Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho awatwika zigo Onana, Chama

Simba Players Chama Robertinho awatwika zigo Onana, Chama

Sun, 3 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ mjanja sana baada ya kusikia kelele na presha kutoka kwa mashabiki fasta akaamua kufanya jambo kambini kwa kuwapa kazi maalumu mastaa watano akiwamo Clatous Chama na Willy Onana ili kurahisisha mambo uwanjani.

Mbrazili huyo ameandaa silaha tano akizitengeneza katika kupiga faulo na kama haitoshi suala la upigaji penalti ameendelea kulipa kipaumbele na sasa wamekuwa na utaratibu wa kuzipiga kila wanapokuwa na programu ya mazoezi kambini kwa kujua lolote linaweza kutokea.

Katika kuhakikisha timu inakuwa na machaguo tofauti ya upigaji faulo, Robertinho amewateua Chama, Onana, Saido Ntibazonkiza, Jean Baleke na Luis Miquissone ambao yeyote anaweza kupiga kutegemea na eneo ambalo itatokea na pia kutokana na mchezaji atakayekuwepo uwanjani.

Wachezaji hao mara kwa mara Simba inapofanya mazoezi kambini, wamekuwa wakipewa programu maalumu ya upigaji wa mipira hiyo ya adhabu, ambapo Robertinho amekuwa akibadilishabadilisha makipa ikionekana analenga kuwapa uzoefu jinsi ya kuokoa mipira hiyo.

Katika upigaji wa mipira hiyo, wachezaji wamekuwa wakirudirudia katika pande tofauti ambazo ni kushoto, kulia na faulo zinazotokea katikati ya usawa wa karibu na lango ambapo mara nyingi nyota hao wamekuwa wakionyesha ustadi wa kufunga.

Uwezo wa kutumia miguu miwili kwa ufasaha umeonekana kuwapa faida zaidi Onana, Chama, Baleke na Saido kulinganisha na Luis ambaye mara kwa mara amekuwa mwiba kwa faulo akipiga na mguu wa kushoto ingawa zile anazopiga na mguu wa kulia zinaonekana kutokuwa tishio.

Hata hivyo, katika mechi mbili za Ligi Kuu ambazo wamecheza dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji, wachezaji wanaoonekana kuwa kipaumbele zaidi katika upigaji wa mipira iliyokufa ni Chama na Saido ambao hata msimu uliopita ndio walikuwa wakitumika mara kwa mara.

Lakini mbali na hilo, wachezaji wa Simba wamekuwa wakifanya mazoezi ya upigaji penalti mara kwa mara ikionekana ni kuwapa uzoefu zaidi iwapo watakutana na mechi itakayolazimika kuamriwa kwa mikwaju ya penalti kama ilivyotokea katika Ngao ya Jamii jijini Tanga, mwezi uliopita.

Katika mashindano hayo Simba iliibuka na ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Singida Big Stars na kushinda kwa penalti  3-1 dhidi ya Yanga kwenye fainali.

Kocha Robertinho alisema kuwa anataka timu iwe bora kiufundi katika nyanja nyingi tofauti za kiufundi ndani ya uwanja akiamini hiyo ni silaha ya kufanya vizuri.

“Tunahitaji kuwa na timu inayofunga kwa staili tofauti kwani kuna mechi ambazo utahitaji kupata mabao kupitia faulo na penalti, lakini pia kuna michezo ya mtoano ambayo mshindi atalazimika kupatikana kwa kupigiana penalti. Tukiwa tumejiandaa inakuwa vizuri,” alisema Robertinho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: