Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sasa mtamkoma baleke

Balekeee Simbas.jpeg Straika wa Simba, Jean Baleke

Sun, 24 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jean Baleke ni mshambuliaji ambaye kazi yake kubwa ni kutumbukiza mipira nyavuni na hilo ndilo linazifanya timu nyingi kusajili washambuliaji wa kati na kuwapa jukumu la kufunga.

Alisajiliwa kwenye dirisha dogo lililopita, siyo mshambuliaji tu bali mfungaji mwenye zile tabia za kufunga kila mara. Angalia alichowafanya Coastal Union juzi kwenye Uwanja wa Uhuru. Tena aliwaambia kabla.

Kutoka kwenye Kibegi cha Ticha leo tunakuletea aina tatu za mastraika.

WACHEKI HAPA:

1. MFUNGAJI ANAYESUMBUA

Huyu humkuti sehemu moja tu, anahangaika kutafuta nafasi, anashuka kuchukua mipira na kutembea nayo kisha kufunga.

2. MFUNGAJI KAMA SANAA

Huyu kufunga kwake ni kawaida, huwezi kujua kama yupo au hayupo bali mpira ukianguka tu unamkuta keshafika na kufunga, pia kufunga kwake ni sanaa yaani anafunga wa utulivu mkubwa.

3. MMALIZIAJI

Ni mfungaji ambaye muda wote wa mpira huwa hahangaiki sana, unamkuta ndani ya 18 kila wakati huku akifunga kirahisi. Namuona Baleke katika fungu hili. Ni aina ya mshambuliaji ambaye mcheze mchezavyo yeye haadimiki sana kwenye eneo la 18 ya timu pinzani.

Baleke ni mmaliziaji mzuri kwani kazi ya kumalizia haihitaji hatua nyingi zaidi ya mguso mara moja au mbili mpira kuingia golini. Anakosa mabao mengi pale anapotumia hatua kadhaa kabla ya kumfikia golikipa kwa sababu umakini kwake hupungua zaidi hivyo kufanya uamuzi tofauti.

Mabao 8 ya msimu uliopita yalimaanisha kuwa Jean Baleke ambaye alikuja kwenye dirisha dogo atakuwa na nafasi nzuri ya kufunga mabao mengi msimu huu.

KIPI KITAMKWAMISHA BALEKE

Jinsi Baleke anavyozidi kufunga kunatoa ishara kwa timu nyingine kuwa makini kila watapocheza dhidi ya Simba na walinzi kumwangalia yeye kwa jicho la tatu.

Lakini Baleke anahitaji kujifua zaidi ili kukamilika. Ni kazi kwa mshambuliaji wa kati kuwa kamili kwa maana hii. Kwanza awe na uwezo wa kufunga kwa miguu yote miwili bila wasiwasi na awe na uwezo wa kufunga kwa kichwa mara kwa mara huku pia akiwa na matumizi mazuri ya nguvu.

Mwenye uwezo wa kupunguza walinzi wachezaji watatu wanne na kufunga huku akijiamini asilimia kubwa.

Baleke ni mshambuliaji anayekupa angalizo huko mbele kuwa anaweza kufikia rekodi zilizowekwa za ufungaji bora wa mabao kuanzia ile ya Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ ya mabao 26, Meddy Kagere (mabao 25), Hamis Tambwe (mabao 21) na wengine wengi.

Bila shaka huu ni msimu wake muhimu na kama atacheza kwa kuaminiwa basi Tanzania tutamshuhudia mshambuliaji mwingine makini na bora. Natabiri hakosi mabao 20 msimu huu.

MECHI YA COASTAL

Simba ilishinda mabao 3-0. Kuna watu waliokuwa na siku nzuri kwenye mchezo huu.

BALEKE: Mashabiki wa Simba walimwambia ‘tumekusamehe kwa mabao uliyokosa Zambia’. Mabao matatu ya mchezo huo yamemfanya afikishe matano na kuwa kinara wa ufungaji kwenye ligi hadi sasa.

MOHAMMED HUSSEIN : Muda wote alikuwa kwenye kibendera cha timu ya Coastal upande wake akishambulia na kupiga krosi 5, ikiwamo asisti ya bao la pili.

Alipanda sana kwa kuwa kule kulia kulikuwa na wachezaji chipukizi kama Cosmas Andrea, Greyson Gwalala na muda mwingine Semfuko Daud.

CLATOUS CHAMA: Ni lazima awe bora hasa anapocheza na timu inayorudi nyuma kila wakati. Alitoa asisti ya bao la kwanza baada ya kumpoka mpira mlinzi wa Coastal na kumpa pasi rahisi Baleke aliyefunga. Alikuwa huru kuchezesha timu huku akikokota mipira isiyopungua 63.

CHE MALONE: Akili ya mpira, utulivu wake, namna ya kuchukua mpira kwa utulivu bila faulo vinaendelea kumweka juu na kumfanya mchezaji tegemeo kwenye nafasi ya ulinzi.

LAMECK LAWI: Mchezaji aliyechukua tuzo msimu uliopita ya mchezaji chipukizi na kwenye mchezo huo ndiye aliyefanya kazi kubwa ya kuzuia nyendo za mwisho za wachezaji wa Simba.

IBRAHIM AJIBU: Siri ya uwezo wake kuwa bora ndani ya uwanja anayo kocha wake Mwinyi Zahera. Ajibu amerudi vyema sana ukianza na bao lake la frii-kiki alilofunga kule Manungu hadi kwenye mchezo wa juzi amekuwa bora sana.

57 - Alikuwa kinara kwenye kutembea na mpira kwa upande wa timu yake akifanya hivyo mara 57 na kupiga kona na frii-kiki nzuri.

SIKU MBAYA KWAO

DAUDI MBWENI: Mchezaji mwenye bahati mbaya ama kujifunga au kusababisha madhara langoni mwake mara kadhaa.

Aliharibu mpango kazi wa mwalimu wake mapema baada ya kulazimisha kukokota mpira kwenye eneo lake na kunyang’anywa kisha kupatikana kwa bao la kwanza la mchezo.

HENOCK INONGA: Alianza vizuri mchezo huku akifurahia kuwa na mpira kwa sababu hakuwa anapata misukosuko yoyote. Alipata ajali mbaya baada ya kukutana na mguu wa Haji Ugando wa Coastal na kumfanya awahishwe hospitalini kwa gari la wagonjwa na kubainika amechanika na sio kuvunjika kama ilivyohisiwa awali.

LOUIS MIQUISSONE: Anajitahidi sana kufanya kila awezalo ili kurudi kwenye ule ubora wake uliomfanya achukuliwe na Al Ahly ya Misri, lakini bado gari halijawaka. Anatengeneza nafasi nyingi lakini hana ile kasi yake, anakosa mabao kwa kuwa anapania zaidi kufunga.

MPAMBANO ULIVYOKUWA

Simba walitumia mfumo wa 4-2-3-1 walipokuwa wakianzisha mashambulizi lakini walibadilika na kuingia kwenye 2-3-4-1 hii ina maana walisogea na kuwaacha Che Malone na Henock huku Mohammed Hussein, Shomary Kapombe na Fabrice Ngoma wakisogea kuongeza mashambulizi na kuwafanya wale wanne yaani Chama, Saido Ntibazonkiza, Mzamiru Yassin na Luis kuongeza idadi ya wachezaji ndani ya boksi la Coastal.

Coastal walicheza mfumo wa 5-3-2 ili kuweza kuzuia vizuri huku timu karibiu yote ikishuka chini kabisa kwenye nusu na hasa baada ya mchezaji mmoja, Ugando kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Waliposhambulia kwa nadra walikuwa katika umbo la 4-2-2-1.

SIMBA HATARI DK 15-20

Rudia magoli mawili yaliyopatikana kwenye mchezo wa kwanza baina yao na Mtibwa ambapo walipata bao mbili za haraka haraka kupitia kwa Willy Onana na Baleke, juzi pia walpata bao mbili za haraka kupitia kwa Baleke. Wanachofanya Simba ni kuhama haraka kutoka kwenye mfumo mama wa 4-2-3-1 na kuingia kwenye 3-5-1-1 ambapo Chama huwa karibu zaidi na mchezaji wa juu kumrahisishia ufungaji.

DAKIKA 25 KASI ILIPUNGUA

Kuumia kwa Inonga katika ajali ya aina ile huwafanya wachezaji walioona tukio kuhamanika, hilo nalo ni jambo lililopunguza mzuka wa mechi na njaa ya kutafuta mabao.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: