Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yavunja rekodi yake

Simba SC Mazoezi Ligi.png Kikosi cha Simba

Sun, 24 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga, Azam FC na Simba zinafukuzana kwa ukaribu katika mbio za ubingwa msimu huu kwa kushinda mechi zote tatu za kwanza za Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ni mara ya kwanza wa Wekundu wa Msimbazi baada ya misimu miwili.

Simba na Azam FC zilikamilisha juzi mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu kwa kuibuka na ushindi na kufikisha pointi tisa, sawa na Yanga iliyoifunga Namungo bao 1-0 na kujichimbia kileleni.

Lakini huu umekuwa mwanzo mzuri kwa Simba, ambayo misimu miwili iliyopita ilishindwa kupata ushindi kwenye mechi zote tatu za kwanza, kwani 2020/21, ilianza kwa suluhu ugenini dhidi ya Biashara United, wakati 2021/22 ikishikiliwa na KMC kwa sare ya 2-2.

Azam FC inayoshika nafasi ya pili iliitandika Singida Fountain Gate kwa mabao 2-1, juzi usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, baada ya Simba kuichapa Coastal Union 3-0, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kabla ya timu hizi tatu kucheza, Mashujaa inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza ilishangaza wengi kwa kukaa kileleni mwa msimamo ikishinda mechi mbili na sare moja.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa timu za juu ya msimamo, timu kongwe za Tanzania Prisons, Coastal Union na BNamungo FC zimekuwa na wakati mgumu katika mechi tatu za kwanza msimu huu.

Tanzania Prisons imeshindwa kuibuka na ushindi katika mchezo wowote wa Ligi Kuu msimu huu, ikiambulia sare moja iliyoipa pointi pekee na kufungwa mara mbili, kitu ambacho pia kimetokea kwa Coastal Union na Namungo.

Licha ya mafanikio ya Simba msimu huu, bado baadhi ya mashabiki wanaona bado kuna kitu kinakosekana katika kikosi chao, ambacho kimeshinda mfululizo hadi sasa.

Simba ambayo imeanza msimu kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii mbele ya Yanga, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union, huku nyota wake, Jean Baleke akifunga 'hat-trick'.

Mabao hayo matatu ya Baleke yanamfanya kuwa kinara wa ufungaji akifikisha matano, wakati wanaomfuata wakiwa na mawili kila mmoja, vita ambayo inaonekana kuwa nyepesi kwa nyota huyo msimu huu.

Ukiachilia mbali mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Simba haikuwa na kiwango kibaya uwanjani katika mechi za Ligi Kuu, huku ikilazimisha sare ya 2-2 na Power Dynamos, lakini mashabiki walitaka kiwango bora zaidi.

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' amewataka mashabiki kuendelea kuisapoti timu yao kwani ina uwezekano mkubwa ikawa bora zaidi ya wanavyoitaka sasa.

"Ukiangalia jinsi timu inavyocheza ina mabadiliko ya kila siku, kila mchezaji amekuwa na mabadiliko na nafurahi kuona timu inaimarika na itakuwa bora zaidi," alisema kocha huyo.

Kwa upande wake, kocha msaidizi wa Coastal Union, Fikirini Elias alisema bado wanaamini kuwa kikosi chake kitaimarika baada ya kuwa na mwanzo mbaya wa Ligi Kuu msimu huu tofauti na ilivyotarajiwa.

Ligi Kuu Tanzania Bara itarejea tena Ijumaa, wakati JKT Tanzania itakapokuwa nyumbani kuialika Kagera Sugar, wakati Coastal Union ikitaka kujiuliza mbele ya Kitayosce kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: