Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 100 za uongozi wa Hersi Yanga

Eng. Hersi Yanga Meeting Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said

Thu, 13 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kutimiza mwaka mmoja tangu amepewa nafasi ya kuiongoza Yanga, Rais Hersi Said amesema umekuwa na wakati mzuri na sasa ana kibarua kigumu miaka mitatu iliyobaki kuvuka mafanikio ya sasa.

Hersi alisema hayo jana baada ya kukabidhiwa mfano wa hundi ya Sh405 milioni na wadhamini wakuu wa Yanga, SportPesa, ikiwa ni bonasi baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu, Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kutinga fainali Kombe la Shirikisho Afrika.

"Mafanikio tuliyoyapata haikuwa kazi rahisi, ni mapambano makubwa yamefanyika, hivyo nafurahi kuwa na mwaka mmoja wa mafanikio, nina kazi kubwa ya kufanya kumaliza miaka mitatu iliyobaki.

"Kwa moyo mmoja kwenye mwaka wangu mmoja wa mafanikio, SportPesa ndiyo chachu ya mafanikio yetu na tunajivunia sana tunavyoona tunaitendea haki nembo yao kwa kuwapa mataji mfululizo," alisema Hersi.

Rais huyo alisema anatambua ushindani mkubwa msimu ujao kutokana na timu kuona walichokifanya, hivyo hawabweteki kwani wamefanya usajili mzuri ambao pia utatoa changamoto kwa wapinzani.

"Naona watu wanaposti sajili zao na kutamba mitandaoni, Wanayanga wasitishike kwani wanayoyafanya sisi tumeshafanya na tumesajili nyota wa kazi hasa.

"Kwa namna tulivyopata mafanikio, kwenye mashindano ya ndani na kimataifa msimu uliopita, tunahitaji jitihada zaidi ili kuvuka hatua hiyo, na kufika huko tunahitaji uwekezaji kwenye usajili," alisema.

Uongozi wa timu hiyo pia umekiri kuhitaji mafanikio zaidi ya hapo walipo sasa na wanatarajia kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutwaa taji la ligi.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa, Tarimba Abbas amewatoa hofu Wanayanga kuwa watarajie furaha zaidi msimu ujao kutokana na usajili uliofanywa na timu hiyo.

"Mimi pamoja na kuwa mdhamini nimekuwa karibu sana na uongozi wa Yanga nimeshuhudia usajili wao, natarajia mambo mazuri zaidi msimu ujao, Wanayanga muwe na amani, msiwe na wasiwasi kwenye ishu ya usajili," alisema.

"Si usajili tu, mikakati iliyonayo Yanga ni mikubwa na yenye faida kubwa kwa klabu, viongozi waliopo ni bora na kwa mafanikio haya kila mtu anajionea maana ni mwendo wa makombe tu kila msimu, kwa misimu miwili mfululizio ni matumaini yangu ushindi huu utakuwa endelevu." alisema Abbas.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: