Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mwendo wa kimyakimya

Vigogo Simba Kimya Kimya Simba mwendo wa kimyakimya

Tue, 20 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mabosi wa Simba wanaendelea kufanya usajili wa kimya kimya kutekeleza mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' aliyepo mapumziko kwao Brazili, huku ikiendelea kuzungumza na baadhi ya nyota wa kikosi cha sasa kwa ajili ya kuwapa 'Thank You'.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo na kukwamia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iking'olewa na waliokuwa watetezi wa taji, Wydad Casabalanca, inataka kusafisha baadhi ya wachezaji ili kujenga kikosi kipya.

Hata hivyo, inaelezwa kuna baadhi ya wachezaji waliopendekezwa kupigwa wana mikataba ya muda mrefu, hivyo kuwafanya mabosi hao kukuna kichwa kwa kutambua watalazimika kuingia gharama za kuvunja mikataba, lakini wapo wengine wanaojadiliana nao kuwatoa kwa mkopo kwa timu nyingine.

Chanzo cha ndani kutoka Simba kinasema mara muafaka utakapopatikana kwa wachezaji watakaotemwa jumla zitatolewa 'thank you' kama ilivyokuwa kwa Mghana Augustine Okrah na makocha waliotemwa wakiwamo wa makipa, Chlouha Zakaria, Kocha wa viungo, Kelvin Mandla, Mtaalamu wa viungo, Fareed Cassim na Kocha wa Simba Queens, Charles Lukula.

"Bado tunaendelea kujadili wachezaji wa kuachana nao, lakini kuna wenye mikataba ni lazima tuzungumze nao tupate muafaka, kuna wa kuwatoa kwa mkopo na wengine wameomba kuondoka. Ila kila kitu kitawekwa bayana mambo yakikamilika," kilisema chanzo hicho.

Mmoja ya wachezaji wanaojadiliwa baada ya kuandika barua ya kutaka kuondoka ni beki Joash Onyango, huku kiungo Sadio Kanoute akirejea kwao akiwa hajakamilisha mazungumzo ya kubakishwa kikosini, ikielezwa mkataba wake wa miaka miwili unaelekea ukingoni. Kiungo huyo kutoka Mali, alisajiliwa na Simba Agosti 20, 2021 akitokea klabu ya Al-Ahli Benghazi ya Libya.

Mbali na Kanoute na Onyango, wengine wanaojadiliwa ni pamoja na Ismael Sawadogo, Jonas Mkude, Habib Kyombo, Jimmyson Mwanuke na Nassor Kapama.

Chanzo hicho kiliongeza mbali na kuwajadili wachezaji watakaotemwa, lakini viongozi wanaendelea kufanya mazungumzo na wachezaji walio kwenye mipango ya benchi la ufundi baada ya baadhi yao kukamilishiwa dili, japo hakuweka bayana ni kina nani waliosainiwa.

Mwishoni mwa wiki katika hafla ya kutambulisha kampuni ya Sandaland iliyoingia mkataba na Simba ya kutengeneza na kusambaza jezi, Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again' aliweka bayana kwamba msimu huu wamejipanga kufanya usajili makini ili kurejesha heshima ya klabu hiyo ndani na anga la kimataifa.

"Nampongeza Sandaland kwa kupata nafasi hii, alijaribu mara ya kwanza hakufanikiwa lakini muda huu amepata. Namshukuru pia VunjaBei kwa udhamini aliotupatia. Tunajipanga kusajili timu yenye ubora na usajili unakwenda vizuri. Simba inakwenda kuondoa unyonge," alinukuliwa Try Again.

Licha ya kufanywa siri kwenye sajili za wachezaji wapya, lakini Mwanaspoti limedokeswa Leandre Onana wa Rayon Sports ya Rwanda ameshasaini mkataba wa miaka miwili kisha kwenda kuagana na mabosi wake wa zamani ili kujiandaa kuja nchini kulianzisha akiwa na Wekundu wa Msimbazi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: