Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho ampa kazi Mtunisia

ROBERTINHO SAD Robertinho ampa kazi Mtunisia

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Leo kikosi cha Simba kinatarajia kusafiri kwenda nchini Guinea kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Horoya AC ya nchini humo utakaopigwa Februari 11, mwaka huu huku kocha mkuu wa Wekundu wa Msimbazi hao, Robertinho akitambia ubora wa wasaidizi wake katika benchi la ufundi.

Robertinho ambaye ni raia wa Brazil, amesema licha ya kuwa na wachezaji bora na kikosi kipana lakini kazi kubwa imekuwa ikifanywa na benchi lake la ufundi lililosheheni wataalamu tofauti huko akiwataja makocha wasaidizi, Juma Mgunda na Mtunisia Ounane Sellami.

Mbrazili huyo amesema anatambua ubora wa Mgunda na anafurahi kufanya naye kazi lakini pia alimuongeza Oanane kwa kazi maalumu kwani amebobea kwenye kuwasoma wapinzani na kuleta mabadiliko ya papo papo wakati mchezo unaendelea jambo litakaloisaidia timu kwenye mechi zijazo hususani Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Bado imani yangu ya kufika nusu fainali na hata fainali ni kubwa sana, na hili silifanyi peke yangu ndio maana unaona nilimuongeza Ounane kikosini, pia yupo Mgunda, wote hao ni wataalamu na kila mmoja anakazi yake sambamba na wataalamu wengine kwenye benchi.

Kwa pamoja tunajenga timu itakayotisha Afrika, ukizingatia katika hatua ya makundi timu tunazokutana nazo ni kubwa hivyo lazima kila mmoja afanye kile anachokiweza kwa asilimia zote ili tuvuke hapa," alisema Robertinho na kuongeza;

"Vipers ninawajua vizuri kwani nimetoka huko na mimi ndiye niliwafikisha Makundi, Mgunda pia anawajua vyema kwani ni ukanda wa Afrika Mashariki na soka la ukanda huu kwa kiasi flani linafanana, hivyo hivyo kwa Raja Casablanca, Ounane anawafahamu vyema na wanatoka ukanda mmoja na soka lao ni sawa na hawa Horoya kwa pamoja tumewasoma na tunajua wanachezaje hivyo tunajiandaa ili kuwafunga," alisema Robertinho.

Mwanaspoti katika mazoezi tofauti tofauti ya Simba iliyoshuhudia, ilimuona Robertinho muda mwingi akiwaachia Mgunda na Ounane kazi ya kuwapigisha matizi mastaa wa kikosi hicho, huku yeye akikaa pembeni na kutizama na kila baada ya muda mfupi alikuwa akiweka kikao na wawili hao kisha kujadili mambo na kuendelea na mazoezi.

Simba imekuwa ikifanya vizuri kwenye michuano ya CAF kwa na katika misimu minne iliyopita imefika mara mbili robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na mara moja Kombe la Shirikisho Afrika na lengo lao kuu msimu huu ni kuvuka hapo na kufika nusu fainali.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: