Mgaaga na upwa hali wali mkavu. Ipo hivyo, lakini kwenye anga za kimataifa, wali mkavu unaliwa kutokana na ugumu uliopo.
Simba rekodi yao ya kadi nne za njano kwenye mchezo mmoja dhidi ya Horoya, bado hawajaivunja, lakini Yanga wao nao wanapasua anga.
Hapa tunakuletea namna wababe hao wanavyopambana kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa hatua ya makundi ambapo Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga Kombe la Shirikisho Afrika.
USHAMBULIAJI
Yanga kwenye dakika 270, imekuwa ni moto anga hizi hatua ya makundi ambapo wametupia mabao manne, kila nyota ana bao mojamoja.
Mtupiaji wa kwanza alikuwa Kennedy Musonda kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe, kisha Mudhathir Yahya na Tuisila Kisinda ambao nao walifunga wakati Yanga ikishinda 3-1 dhidi ya TP Mazembe, Uwanja wa Mkapa, Dar.
Bao moja ni mali ya Fiston Mayele ambaye alifunga kwenye mchezo dhidi ya Real Bamako ugenini kwenye sare ya kufungana bao 1-1
Simba kwenye mechi tatu kimataifa ambazo ni dakika 270, bao moja wamefunga, huku mtupiaji akiwa ni Henock Inonga ambaye ni beki, ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Vipers ugenini.
Kikosi cha Simba
ULINZI
Hapa Yanga imeokota mabao manne nyavuni kwenye mchezo wa kwanza walipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya US Monastri ugenini, wa pili walishinda mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe na ule wa tatu ngoma ilikuwa Real Bamako 1-1 Yanga. Kwenye kila mchezo wametunguliwa.
Simba kwenye ulinzi walianza kutunguliwa dhidi ya Horoya bao 1-0, wakachapwa na Raja Casablanca 0-3 Uwanja wa Mkapa, kisha dhidi ya Vipers hawakutunguliwa, walishinda bao 0-1.
Yanga na Simba kila moja imetunguliwa mabao manne kwenye mechi za kimataifa hatua ya makundi.
MANULA NA DIARRA
Aishi Manula ambaye ni kipa wa Simba, anapata tabu akiwa amepata kazi ya kupigiwa penalti mbili, huku moja akiipangua dhidi ya Horoya na dhidi ya Raja Casablanca alitunguliwa. Kwenye mechi tatu hajafungwa mechi moja, ilikuwa dhidi ya Vipers.
Kipa wa Yanga, Djigui Diarra, kwenye mechi tatu katunguliwa kila mechi akiwa hajakusanya clean sheet yoyote.
MABEKI
Beki wa Simba, Henock Inonga ni yeye mwenye bao kimataifa huku Joash Onyango akiwa amesababisha penalti mbili, dhidi ya Horoya na Raja Casablanca.
WAKALI WA PASI
Aziz KI ana pasi moja ya bao dhidi ya Real Bamako, alimpa Mayele ambaye naye ana pasi moja ya bao dhidi ya TP Mazembe, alimpa Tuisila Kisinda.
Kenedy Musonda ana pasi moja ya bao, alimpa Mudhathir Yahya, bao la Musonda alitumia pasi ya Djuma Shaban.
Kwa Simba ni Moses Phiri alimpa pasi ya bao Inonga dhidi ya Vipers.
MIPIRA YA KUTENGWA TATIZO
Yanga mabao yake yote manne yametokana na mapigo huru huku Simba ikitunguliwa bao moja kwa penalti.
YANGA
Kwenye Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga ipo nafasi ya pili, ina pointi nne baada ya kucheza mechi tatu, imeshinda moja, sare moja, imetunguliwa mechi moja. Tofauti yao na vinara ambao ni US Monastri ni pointi tatu ambapo wao wamekusanya pointi saba.
Wanaoburuza mkia ni Real Bamako, wana pointi mbili, wamepoteza mchezo mmoja, kisha sare mbili, huku nafasi ya pili ikiwa mikononi mwa TP Mazembe, ina pointi tatu baada ya kucheza mechi tatu, imeshinda mchezo mmoja, ikiwa imepoteza mechi mbili.
SIMBA
Kwenye Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ipo nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi tatu, imepoza mechi mbili, ikiwa imeshinda mchezo mmoja.
Raja ni wababe wa kundi wakiwa wamekusanya pointi 9 baada ya kucheza mechi tatu na kushinda zote, wakitupia mabao 10.
Vipers wanaburuza mkia wakiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi tatu, hawajaambulia ushindi huku wakiwa wamepata sare moja na kutunguliwa mechi mbili.
KUNDI D KOMBE LA SHIRIKISHO
P W D L GF GA GD Pts
US Monastir 3 2 1 0 5 1 +4 7
Yanga 3 1 1 1 4 4 0 4
TP Mazembe 3 1 0 2 4 6 −2 3
Real Bamako 3 0 2 1 3 5 −2 2
MATOKEO & RATIBA YA YANGA
FEBRUARI 12, 2023
US Monastir 2–0 Yanga
FEBRUARI 19, 2023
Yanga 3–1 TP Mazembe
FEBRUARI 26, 2023
Real Bamako 1–1 Yanga
MACHI 8, 2023
Yanga v Real Bamako
MACHI 19, 2023
Yanga v US Monastir
APRILI 2, 2023
TP Mazembe v Yanga
KUNDI C LIGI YA MABINGWA
P W D L GF GA GD Pts
Raja CA 3 3 0 0 10 0 +10 9
Horoya 3 1 1 1 1 2 −1 4
Simba 3 1 0 2 1 4 −3 3
Vipers 3 0 1 2 0 6 −6 1
MATOKEO & RATIBA YA SIMBA
FEBRUARI 11, 2023
Horoya 1–0 Simba
FEBRUARI 18, 2023
Simba 0–3 Raja CA
FEBRUARI 25, 2023
Vipers 0–1 Simba
MACHI 7, 2023
Simba v Vipers
MACHI 18, 2023
Simba v Horoya
MACHI 31 – APRILI 1, 2023
Raja CA v Simba.