachezaji wa nafasi za mbele ambazo hazikuonyesha udhaifu mkubwa msimu uliopita huku zile za nyuma zikionekana kusahaulika?

Timu imara na inayohitaji kushinda makombe, hutoa kipaumbele zaidi katika eneo la ulinzi kwa vile uimara wa hapo ndio unaiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa mataji, Simba inakubali vipi kuwa na kikosi chenye namba ndogo ya wachezaji wa safu ya ulinzi?

Eneo hilo ni nyeti sana na ndilo ambalo Simba ilipaswa kuumiza zaidi kichwa ili kupata wachezaji wazuri na wa kutosha ili isiwe na presha kubwa iwapo mchezaji anapopata majeraha au kutumikia adhabu lakini kwa kinachoendelea sasa, inaonekana bado inawaza wale wa ushambuliaji tu ambao wengi hawakuonyesha mapungufu msimu uliomalizika.

Hadi sasa, Simba ina wachezaji tisa wa kigeni, hivyo imebaki na nafasi tatu tu lakini bado ina uhitaji wa kipa, beki mmoja wa kati, kiungo mshambuliaji wa kumsaidia Chama na bejki mwingine wa kati, dalili zinaonyesha kuwa kuna nafasi kati ya hizo itabaki bila kupata mchezaji wa kigeni ili kukidhi matakwa ya kikanuni.

Eneo la ushambuliaji la Simba halikuwa na shida kubwa sana msimu uliopita kiasi cha kuifanya timu hiyo kuanza kulipa kipaumbele badala ya nafasi nyingine na uthibitisho wa namba unadhihirisha hilo.

Mfano katika Ligi Kuu msimu uliopita, Simba ilifunga mabao 75, kati ya hayo mabao 59 yalifungwa na washambuliaji, mabao nane yakifungwa na viungo, sita yakiwa ya mabeki na mawili ya kujifunga, hii inamaanisha kuwa wachezaji wa mbele walitimiza vyema jaukumu yao, iweje tena Simba iwe na presha na eneo hilo? Unapojaza wachezaji wa nafasi moja, unapunguza uwezekano wa kuwa na namba iliyo na uwiano mzuri katika nafasi nyingine na hicho ndicho kinaonekana kuinyemelea Simba katika msimu unaofuata.

Ikiwa Baleke atakosekana Simba inaweza kuwatumia Bocco, Onana na Mohamed Musa. Iwapo Kibu na Saido wakikosekana Simba itawatumia Kramo, Sakho na Banda. Je wakikosekana Tshabalala, Inonga, Malone, Mzamiru, Kanoute na Chama nafasi zao zitazibwa na nani?

Ukikipanga kikosi cha kwanza cha Simba msimu ujao, kuna nafasi zinaonekana wazi bado hazina wachezaji wa kutumika pindi walioanza wakikosekana. Hapa ndipo pa kuanzia katika usajili sio kujaza watu katika zile ambazo hazionyeshi uhitaji mkubwa. Usajili bado unaendelea, Simba wana nafasi ya kujitafakari na kutoamua au kuamua kutengeneza mwili wa baunsa kwenye kikosi chao.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: