Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga yoyote aje tu!

Simba Yanga Caf Rank Simba, Yanga yoyote aje tu!

Wed, 5 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Leo ni siku muhimu kwa soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla wakati ambapo droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali itakuwa ikipangwa pale Cairo nchini Misri.

Kutokana na uwezo ambao Simba na Yanga wameonyesha hatua ya makundi, ukweli ni kwamba sasa wanamtaka yeyote na wanaweza kupambana naye.

Tofauti na miaka kadhaa iliyopita, hii itakuwa mara kwanza kwa mashabiki wa Simba na Yanga kukaa wakisubiri kufahamu timu yao itavaana na nani kwenye robo, awali miaka ya hivi karibuni Simba ndiyo pekee walikuwa wanasubiri droo hii.

Simba ambayo imefuzu hatua hiyo kwa miaka mitatu ya hivi karibuni imekuwa ikiishia hapa lakini sasa inataka kuvuka hapa, wakati ambapo itavaana na aidha Wydad, Mamelodi au Esperance de Tunis na wataanzia nyumbani Dar na kumaliza ugenini.

Huku Yanga yenyewe ikiwa imefika hatua hii kwa mara ya kwanza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika nayo ikiwa inatafuta nafasi ya kwenda mbele zaidi ambapo baada ya kumaliza ya kwanza kwenye kundi lake sasa itavaana na kigogo mmoja, aidha Us Algier, Rivers United au Pyramids, lakii itakuwa na faida ya kuanzia ugenini na kuja kumalizia nyumbani.

LIGI YA MABINGWA

Simba tayari imeshaonyesha umwamba wake msimu huu ikiwapasua Vipers nyumbani na ugenini, lakini wakiwa pia wamepata ushindi dhidi ya Horoya wa mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, ukweli ni kwamba wanaonekana kuwa tayari kwa ajili ya mchezo wa robo fainali na yeyote wanayeweza kukutana naye wanaweza kumpasua.

Simba wanaweza kukutana na Mamelodi ya Afrika Kusini timu iliyoshika nafasi ya pili kwa kupiga mashuti hatua ya makundi, Mabingwa watetezi Waydad Casablanca au Esperance de Tunis ya Tunisia kwenye droo itakayopangwa kesho.

Simba wamezichapa timu kubwa huko nyuma kama Al Ahly ya Misri wakati ikiwa kwenye ubora wa hali ya juu haina hofu na timu yoyote.

Endapo itapangwa na Mamelodi , Simba watalazima kurejea tena Afrika Kusini kwa miaka ya hivi karibuni baada ya awali kuchapwa mabao 4-0 na Kaizer Chiefs kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho, lakini Mamelodi wa sasa wakiwa wa moto zaidi baada ya kuonyesha ubora wa juu kwenye michezo yake.

Kwenye Kundi B, ambalo Mamelodi walifuzu wakiwa na Al Ahly hawakupoteza mchezo hata mmoja baada ya kuambulia sare mbili wamekuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao baada ya kufunga 14 na kufungwa saba tu wakiwa wamekusanya pointi 14 kwenye michezo sita waliyocheza hadi sasa, hata hivyo hawatarajii kukutana na mechi rahisi kutoka kwa Simba.

Simba kwenye michezo sita wamekusanya pointi tisa tu, lakini wakiwa wanazitisha timu zote ambazo wanakutana nazo kutokana na uwezo wa juu wa kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Mkapa ikiwa ni sehemu ambayo walifanikiwa kuwachapa Al Ahily, Horoya, AS Vita, Vipers, Kaizer Chiefs na timu nyingine kubwa, lakini msimu huu wakiwa na wastani mzuri wa mabao baada ya kufunga mara kumi wakiwa wanashika nafasi ya pili kwa timu iliyomaliza ya pili kwenye makundi yote.

Mbali na hawa Simba wanaweza pia kupangwa na Waydad ambao ndiyo mabingwa watetezi, hawa waliomaliza kwenye Kundi A wakiwa vinara na pointi 13, wamepoteza mchezo mmoja na kutoka sare mmoja ikiwa ni timu tishio kwenye aridhi ya nyumbani kwao Morocco.

Simba wakipangwa na hawa wanaweza kurudi kwenye Uwanja wa Stade Mohamed V, sehemu ambayo walichapwa mabao 3-1 na Raja Casablanca.

Hii ni timu kubwa nchini Morocco ikiwa na mashabiki wengi, siyo timu rahisi sana ikiwa imeruhusu kufungwa bao moja tu kwenye michezo sita lakini ikiwa imefunga mabao saba, hapa ni sehemu ambayo Simba wasingependa kurudi tena, lakini ikitokea, hawana jinsi watapambana.

Esperance na Simba ni mechi nyingine ambayo mashabiki wa Simba wanatamani kuiona kwenye Uwanja wa Mkapa, hawa ni mabingwa wazamani wa michuano hii lakini ikiwa ni timu yenye ulinzi mkali lakini pia ikiwa haina safu kali ya ushambuliaji ndiyo maana kwenye michezo sita ina wastani wa bao moja kwenye kila mchezo.

Espérance de Tunis wametwaa ubingwa mara nne, hawa Simba wanaweza kuomba kukutana nao, wameonekama kushuka sana kwa kipindi cha hivi karibuni, hawana makali ya kufunga mabao na hawana makali ya ulinzi, ukiwatazama wamefanikiwa kufunga mabao sita, lakini wakiwa wameruhusu kufungwa manne kwenye michezo sita, inawezekana huko Simba walipo wanasema tupeni hawa tuwanyooshe.

Wanaonekana kuwa bora zaidi wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani pale Tunisia lakini wanapata wakati mgumu sana wakitoka nje ya hapo, ambapo Zamalek waliwachapa mabao 3-1 kikiwa ni kichapo kikikubwa kwao kwenye hatua ya makundi.

KOMBE LA SHIRIKISHO

Yanga wamemaliza wakiwa vinara wa kundi na sasa watakutana na mshindi wa pili kwenye makundi kati ya USM Alger, Pyramids FC na Rivers United FC, huku timu zote zikionekana kuwa za kawaida kwa Yanga.

Rekodi zinaonyesha kuwa kati ya timu zote ambazo zinakutana na Yanga walishakutana huko nyuma na Yanga wakachapwa na sasa wanasubiri kwa hamu kubwa wanakutana na nani ili waweze kulipa kisasi.

Tofauti na misimu mingine kwa sasa timu yenye zenye rekodi kubwa kwenye michuano hii hazijafuzu na hii inaweza kuwa nafasi kubwa kwa Yanga.

USM Alger ni vigogo kutoka nchini Algeria wakiwa na hawajawahi kutwaa ubingwa huu lakini wakiwa na rekodi ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2015, rekodi zake za msimu huu zinaonyesha kuwa siyo timu ya kutisha sana kwa kuwa kwenye michezo sita waliyocheza wamepoteza miwili wakiwa wameshinda mitatu na sare mbili, wamekuwa wanafunga lakini wanaruhusu sana kufungwa mabao ambapo wamefunga 11 na kufungwa matano jambo ambalo litakuwa gumu kwao watakapovaana na Yanga yenye, Fiston Mayela na Kennedy Musonda ambaye ameshafanya vizuri sana msimu huu, rekodi zinaonyesha kuwa wamewahi kuitupa nje Yanga kwa jumla ya mabao 4-1.

Pyramids FC hii ni kati ya timu yenye rekodi kubwa kwenye michuano ya mwaka huu ikiwa inatokea nchini Misri na inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri na sasa inaweza kukutana na kigingi Yanga.

Timu hii inaonekana imeshakutana na Yanga mara mbili na kushinda michezo yote na sasa ni zamu ya Yanga kulipa kisasi kwenye Uwanja wa Mkapa, wamekusanya pointi 11 wakiwa wamefunga mabao kumi lakini jambo la faida kwa Yanga ni kwamba hawana safu nzuri ya ulinzi baada ya kufungwa mabao sita.

Uwanja wao wa nyumbani hawana mashabiki wengi sana na wanaonekana kuwa wanaweza kubadilika kwenye hatua inayofuata wakiwa na rekodi ya kushika nafasi ya pili kwenye kombe hilo msimu wa 2019/2020.

Rivers, ni ya Nigeria haikuanza vizuri msimu huu vizuri lakini ikabadilika kwenye michezo ya mwisho ya makundi, ikiwa ndiyo timu changa zaidi kwenye michuano hii ikiwa imeanzishwa mwaka 2016.

Rivers ina rekodi ya kuwachapa Yanga kwenye michuano hii ambapo imeshakutana nao mara mbili na zote ikawachapa jambo ambalo linawapa Wanajangwani hao tahadhari kubwa watakapoanzia pale Nigeria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: