Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba: Kazi imeanza rasmi

IMG 4108 Simba Training.jpeg Simba: Kazi imeanza rasmi

Wed, 5 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya 'kula bata' kwa siku zisizopungua 20 katika maeneo tofauti, Mastaa wa Simba kuanzia jana wameanza kuwasili kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao huku wakitamba kujifua na kuhakikisha msimu ujao wanafanya vizuri zaidi ikiwemo kutwaa makombe.

Wachezaji wote wa Simba walipewa mapumziko kuanzia Juni 10, mwaka huu baada ya kumalizika kwa ligi ambapo kila mmoja alienda sehemu aliyochagua kupumzika na sasa wanarejea wakiwa wamepania kuanza kazi kwa nguvu zote katika maandalizi ya msimu ujao.

Mwanaspoti limepenyezewa, kambi ya Simba tayari imeanza jijini Dar es Salaam ambapo kikosi kitakuwa hapo kwa siku zisizopungua 10 kikisubiri kukamilika kwa kila kitu ikiwemo mastaa wapya na baada ya hapo kwa pamoja watapaa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya maandalizi kamili ya msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Saidi Ntibanzokiza 'Saido' aliyekuwa zake kwao Burundi amesema yeye tayari ameanza kazi.

"Nipo nyumbani kwa mapumziko, kipindi hiki sijacheza kabisa mpira nimekitumia kupumzika lakini siku za hivi karibuni nimeanza maandalizi ya msimu nikifanya mazoezi mepesi ya viungo ili kujiweka sawa binafasi.

Najua hivi karibuni kazi itaanza rasmi hivyo lazima niwe fiti." alisema Saido aliyejiunga na Simba dirisha dogo la msimu uliopita akitokea Geita Gold.

Kwa upande wa mshambuliaji Kibu Denis aliyekwenda kupumzika Dubai, alisema kipindi cha mapumziko sasa kimeisha na kinachofuata ni kujifua kwa ajili ya msimu ujao.

"Muda wa mapumziko umemalizika na sasa tunarejea kambini. Msimu uliopita tuliteleza lakini msimu ujao nadhani tutafanya vizuri zaidi na kila kitu kitaanzia kwenye 'Pre Season'," alisema Kibu anayesifika kwa nguvu akishambulia na kukaba.

Pamoja na hao, Mwanaspoti linajua Simba inaendelea na usajili wa majembe mapya kimya kimya ambao wataungana na waliopo ili kuhakikisha malengo yao ya msimu ujao yanatimia.

Mwanaspoti linajua tayari Simba imekamilisha usajili wachezaji wawili kutoka Cameroon, winga Leandre Onana aliyeibuka mchezaji na mfungaji bora wa Ligi ya Rwanda akiichezea Rayon Sports na kufunga mabao 17, sambamba na beki Che Fondoh

Malone kutokea Coton Sports na muda wowote watatambulishwa Msimbazi huku ikiwa imeshamtumia mkataba kipa Mbrazili Caique Luiz Santos da Purificacao, anayetarajia kutua nchini wiki ijayo akiambatana na kocha mkuu wa Simba Roberto Oliveira 'Robertinho', aliyekuwa kwao.

Aidha Simba inatafuta beki wa kushoto atakayekwenda kusaidiana na Mohamed Hussein 'Tshabalala', kiungo wa kati sambamba na mshambuliaji wa kati na wako kwenye mazungumzo na baadhi ya nyota wanaowahitaji.

Pamoja na kuendelea na usajili lakini pia Wanamsimbazi hao wameagana na nyota wake Ismael Sawadogo, Gadie Michael, Agustine Okrah, Nelson Okwa, Victor Akpan, Beno Kakolanya, Mohamed Ouattara, Erasto Nyoni na Jonas Mkude.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: