Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba wana mambo mawili tu

VIDEO: Simba Waondoka Tanga, Wawafuata Mtibwa Kibabe!.jpeg Wachezaji wa Simba SC

Sun, 20 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba wana mambo mawili tu Leo kwenye Ligi. Kuendeleza rekodi ya ushindi mbele ya Dodoma lakini kutoa gundu la kutoongoza Ligi.

Simba imeshindwa kuongoza msimamo wa Ligi kwa miezi nane na leo inaweza kukaa kwa mara ya kwanza ikiwa itaibuka na ushindi katika mechi yake ya nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Mara ya mwisho kwa Simba kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ilikuwa ni Disemba 4 mwaka jana na baada ya hapo haikuweza kufanya hivyo tena hadi msimu uliopita ulipomalizika na hata msimu huu ulipoanza bado haijafanikiwa kuwepo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi.

Kuanza kuimarika kwa safu ya ushambuliaji ambayo imepachika mabao manne katika mchezo uliopita ni jambo linaloipa faraja Simba ambayo kabla ya hapo ilicheza mechi za Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Big Stars na Yanga bila kupata bao dakika 90 za mchezo.

Na jambo zuri kwa Simba ni kwamba kati ya mabao hayo manne iliyopata katika mechi iliyopita, matatu yalifungwa na nyota wake wanaocheza katika nafasi za kushambulia ambao ni Clatous Chama, Jean Baleke na Willy Onana.

Wenyeji Simba wamekuwa na historia nzuri ya ubabe dhidi ya Dodoma Jiji kila wakutanapo kwenye ligi ambapo wameshinda michezo yote sita waliyowahi kukutana hapo awali.

Katika mechi hizo sita zilizopita baina yao, Simba imefumania nyavu mara 12 ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa mchezo wakati Dodoma Jiji yenyewe imefunga mabao mawili tu.

Timu zote mbili zinaingia katika mchezo huo zikiwa zimetoka kupata ushindi katika mechi zao za kwanza za ligi kuu msimu huu na ushindi wa leo unaweza kuifanya mojawapo isogee kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Wenyeji Simba wametoka kupata ushindi mnono wa mabao 4-2 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar wakati Dodoma Jiji walipata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Coastal Union.

Katika mchezo huo, Simba itaendelea kumkosa beki wake tegemeo, Henock Inonga ambaye anauguza majeraha yake ya bega aliyoyapata katika mchezo mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Big Stars na Mwanaspoti linajua amerudi kwao DR Congo kujitibia.

Kocha Robertinho alisema: “Tunaingia katika mchezo huu tukiwa na lengo la kufunga mabao na kupata ushindi. Wachezaji wamefanya maandalizi mazuri na wanaonyesha kiwango kizuri na kila mmoja ana nafasi ya kuwemo kikosini. Tunawaheshimu wapinzani wetu Dodoma Jiji na mchezo hauwezi kuwa rahisi lakini tunafahamu mahitaji ya ushindi,” alisema Robertinho ambaye bado baadhi ya mashabiki hawajamuelewa msimu huu.

Kocha msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope alisema: “Tumejipanga vizuri tukijua tunaenda kucheza mechi ngumu kwa sababu Simba ni miongoni mwa timu bora Afrika lakini tumeshawahi kucheza nao na kuwaona wakicheza na tunajua namna ya kuwadhibiti,” alisema Liogope na kusisitiza kuwa rekodi za nyuma hazina lolote kwenye mchezo wa leo kila kitu kitafanyika Uwanjani.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: