Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yakusanya mabao ya Afrika

Onana Willy Esomba Simba yakusanya mabao ya Afrika

Sat, 15 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' ashindwe mwenyewe, alitoa agizo la kila nafasi iwe na ushindani mkali, hilo limetimia kwenye safu yake ya ushambuliaji itakayokuwa na ushindani mkali zaidi baada ya kukusanya mabao ya Afrika katika kikosi cha timu hiyo.

Msimu uliopita timu hiyo iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara, ilikuwa kinara kwa kufunga mabao 75, lakini kama haitoshi kwenye usajili unaoendelea kwa sasa imeongeza mabao mengine kutoka kwa nyota wawili wanaocheza eneo la ushambuliaji.

Simba imemsajili Willy Onana kutoka Rayon Spors aliyekuwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Rwanda akifunga 16 sambamba na Aubin Kramo kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast na kuifanya safu ya mbele kukusanya mabao ya kutosha kabla hata msimu haujaanza.

Simba iliyotoka kapa msimu uliopita kwa kushindwa kutwaa taji lolote mbele ya Yanga, iliongoza kwa mabao 75, lakini 59 yakiwa yamefungwa na washambuliaji wakiongozwa na Saido Ntibazonkiza (mabao 13) mbali na mabao manne aliyotoka nayo Geita Gold na kumfanya awe kinara wa Ligi Kuu sambamba na Fiston Mayele wa Yanga kila mmoja akifunga mabao 17.

Pia kuna mabao 10 kutoka kwa Mzambia Moses Phiri (10), John Bocco (10), Jean Baleke (8), Augustine Okrah (4),Habib Kyombo(2), Peter Banda (1), Kibu Denis (2),Ousmane Sakho(8) na Dejan Georgejevic (1).

Hivyo ujio wa Onana aliyefunga mabao 16 na asisti tano Rayon Sports ataongeza nguvu na idadi zaidi ya mabao endapo tu akiendana na Ligi Kuu ilivyo na ushindani ndani ya kikosi cha Simba.

Kocha Robertinho atakuwa na kazi ya nani ampange kati ya Onana na Baleke, Bocco na Phiri pia itategemeana na ushawishi wao kwenye maandalizi ya msimu ambapo timu hiyo imeweka kambi Ituruki.

Ukiachana na nafasi hiyo, Onana anaweza akacheza kama winga ukiondoa Saido aliyekuwa kinara wa mabao 17 na asisti 12, pia kuna Clatous Chama aliyemaliza na mabao manne na asisti 14, hivyo nafasi zote anazocheza zina watu wenye uwezo mkubwa. Simba ilimuona Kramo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) ambako alimaliza na mabao manne, pia kocha atakuwa na kazi ya ziada kujua nani amuanzishe na nani asubili benchi.

Beki wa zamani wa Yanga, Williams Mtendamema alitoa mtazamo wake kuhusiana na safu ya mbele ya Simba, namna itakavyompa changamoto kocha kujua jinsi ya kuwatumia wote kwa faida.

"Nililiona hilo kwa kocha aliyeondoka Yanga, Nabi Nasreddine jinsi alivyokuwa anampa kila mchezaji nafasi ya kucheza, ndio maana kikosi chake kilikuwa imara sana, vivyo hivyo kwa kocha wa Simba akikitumia kikosi chake vyema kitazalisha mabao mengi zaidi," alisema.

Hoja yake iliungwa mkono na kocha Meja mstaafu wa jeshi, Abdul Mingange aliyesema "Simba ina wachezaji wazuri hasa kwenye safu yao ya ulinzi na wameiboresha zaidi, natarajia itakuwa na ushindani mkali sana."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: