Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo la Simba liko hapa

Simba 067333455 Tatizo la Simba liko hapa

Tue, 27 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika misimu 10 iliyopita ya Ligi Kuu Bara kuanzia 2013-14 hadi 2023-24, Simba imepata tuzo sita za Mfungaji Bora wa ligi hiyo.

Msimu uliopita tuzo hiyo ilikwenda Yanga ikichukuliwa na Stephane Aziz Ki aliyefunga mabao 21 akifuatiwa na Feisal Salum wa Azam (19). Hawa wote wanacheza nafasi ya kiungo.

Ukiangalia kikosi cha Simba hivi sasa kina maingizo mapya 15 katika nafasi zote kuanzia kipa hadi ushambuliaji.

Hii yote ni katika kuendelea kuimarisha kikosi chao kukirudisha kwenye ushindani wa mataji baada ya kukosa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA misimu mitatu mfululizo.

Katika maboresho ya eneo la ushambuliaji, imeonekana kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ambayo yanaacha maswali mengi.

Kwa muda mrefu kipindi cha usajili, Simba imekuwa ikiwashangaza wengi kwa uamuzi wake wa kuwaondoa washambuliaji wanaoonekana kuwa vizuri na kuleta wengine ambao baadhi wanashindwa kufikia matarajio.

Hivi sasa wamemleta mshambuliaji Leonel Ateba raia wa Cameroon, hiyo ni baada ya benchi la ufundi chini ya Fadlu Davids kutoridhishwa na mwenendo wa waliopo.

Kumbuka kabla ya ujio wa Ateba dakika za mwisho kabla ya usajili kufungwa, Simba ilimsajili Steven Mukwala raia wa Uganda ambaye ametokea Ligi Kuu ya Ghana katika timu ya Asante Kotoko.

Mwanzo Mukwala alionekana kuwa suluhisho la ushambuliaji Simba kutokana na msimu uliopita Ligi Kuu ya Ghana kufunga mabao 14 na asisti 2 katika mechi 28, lakini ghafla kibao kikageuka.

Ateba naye akitokea USM Alger ya Algeria, namba zake zinaonyesha kwamba alifunga mabao matatu na asisti nne katika mechi 19 za michuano yote aliyocheza ndani ya kipindi cha miezi sita. Katika kipindi kama hicho cha miezi sita, Freddy alifunga mabao nane katika mashindano yote akiwa Simba.

Rekodi za Ateba anayeonekana kuaminiwa kuja kutibu eneo la ushambuliaji, huku akiondolewa Freddy Michael aliyefunga zaidi yake, zinatukumbusha yaliyowahi kufanywa na Simba miaka ya nyuma katika uamuzi wa kuimarisha safu ya ushambuliaji.

Amissi Tambwe

Katika msimu wa 2013/14, Simba ilimsajili Amissi Tambwe raia wa Burundi, akamaliza ligi kinara wa mabao akifunga 19. Lakini msimu uliofuatia, aliachwa dirisha dogo.

Baada ya kuachwa dirisha dogo msimu uliofuatia akiwa amefunga bao moja, akajiunga na Yanga akamaliza msimu na mabao 14 kutokana na kufunga 13 ndani ya Yanga akiwa namba mbili kwa ufungaji bora wa jumla nyuma ya Simon Msuva wa Yanga aliyefunga 17. Simba kinara wao wa mabao alikuwa Emmanuel Okwi aliyefunga 10. Wakati Tambwe ameondoka alisajiliwa Mganda, Dan Sserunkuma ambaye alidumu nusu msimu akasema bila ya kufikia matarajio ya timu.

Ikumbukwe kwamba, Tambwe aliendelea kukiwasha ndani ya Yanga kwani msimu wa 2015/16 akafunga mabao 21 na kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu akimuacha Hamis Kiiza wa Simba nafasi ya pili na mabao 19.

Wakati Tambwe akiendelea kuwaonyesha Simba walikosea kumuacha mapema, timu hiyo ilitafuta washambuliaji wengine wa kimataifa katika msimu wa 2016/17 wakimshusha Laudit Mavugo na Fredrick Blagnon lakini hawakufua dafu. Mavugo alimaliza ligi na mabao 7 wakati Blagnon (3), yakiwa ni machache wakipitwa na viungo Shiza Kichuya (12) na Mzamiru Yassin (8).

Baadaye walipata dawa msimu wa 2017/18 pale Emmanuel Okwi alipokuwa Mfungaji Bora Emmanuel Okwi akifunga mabao 20 akifuatiwa na John Bocco (14) wakati Laudit Mavugo akiendelea kujitafuta akifunga 4.

Meddie Kagere Naye alikuwa moto msimu wa 2018/19 na 2019/20 ambayo yote alikuwa mfungaji bora akifunga mabao 23 na 22. Katika msimu wake wa tatu alifunga mabao 13 kisha 7, Simba ikaona chaji imeisha, wakaachana naye kirahisi.

Chris Mugalu Alikuwa mshambuliaji kinara katika eneo la ushambuliaji akifanya vizuri kimataifa, lakini alipoachwa ilishtusha kidogo kwani alikuwa bado anahitajika.

Katika msimu wa 2020/21 wakati John Bocco akiwa kinara wa mabao Ligi Kuu akifunga 16, Mugalu alikuwa wa pili na mabao 15, wakati Kagere wa nne akifunga 13, katika nne bora, Simba ilitoa washambuliaji watatu, baadae wakaonekana hawafai wakaletwa wengine ambao walishindwa kufikia malengo kwani ilishuhudiwa msimu wa 2021/22 kinara wa mabao ndani ya Simba akiwa Kibu Denis aliyefunga 8.

Saidi Ntibazonkiza Alifanya vizuri ndani ya Simba kabla ya kuachwa mwishoni mwa msimu uliopita. Msimu wa kwanza ndani ya Simba 2022/23 aliingia dirisha dogo akitokea Geita Gold, akawa mfungaji bora sawa na Fiston Mayele wa Yanga wote wakifunga 17.

Msimu uliopita alifunga mabao 10 na ndiye kinara wa mabao ndani ya Simba, lakini ameachwa. Kumbuka wakati Simba ikiimarisha eneo la ushambuliaji msimu wa 2022/23 ilimshusha Moses Phiri kutoka Zambia na Dejan Georgijevic raia wa Serbia. Phiri alimaliza na mabao 10 wakati Dejan alisepa dirisha dogo na bao moja.

Hamis Kiiza Alifanya vizuri msimu wa 2015/16 akafunga mabao 19 akishika nafasi ya pili kwa ufungaji Ligi Kuu nyuma ya Amissi Tambwe wa Yanga aliyefunga 21. Naye hakudumu sana, akaondoka.

Jean Baleke Alikuwa mshambuliaji kinara wa Simba akiingia dirisha dogo msimu wa 2022/23 akamaliza na mabao nane, msimu uliofuatia 2023/24 akafunga mengine nane lakini akaishia dirisha dogo akaondoshwa.

Baleke aliondoka Simba akiwa bado anahitajika kwani waliokuja nyuma yake walishindwa kumfikia kwa mabao ambao ni Freddy Michael (6) na Pa Omar Jobe (1).

Moses Phiri Msimu mmoja na nusu alicheza Simba, ule wa kwanza 2022/23 alifunga mabao 10, kisha ule wa pili aliocheza nusu akafunga matatu. Akasepeshwa. Freddy Michael aliyekuja baada ya kuondoka yeye, alijitahidi kufunga mabao mengi zaidi (6) lakini Pa Omar Jobe alifeli akifunga moja.

Freddy Michael Ameingia dirisha dogo Simba msimu wa 2023/24 akafunga mabao sita Ligi Kuu. Alipotoka Zambia alifunga mabao 11 nusu msimu, jumla msimu wa 2023/24 alifunga mabao 17.

Waliokuja badala yake wana kazi ya ziada lakini hata rekodi zao za msimu uliopita zimezidiwa na za Freddy.

Steven Mukwala msimu uliopita Ligi Kuu ya Ghana, alifunga mabao 14, wakati Ateba akifunga mabao jumla ya mabao 10, matatu nusu msimu akiwa USM Alger na saba alicheza Douala ya Cameroon akicheza pia nusu msimu.

Wakati Freddy anaondoka na anakuja Ateba, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema hayo ni maamuzi ya kocha.

"Tukiwa pre-season Misri, kocha hakuridhishwa na viwango vya washambuliaji waliopo ndio maana akataka mshambuliaji mwingine na Freddy hakuwa katika mipango yake."

Hivi karibuni Freddy alipopata dili Algeria, Ahmed Ally alisema: "Freddy bado alikuwa na mkataba na sisi, tumepata ofa kutoka Algeria hivyo anaenda huko. "Anaondoka Simba baada ya kutokuwa kwenye mipango ya kocha licha ya kwamba bado tulikuwa na mkataba naye."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: