Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Skudu, Maxi wampagawisha Gamondi

Maxi Avic Town Skudu, Maxi wampagawisha Gamondi

Sat, 22 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama ulipanga kukosa kwenye kilele cha wiki ya wananchi pale Uwanja wa Benjamin Mkapa. Badili akili yako,huo moto ulioko huko mazoezini siyo wakuukosa. Mastaa wapya wana vitu haswa.

Baada ya siku kadhaa za mazoezi ya kiufundi, Kamera zilitinga laivu kwenye mazoezi yao pale kambini Avic Town na kujionea ufundi na ubora wa wachezaji wao wapya ambao wamesajiliwa katika dirisha hili kubwa la usajili.

Kila mmoja kwenye nafasi yake amekuwa akionyesha utofauti na kutaka kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha Miguel Gamondi. Lakini kivutio zaidi kwa viongozi na baadhi ya wadau walioruhusiwa kushuhudia tizi hilo ni Maxi Nzengeli Mpia. Huyu ni winga Mkongomani anayefanya vizuri mazoezini ambapo tayari hata Gamondi amemuelewa.

Akiwa mazoezini Maxi ameonyesha ubora na uzoefu mkubwa haswa kwenye eneo la kasi ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu mabeki wa pembeni wa timu hiyo huku pia akiwa mgumu kupoteza mpira kutokana na nguvu za kutosha na uchu alionao.

Akiingia ndani ya eneo la hatari akili yake ni moja tu kama sio kutoa pasi basi kipa ajipange. Ameonyesha akili kubwa kwenye kupiga mashuti makali ambayo yalikuwa ni mtihani kwa makipa wa timu hiyo Aboutwalib Mshery na Metacha Mnata.

Kwa tafrisi ya haraka kama ataendelea na moto huu alionao mazoezini mashabiki kesho Jumamosi watapata raha ya aina yake kwenye Uwanja wa Mkapa dhidi ya Kaizer Chiefs. Lakini ni kama ameshajihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha msimu ujao.

Achana na Maxi kuna huyu winga aliyepewa jezi namba 6. Msauzi, Mahatse Makudubela 'Skudu' nae wamoto kwelikweli mazoezini. Akiwa katika mazoezi yake ya kwanza tu ukiona unaweza kudhani jamaa amekaa na wenzake siku tano.

Ni mchezaji mcheshi na mwenye akili kubwa ya kujichanganya kisela jambo ambalo limefanya kuwa mshikaji na wachezaji wengi kwa haraka na hata mbwembwe zake mazoezini wamezielewa.

Ndani ya uwanja kimbinu ni mahiri wa kuwatoroka mabeki hata kama wako zaidi ya wawili, wepesi wa miguu yake kuuchezea mpira umewafanya mashabiki wanaoangalia mazoezi hayo nje ya uzio wa uwanja huo kujikuta wanashangilia kila anapokamata mpira.

Akizungumzia mchezo wa wiki ya Wananchi, Skudu alisema anafurahia kuja karibu na mchezo huo akisema Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo ndiyo itacheza na Yanga mechi ya kirafiki atawaonyesha kitu kwavile wanamjua vizuri.

"Nimefurahi sana kujiunga na hii klabu kubwa, wakati tunatolewa na Yanga kwenye mashindano ya Afrika niliumia sana lakini baada ya mechi kuisha nikakumbuka umati wa mashabiki tulipocheza hapa, nikaangalia ubora wa wachezaji wa hii timu haraka akili yangu ikaniambia hii ndio timu kubwa na sasa nipo hapa," alisema Skudu ambaye ni raia wa Afrika Kusini wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

"Nimeambiwa siku hiyo ya wananchi inakuwa na shangwe kubwa, mimi nasubiri kwa hamu lakini kama kuna kitu kimenifurahisha basi ni kwamba tutacheza na Amakhosi (Kaizer Chiefs), wananijua mashabiki watafurahi waambieni waje,"alisema Skudu.

Mashabiki wa Yanga pia wanatarajia ujio mpya wa kiungo wao, Jonas Mkude. Jamaa yuko siriazi na pale mazoezini kwanza anaonekana ana furaha akiwa tayari ameshajichanganya na wenzake lakini kuna muunganiko anautengeneza na beki wa kulia Kouassi Yao.

Iko hivi; Yao ni beki wa kupandisha mashambulizi na kupiga krosi za kutosha huku akiwa na mbinu nyingi za kuwapindua mabeki wenzake na kupiga visigino kisha akakutana na Mkude ambaye naye akamuonyesha kwamba Nungunungu yupo akagusa na visigino mashabiki wakafurahia nje.

Mkude ameonyesha kwamba bado zile pasi zake ndefu zipo akiwa ndiye anaongoza kwa kumjulia Yao kwa kumchungulia kwa mbali anavyopanda mbele kisha kumfikishia mipira anayotaka beki huyo ambaye naye akifika mbele jambo ni moja tu krosi kwa washambuliaji wa kati.

Beki wa kushoto, Nickson Kibabage ambaye naye amesajiliwa katika dirisha hili tayari ameshapewa ubavu mmoja wa kushoto huku mkongwe Lomalisa Mutambala naye akipewa shavu lingine wote wakicheza vikosi viwili tofauti wakiwa mazoezini. Gamondi amekuwa akijaribu kumpima Kibabage kwa matumizi ya beki wa kushoto huku kinda huyo akiendelea kuonyesha ubora mkubwa mazoezini kwa kuwa mwepesi wa kukaba na kupandisha mashambulizi kwa haraka.

Kuna kile kitasa kipya beki wa kati Mganda Gift Fred tayari makocha wa timu hiyo wanampigia hesabu za kumpunguza mwili kidogo jukumu ambalo ameachiwa kocha mpya wa mazoezi ya viungo, Taibi Lagrouni.

Kabla ya kazi hiyo haijaanza Gift ameonyesha ubora mkubwa kukabiliana na mipira ya juu ambapo krosi za Yao zile za juu zimekuwa katika wakati mgumu kupita kwa beki huyo raia wa Uganda.

Makocha wa Yanga wameanza kupiga hesabu ndefu kwamba endapo beki huyo atasimama na yule mtu wa kazi Ibrahim Hamad 'Bacca' basi ukuta wao utakuwa wa chuma kupitika kutokana na makali yao.

PACHA YA YAO NA MUSONDA

Mshambuliaji Kennedy Musonda amekuja na kanuni ya dakika 10 kila siku mazoezini. Yuko katika maandalizi makali kambini akionyesha kwa vitendo kwamba anaitaka nafasi sasa ya kuaminiwa kucheza pale kati kama mshambuliaji wa mwisho.

Yaani kwa kifupi anataka kuvaa viatu vya Fiston Mayele kwa asilimia zote. Kwenye mazoezi amejiwekea ratiba moja ya binafsi ya dakika 10 kila siku.

Anafika mapema mazoezini kabla ya wenzake hawajafika kisha anamuomba beki mpya wa kulia Kouassi Yao kumpigia krosi kali kisha yeye anamalizia kwa kuweka mpira wavuni kwa muda usiopungua dakika 10.

Ratiba hiyo pia amekuwa akiifanya hata mazoezi yanapomalizika akipigiwa krosi 10 kila upande kisha anamalizia akitumia ubora wa beki huyo ambaye anaweza pia kucheza kama beki wa kushoto akitumia miguu yote.

Ratiba hiyo imekuwa inawakosha makocha wa timu hiyo hasa kocha msaidizi Mussa Nd'ew ambaye alikuwa mshambuliaji hatari wa zamani wa Wydad Athletic ya Morocco.

Mazoezi hayo sio kwamba amemaliza Musonda raia wa Zambia anapokuwa kwenye mazoezi na wenzake sasa ndio kabisa ambapo amekuwa akipambana kuhakikisha anafunga mabao na juzi jioni akafanikiwa kufunga mara mbili.

Akizungumzia ratiba hiyo Musonda ameliambia Mwanaspoti kuwa tayari akili yake imeshaanza kujipanga kwa hesabu za msimu mpya ambapo anataka kuwa tayari ili aingie kwenye hesabu za kocha mpya Miguel Gamondi.

"Kila kocha anakuja na hesabu zake lakini malengo makuu yanabaki kwamba atahitaji ushindi wa kila mchezo lakini pia kushinda mataji, hapohapo najiuliza kwangu kama mshambuliaji atahitaji nini na majibu yanakuja kwamba atataka kuona nafunga ndio maana naanza kujipanga sasa ili ajue kitu gani ninacho."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: