Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba vs Yanga; Waleteni hao

Simba Yanga Caf Rank Simba vs Yanga

Thu, 13 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waleteni hao! Ndio kauli ya kijasiri inayotolewa hivi sasa na wachezaji, viongozi na mashabiki wa Simba na Yanga katika kuelekea Kariakoo Dabi.

Kariakoo Dabi hiyo itazikutanisha timu kongwe za Simba dhidi ya Yanga, mchezo utakaopigwa Jumapili hii saa kumi na moja jioni kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zitavaana katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara, wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 la Simba likifungwa Augustine Okrah huku la Yanga likipachwa na Stephane Aziz Ki.

Katika mchezo huo, Simba wataingia uwanjani wakiwa na hasira za kufungwa mara mbili katika Dabi ambayo yote wakifungwa katika michezo miwili mfululizo ya Ngao ya Jamii msimu huu na uliopita.

Kuelekea mchezo huo, kila timu inahitaji ushindi ili ijiweke katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa huo wa ligi katika msimu huu ambao umeonekana ushindani kuongezeka.

Pambano hilo linaongeza utamu kutokana na ubora wa kila timu ambao wanao hivi sasa, kwa timu zote kufuzu hatua ya robo fainali, Simba wakicheza Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Simba wenye pointi 57 katika msimamo wa ligi ndio wenyeji wa mchezo huo, wataingia uwanjani wakiwa na jeuri ya mshambuliaji wao mpya Mkongomani, Jean Baleke aliyepiga hat trick mbili akiwa na msimu wake wa kwanza alizozipiga katika ligi na Kombe la FA.

Yanga ambao ni vinara katika msimamo wa ligi wenye pointi 65 (kabla ya mchezo wa juzi), wana jeuri ya Fiston Mayele ambaye amekuwa katika kiwango bora tangu ajiunge na timu hiyo, katika msimu uliopita hivi sasa ndiye kinara mabao katika ligi akifunga 15 huku anayemfuatia akiwa Moses Phiri anayekipiga Simba mwenye 10. Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba Mbrazil, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alisema kuwa hana presha yoyote kukutana dhidi ya Yanga, kwani anajua vizuri kuzicheza dabi.

“Sina presha kukutana na Yanga, mimi mechi kama hizo ndio nazipenda zile mechi zenye presha ambazo zina mashabiki wengi uwanjani.

“Nimeshinda michezo mingi na mikubwa kwenye uwanja kama Maracana wa kule kwetu Brazil ukiwa umejaa, tunaiheshimu Yanga lakini hata sisi tunaitaka hii mechi ili tuthibitishe ubora wetu kwa mashabiki wetu,” alisema Robertinho.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema kuwa: “Tuna ratiba ngumu mbele, tuna mechi ambazo zinaweza kuamua hatima yetu ya ubingwa wa ligi na Caf.

“Nimezungumza na wachezaji wote na nimewaambia mashabiki wanategemea makubwa kutoka kwetu hivyo ni lazima waongeze bidii mazoezini ili kufikia malengo yetu msimu huu.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: