Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kwa Mkapa ni Unyama mwingi mpaka unyama tena!

Simba Unyamaaaa Simba kwa Mkapa ni Unyama mwingi mpaka unyama tena!

Sun, 6 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mashabiki wa Simba wanahesabu saa tu kabla ya kushuka Kwa Mkapa ili kushangweka katika Tamasha la kibabe la Simba Day. Ni siku ambayo huenda kukashuhudiwa Farasi kadhaa wakiwa wamewabeba viongozi wa Simba.

Hili ni zaidi ya tamasha. Hii ni sikukuu kwa wanasimba kutokana na ukweli mbali na kuwapa fursa wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kushuhudia utambulisho wa kikosi kipya cha msimu ujao, lakini watapata burudani mbalimbali uwanjani hapo.Usisahau tangu Alhamisi tiketi ziliisha, kwahiyo kama huna tiketi mpaka sasa tulia zako kwenye runinga.

Ukiachana na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali, pia kutakuwa na mechi za utangulizi kabla ya pati kufungwa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Simba na Power Dynamo kutoka Zambia.

Tofauti na kawaida wakati tamasha likiasisiwa mwaka 2009, msimu huu tamasha linafanyika Agosti 6 badala ya nane iliyozoeleka kutokana na muingiliano wa ratiba za michuano ya Ngao ya Jamii itakayopigwa jijini Tanga ambayo itaanza mechi za awali za nusu fainali Agosti 9.

Tamasha la safari hii ni la 15 tangu lilipoanzishwa mwaka 2009 chini ya uongozi wa Hassan Dalali ‘Field Marshal’ na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda’ na wenzao ambao baadhi yao wametangulia mbele ya haki.

Kina Dalali waliasisi siku hiyo ili kukutanisha wanasimba wote ili kupanga mikakati ya maendeleo kwa timu yao kabla ya kugeuzwa kuwa ni mahususi kutambulisha kikosi na jezi mpya za msimu ikiambatana na mechi maalumu ya kirafiki.

Simba inalifanya tamasha hilo siku nne tu kabla ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Fountain Gate utakaotanguliwa na mechi nyingi ya awali ya michuano hiyo itakayokutanisha watani wao, Yanga dhidi ya Azam.

Mechi za Ngao safari hii inahusisha timu nne badala ya mbili kama ilivyozoeleka kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) ikiwa ni uzinduzi wa msimu wa 60 wa Ligi Kuu Bara tangu ilipoasisiwa mwaka 1965.

Ligi ya msimu huu imepangwa kuanza Agosti 15 ikishirikisha timu 16, zikiwamo tatu zilizopanda daraja kutoka Championship, JKT Tanzania, Mashujaa na Tabora United (Kitayosce).

Wakati wanasimba wakijiandaa na tamasha hilo linaloenda sambamba na maadhimisho ya miaka 87 tangu kuasisiwa kwa klabu yao mwaka 1936, Mwanaspoti inakuletea baadhi ya rekodi za kusisimua za Simba ambayo misimu miwili mfululizo iliyopita iliambulia patupu kwa kukosa taji hata moja.

KILA JIPYA LAO

Licha ya Simba kukosa mataji misimu miwili iliyopita, lakini klabu hiyo ina rekodi tamu ya kuwa Wazee wa Kuliamsha, yaani kila kitu kipya wapo wanaongoza kulianzisha.

Ndio, achana na rekodi za kuwa klabu ya kwanza kuvaa jezi na viatu nchini ama kumiliki gari ama kuwazawadiwa nyota wake magari, Simba pia ina rekodi nyingine tamu ikiwamo ya kuwa timu yenye bahati ya kunyakua kila taji jipya lililoanzishwa.

Simba ndio klabu ya kwanza kubeba taji la Ligi ya Soka Tanzania (sasa Ligi Kuu Bara) ikifanya hivyo mwaka 1965. Klabu hiyo ilibeba bila kutoka jasho baada ya watani zao Yanga kususia mechi yao iliyovunjika dakika ya 80, huku wakiwa mbele kwa bao 1-0 na Chama cha Soka (FAT) kuamuru urudiwe na Vijana wa Jangwani kuingia mitini na Simba kupewa taji.

Simba ililitetea taji hilo kipindi hicho ikitumia jina la Sunderland kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Simba mwaka 1971. Klabu sita pekee ndizo zilizoasisi Ligi Kuu ya sasa ambazo ni Tobacco au Sigara (Pwani), Young African, Coastal Union na Manchester United (Tanga), TPC (Moshi) na mabingwa Sunderland (Pwani).

Pia Simba ndiye klabu ya kwanza kubeba taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame) ikifanya hivyo mwaka 1974.

Kama haitoshi imelibeba pia taji la Tusker lilioasisiwa mwaka 2001 na kulitetea kwa miaka mingine miwili mfululizo, kadhalika ilikuwa ya kwanza kubeba taji la michuano ya BancABCSuper8 iliyofanyika mara mmoja tu na kuzimika 2012.

Na hata ishu za matamasha ni Simba iliyoyaasisi kwa kuleta Simba Day likiwa tamasha la kwanza kwa klabu za soka nchini, kabla ya Yanga, Azam, Ndanda, Geita Gold na sasa Singida Fountain Gate nao kuiga, mbali kuwa klabu ya kwanza kuingia mfumo wa hisa ikiwapiga bao watani zao Yanga.

KIMATAIFA NDO USISEME

Licha ya Yanga kuwa klabu za kwanza kuiwakilisha nchi kikamilifu katika michuano ya kimataifa kwa timu za Tanzania na kufika robo fainali kwa miaka miwili mfululizo 1969 na 1970, lakini Simba ndiyo yenye rekodi tamu katika mechi za kimataifa.

Simba ndio klabu ya kwanza Tanzania kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika), ikifanya hivyo mwaka 1974, pia ilikuwa klabu ya kwanza Bongo kufika fainali za Afrika ikifanya hivyo kwenye michuano ya Kombe la CAF 1993 (kwa sasa michuano hiyo haipo tena).

Simba ilipoteza 2-0 nyumbani mbele ya Stella Abidjan baada ya suluhu ya mechi ya ugenini, Ivory Coast, pia ndio klabu pekee nchini kuwahi kumvua taji mtetezi wa Afrika ikifanya hivyo 2003 dhidi ya Zamalek ya Misri na kutinga makundi.

Simba pia ndio klabu inayoongoza kwa kufika mara nyingi hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF kwa miaka ya karibuni, ikitinga mara nne Ligi ya Mabingwa Afrika na mara moja katika Kombe la Shirikisho (michuano iliyounganishwa Kombe la Washindi na Kombe la CAF, mwaka 2004).

Kubwa linalokumbukwa kwenye anga hizo za kimataifa ni rekodi ya kipekee ambayo haijawahi kufikiwa na klabu yoyote nchini, Afrika na duniani kwa ujumla kupindua matokeo ya kufungwa nyumbani mabao 4-0 na Mufurila Wanderers ya Zambia mwaka 1979 na kwenda kushinda ugenini 5-0.

WAZEE WA DOZI NENE

Kama unashangaa Simba kwenda kuwafunga Wazambia nyumbani kwao na kusonga mbele kibabe, hata kwenye soka la ndani Mnyama wanasifikia kwa kugawa dozi nene.

Ni kweli Yanga ndio klabu ya kwanza kutoa kipigo kikali katika mechi ya watani wa jadi nchini ikiisulubu Simba mabao 5-0 mnamo Juni 1, 1968, ila kwa miaka 46 sasa inateseka na kipigo cha paka mwizi ilichopewa na Simba mwaka 1977 wakati Wekundu wakilipa kisasi.

Simba ililipa kisasi hicho na kuandikisha rekodi inatowatesa Yanga kwa miaka zaidi ya 40 kwa kuifumua mabao 6-0 Julai 19, 1977 ikishuhudiwa King Abdallah Kibadeni akipiga hat trick. Hat trick pekee katika Kariakoo derby.

Kama haitoshi wakati Yanga ikipambana kutaka kufuta aibu hiyo wakati ikitimiza miaka 35, iliongezewa tena dozi kwa kukandikwa mabao 5-0 na Simba katika mechi ya Mei 6, 2012.

Kama unataka kuwakera Wanayanga wakumbushie vipigo hivyo vya paka mwizi ilivyopewa timu yao na wapinzani wao hao.

Hata kwenye michuano mingine Simba imekuwa ikitoa dozi kwa watani wao, ikifanya kwenye Kombe la Tusker na Mapinduzi na hata mwaka jana katika Kombe la Shirikisho (ASFC) waliwanyoosha watani wao kwa mabao 4-1.

JUMBA LA MATAJI

Ukiondoa mataji 22 iliyonayo katika Ligi Kuu Bara ikiwa nyuma ya Yanga iliyotwaa mara 29, Simba pia ina mataji mengine lukuki yanayoifanya itishe kwa klabu za soka za Tanzania.

Katika Ligi, Simba ilibeba mataji yake 22 katika misimu ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2009-10, 2011-12, 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2021.

Katika Kombe la Kagame Simba inashikilia rekodi ya kubeba mataji mengi, ikifanya hivyo mara sita katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002.

Simba pia inashikilia rekodi ya kubeba Kombe la Tusker mara nyingi zaidi kwa klabu za Afrika Mashariki ikifanya hivyo mara nne 2001, 2002, 2003 na 2005.

Katika Ligi Kuu ya Muungano pia ilimenyakua jumla ya mataji sita ikifanya hivyo 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002, huku katika Kombe la Nyerere (FA, sasa ASFC) imenyakua mara sita miaka ya 1984, 1995, 2000, 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021.

Pia imebeba mataji matatu ya michuano ya Kombe la Mapinduzi inayofanyika kila mwanzoni mwa mwaka visiwani Zanzibar, hapo ni mbali na Ngao ya Jamii ikiwa ndio kinara ikibeba mara tisa, pia imewahi kubeba taji la michuano ya Kombe la CCM. Ukipiga hesabu za haraka ni kwamba Simba ina mataji karibu 50, halafu wala hawaringi!

HUKU NAKO BALAA

Simba ni moja ya klabu inayoongoza nchini kwa kuuza wachezaji wake nje ya nchi tangu miaka ya nyuma, wenyewe wanasema mabosi wake hawana mbambamba linapokuja dili la mchezaji kutakiwa nje ya nchi.

Utabisha nini wakati kina Idd Pazi ‘Father’ alikuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kucheza soka la kulipwa Indonesia miaka ya 1980 kabla ya kina Athuman Machuppa, Henry Joseph, Haruna Moshi, Nico na Renatus Njohole kama sio Mbwana Samatta na wachezaji wa kigeni kama Emmanuel Okwi, Patrick Ochan na sasa Pape Ousmane Sakho wote wameuza na kuiingizia klabu fedha za kutosha.

Mbali na kuuza wachezaji nje ya nchi, lakini Simba kwa miaka ya karibuni kupitia mradi wake wa vijana U20 wamesambaza wachezaji karibu kila klabu ya Ligi Kuu Bara na madaraja mengine hata kama haikuwauza, lakini ni chumo la mikono ya Wekundu hao.

Katika soka la Wanawake, Simba pia wamefunika mbaya ikiwa imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) mara tatu mfululizo ikiwa ni rekodi, lakini imetwaa ubingwa wa Cecafa na kushiriki fainali za Klabu Bingwa Afrika msimu uliopita na kufika nusu fainali, ikimaliza ya nne.

Sasa kwa rekodi hizo tamu kwanini Wekundu wa Msimbazi wasiitwe ‘Taifa Kubwa’? Kwa hakika kabisa Simba levo ya mbali na wana kila sababu ya kutamba kwani, unyama ni mwingi kwelikweli!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: